May 17, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Zuio la mawakala lawaliza wapinzani

Spread the love

WAGOMBEA wa vyama vya upinzani katika Uchaguzi Mkuu nchini Tanzania unaofanyika leo Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020 wamelalamikia dosari zinazojitokeza kwenye uchaguzi huo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Dosari ambazo hado sasa zimelalamikiwa ni mawakala wa vyama vya upinzani kukwama kuingia kwenye vituo vya kupigia na baadhi ya masanduku ya kura kuwa na kura za kughushi ndani yake.

Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema, kuna changamoto ya mawakala wa chama hicho katika baadhi ya maeneo kuzuiwa kuingia vituoni.

“Ripoti za uchaguzi zinaonyesha kasoro zilizoenea kwa njia ya kuzuia mawakala wetu wa kusimamia uchaguzi kuingia kwenye vituo vya kupigia kura,” amesema Lissu

Mbali na Lissu, Mgombea Urais wa Tanzania wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba amesema, kitendo cha baadhi ya mawakala kuzuiwa kuingia katika vituo vya kupigia kura haiashirii hali nzuri na kuiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuingilia kati suala hilo.

“Kuna taarifa mawakala wamezuiwa, hili suala haliashirii hali nzuri, lakini nitoe wito kwa tume kuangalia wasimamizi waweze kusimamia vizuri watende haki, mawakala waruhusiwe waweze kushiriki kikamilifu, muhimu tumalize zoezi hili kwa amani,” amesema Prof. Lipumba.

Prof. Lipumba amesema “Tusubiri matokeo ya uchaguzi tuwe wavumilivu, tusiingie kwenye machafuko. Suala la demokrasia ni mchakato.”

Naye Mgombea Ubunge Kigoma Mjini kupitia ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema “Tumekamata kura ambazo zimeshapigwa katika Jimbo langu la Uchaguzi. Tutazuia kila mbinu yao chafu. Kila mbinu yao chafu.”

Halima Mdee, Mgombea ubunge Kawe kwa tiketi ya Chadema akikwaruzana na msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo

Mgombea Ubunge Mbeya Mjini kupitia Chadema, Joseph Mbilinyi maarufu ‘Sugu’ amelalamikia kitendo cha mawakala wake kuzuiwa kuingia katika vituo takribani 10 vya uchaguzi jimboni humo.

Amesema mawakala wengi walizuiwa kuingia vituoni kwa kigezo cha kutokuwa na barua huku akitupia lawama kwa mamlaka husika kuhusu changamoto hiyo akisema walichelewa kuwapa barua za utambulisho mawakala wake.

“Kwa ripoti ya asubuhi, takribani mawalaka wa vituo 10 walizuiwa na wengine kuruhusiwa baada ya masaa mawili kupita. Tunataka tujue vituo vingapi vimechelewa ili tuviangalie vizuri,” amesema Sugu.

Naye Mgombea Ubunge wa Kawe jijini Dar es Salaam kupitia Chadema, Halima Mdee mapema leo alidai kukamata masanduku ya kura yakiwa na kura za kughushi.

Wagombea Ubunge wa Kinondoni, Saed Kubenea (ACT-Wazalendo), Susan Lyimo (Chadema) wamelalamikia mawakala wao katika baadhi ya maeneo kuzuiwa.

Mchungaji Peter Msigwa, mgombea Ubunge Iringa Mjini kupitia Chadema amesema, mawakala wake walizuiwa kuingia mida ya asubuhi lakini baadae waliruhusiwa wakati shughuli ya upigaji kura ikiendelea.

Nacho Chama cha ACT-Wazalendo kimelalamika mawakala wake kuzuiwa kuingia katika vituo vya kupigia kura kwenye baadhi ya maeneo.

Taarifa ya chama hicho inaeleza Jimbo la Musoma Vijijini Mkoa wa Mara, mawakala tisa wa Kata ya Etaro wameondolewa katika vituo kwa madai ya kutokuwa na kazi za chama.

“Jimbo la Masasi hadi sasa mawakala wetu 53 wamekataliwa kwa sababu za kukosa kitambulisho. Kata ya Chanika Nguo (13), Jida (24), Mumbaka(16). Tunaendelea kufuatilia kata zingine za jimbo hilo,” inaeleza taarifa ya ACT-Wazalendo.

Semistocles Kaijage, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Tanzania (NEC)

Mgombea Ubunge wa Kinondoni kupitia NCCR-Mageuzi, Mustafa Muro amesema, maeneo mengi ya vituo, mawakala wamezuiwa kupiga kura na baadhi ya maeneo, maboksi yameonekana kuwa na kura kabla ya shughuli ya uchaguzi kuanza asubuhi.

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage amesema, tume inaendelea kufuatilia kile kinachoendelea katika uchaguzi huo ikiwemo masanduku ya kura yanayoripotiwa katika majimbo ya Kawe-Dar es Salaam, Pangani-Tanga na Buhigwe mkoa wa Kigoma.

Jaji Kaijage amesema, taarifa hizo hazina ukweli kwani wao kama NEC hawajapokea taarifa zozote za “madai hayo hazijathibitishwa na tume tunawaomba wananchi ipuuze taarifa hizo.”

error: Content is protected !!