ASKARI wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Denis Urio, amedai hakuamini kama Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, anaweza kufanya vitendo vya kigaidi kwa kuwa hana historia hiyo, lakini baadae alibaini kwamba alikuwa amedhamiria. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Luteni Urio ametoa madai hayo leo Jumatatu, tarehe 31 Januari 2022, akitoa ushahidi wake katika kesi ya uhujumu uchumi namba 16/2021, inayomkabili Mbowe na wenzake watatu, katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam, mbele ya Jaji Joachim Tiganga.
Ni baada ya Wakili wa utetezi, Peter Kibatala kumhoji kwa nini hakuieleza mahakama hiyo tarehe ambayo Mbowe alimueleza nia yake ya kupanga njama za kufanya vitendo vya kigaidi.
Na tarehe ambayo aliripoti njama hizo kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI) Robert Boaz na aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha (RCO), ACP Ramadhan Kingai.
Ambapo Luteni Urio alijibu akidai hakumbuki.
Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni waliokuwa makomando wa JWTZ, Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya, ambao wanakabiliwa na mashtaka sita ya ugaidi, ikiwemo kutaka kudhuru viongozi wa Serikali walioonekana kikwazo kwa vyama vya siasa vya upinzani.
Mahojiano kati ya Wakili Kibatala na Luteni Urio yalikuwa kama yafuatavyo;
Kibatala: Ni kweli kwamba matukio haya ya kukutana na mtu ambaye ulikuwa na uhusiano naye wa karibu akakwambia mipango ya kufanya vitendo vya ugaidi, ni kitu kizito kimetokea mara ya kwanza katika maisha yako ya utumishi wa umma?
Shahidi: Kuambiwa sijawahi
Kibatala: Utakubaliana na mimi ni kitu fulani kina uzito wa kipekee katika maisha yako?
Shahidi: Sahihi kina uzito wa kipekee
Kibatala: Nakumbuka ulitoa ushahidi kwamba hauna matatizo yoyote ya kumbukumbu?
Shahidi: Sina matatizo yoyote ya kumbukumbu
Kibatala: Shahidi naomba utusaidie, inawezekana vipi usikumbuke tarehe za muhimu mbili ambazo ziko central kwenye suala lote hili.
Tarehe mahususi ya kuongea na Mbowe akakwambia mambo mazito na tarehe ya kwenda ofisini kwa DCI kumpa taarifa nzito namna hii, inakuwaje unashindwa kukumbuka?
Shahidi: Mheshimiwa Jaji kwanza Mbowe namfahamu, lakini sikuamini anaweza kufanya kitu kama hicho, ndio maana nikaenda kuripoti polisi inawezekana kweli au si kweli, na-asume anaweza kufanya kweli, nilipojiridhisha nilijua ilikuwa serious
Kibatala: Jibu swali langu inawezekana matukio kama haya huwezi kukumbuka?
Shahidi: Sijawahi kusikia matukio hayo, ndio maana nikaenda kuripoti kama kufanya uchunguzi polisi wakafanya uchunguzi, ndio ukamataji ukaendelea
Kibatala: Inawezekana vipi ushindwe kukumbuka matukio muhimu kama hayo?
Shahidi: Mara ya kwanza kupata taarifa kama hizo kwa Mbowe sikuamini kama kitatokea kitu kama hicho, nikaripoti, kama kungekuwa na historia nyingine au kuwa na rekodi ningeamini, lakini hana rekodi hiyo
Kibatala: Kuripoti DCI ni tarehe muhimu kwa nini hukumbuki?
Shahidi: Siwezi kukumbuka sababu sio duty yangu kupeleleza, mimi nilienda kutoa taarifa ya uhalifu
Kibatala: Unaweza kueleza kwa nini hata DCI katika maelezo yake kwenye bando la Committal hafahamu tarehe mahususi?
Shahidi: Sifahamu
Kibatala: Kwa nini hata ACP Kingai katika maelezo yake naye hakumbuki tarehe mahususi ambayo wewe umeenda ripoti kwa DCI, unaweza tusaidia kujua ni kwa nini?
Shahidi: Sijui kwa nini
Kibatala: Kwa nini pia Inspekta Swilla ambaye maelezo yake tumepewa naye hakumbuki tarehe mahususi, isipokuwa tarehe ya kufungulia kesi 18 Julai 2020, unaweza fahamu kwa nini?
Shahidi: Sifahamu
Kibatala: Hii hali Luteni unaiona ya kawaida? Wewe hukumbuki uliyeenda kuripoti kwake, DCI hakumbuki, ACP Kingai hakumbuki, Inspekta Swilla aliyekufanyia upelelezi na kuchukua simu zako hakumbuki, unaona ni hali ya kawida?
Shahidi: Siwezi kujibia chombo cha polisi
Kibatala: Unaona ni hali ya kawaida?
Shahidi: Nimeenda kwenye ofisi ya mtu suala la ku-take note, kutoku-take note siwezi kumlazimisha
Kibatala: Kwa nini kama kweli Inspekta Swilla anavyodai alifungua faili tarehe 18 Julai la tuhuma za kula njama za kufanya vitendo vya ugaidi, shtaka linalohusisha zaidi ya mtu mmoja, unaweza kutusaidia kwa nini alisubiri mpaka angalau mwezi mmoja baadae tarehe 11 Agosti 2020 aliandika maelezo yako ambayo yalitumika kuanzisha jalada, unafahamu kwa nini maelezo yako yamekuja kundikwa tarehe 11 Agosti 2020?
Shahidi: Sifahamu
Kibatala: Katika hali ya kawaida sababu sio afisa wa polisi ni mtu mwenye upeo fulani, sio kitu cha busara na ambazo kinategemewa kwa watu wanaofahamu majukumu yao kurekodi taarifa za uhalifu mapema iwezekanavyo, nataka tathmini yako, huoni kwamba inategemea maelezo ya mtu muhimu kama mtoa taarifa yaandikwe mapema?
Shahidi: Sifahamu sababu ni taasisi mbili tofauti, ataandika muda gani ni juu yake yeye
Luteni Urio anaendelea kutoa ushahidi wake mahakamani hapo.
Katika ushahidi wake mkuu, Luteni Urio alidai Julai 2020 alikutana na Mbowe kisha mwanasiasa huyo akamuomba amtafutie makomando wa JWTZ waliofukuzwa ama kustaafu jeshini, ili wamsaidie katika harakati za chama chake kuchukua dola kwa gharama yoyote.
Ikiwemo kuzua taharuki kwa jamii kwa kuchoma vituo vya mafuta na kulipua maeneo yenye mikusanyiko ya watu, kukata miti iliyoko maeneo ya barabarani na kupanga magogo barabarani.
Luteni Urio anadai aliripoti njama hizo za Mbowe kwa DCI Boaz ambapo alimuelekeza atekeleza ombi la mwanasiasa huyo la kumtafutia makomando kisha aripoti mwenendo wake kwa ACP Kingai.
Leave a comment