September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lissu kukamatwa?

Robert Katula, mdhamini wa Tundu Lissu akitoka mahakamani

Spread the love

OMBI la kutaka mahakama itoe hati ya kukamatwa Tundu Lissu, mshitakiwa wa nne katika kesi ya tuhuma za uchochezi inayowakabili pia wahariri wawili wa gazeti la MAWIO, litasikilizwa tarehe 10 Machi mwaka huu. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Lakini wakati mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam inapanga siku ya kusikiliza ombi hilo leo imezidi kuhimiza kutimizwa kwa maelekezo yake kwa wadhamini wa Lissu kumleta mshtakiwa huyo kama ilivyoelekeza tarehe 20 Januari 2020, kesi iliposikilizwa mara ya mwisho.

Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba amesema mahakamani leo kuwa ombi la hati ya kukamatwa Lissu ambaye ni mshitakiwa wa nne, ni ombi mahsusi lenye jalada lake, mbali na jalada linalohusu kesi ya msingi.

“Ndio maana nasema kwamba haya mambo ni tofauti na hili la ombi haliwezi kuisimamisha kesi hii ya msingi ambayo inatakiwa iendelee na amri zake zote ni halali na hazibadiliki labda ikitokea lazima kufanya hivyo… wadhamini mkumbuke msikae mkadhani hili la kumleta mshitakiwa linasimama maana tumekubaliana hivyo,” alisema baada ya upande wa mashitaka kuomba “muda wa kutosha” wa kuandaa hati ya kiapo ya majibu ya kiapo cha waleta ombi.

Wankyo Simon aliyewakilisha upande wa mashitaka, ameiambia mahakama kuwa wanahitaji muda zaidi wa kushughulikia alichokiita “hati kinzani” kuhusu maelezo yaliyomo kwenye hati ya kiapo ya wadhamini wa Lissu.

Wakili Wankyo amesema hati ya kiapo ya wadhamini ina mambo mengi yanayohitaji kufanyiwa kazi kwa utulivu mkubwa.

Maelezo hayo yalikuja wakati ilionekana kama mahakama ingeliita shauri hilo Jumatatu ijayo kutokana na ombi la Peter Kibatala, aliyetajwa leo kuwa amenuia kumwakilisha Lissu katika usikilizaji wa ombi la hati ya kukamatwa Lissu.

Kibatala amekuwa wakili wa washitakiwa Jabir Idrissa, wa kwanza na Simon Mkina wa pili, tangu kesi Na. 208 ya mwaka 2016 ilipofikishwa mahakamani Juni 2016. Leo Kibatala hakuwepo mahakamani; akasemewa na wakili Rweikiza Rwekamwa kuwa anahudhuria kwenye kesi Mahakama ya Rufaa Tanzania jijini Dar es Salaam inayosikilizwa na majaji watatu.

Wakili Rwekamwa katika kesi hiyo ambayo imekwama usikilizwaji kutokana na kutokuwepo kwa Lissu tangu Septemba 2017 aliposhambuliwa kwa risasi akiwa jijini Dodoma kwa ajili ya shughuli za Bunge, anamwakilisha Ismail Mehboob, mashitakiwa wa tatu.

Hakimu Mkazi Mwandamizi Simba ameahirisha kesi mpaka tarehe 10 mwaka huu huku akisisitiza kuwa amri zote za awali zikiwemo za dhamana kwa washitakiwa wote, zinaendelea. Tangu awali, washitakiwa ambao walikana mashitaka yote matano, walidhaminiwa.

Siku hiyo, mahakama itaanza kusikiliza ombi la wadhamini wa Lissu ambaye amekuwa nje ya nchi,

Lissu, Jabir na Mkina wanakabiliwa na mashitaka matatu: La kwanza la kuandika habari ya uchochezi yenye kichwa cha habari Maafa yaja Zanzibar; pili ni kuchapisha habari hizo kwa lengo la kueneza chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Shitaka la tatu la kuchapisha gazeti la MAWIO la Januari 13, 2016 na la nne la kuchapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti wa Serikali, yanamhusu Mehboob ambaye ni Meneja wa kampuni ya uchapishaji ya Flint.

Shitaka la tano la kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar ili wasiweze kuingia kwenye uchaguzi wa marudio linawahusu washitakiwa wote.

Kuliibuka hoja ya kutokuwepo mahakamani kwa Mkina pale Wankyo alipoiomba mahakama kuelekeza kuwa mshitakiwa huyo afike kwa kuwa hakuwepo na wadhamini wake pia hawakufika. Wakili Nyaronyo Kicheere akimwakilisha alieleza kuwa ana hali mbaya kiafya tangu jana baada ya kufika lakini akapata ugonjwa kabla ya kesi kuanza.

Lissu alikuwa chanzo cha habari husika wakati huo akiwa Mbunge wa Singida Mashariki na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Jabir aliandika habari hiyo huku Mkina akiwa Mhariri wa gazeti hilo kupitia kampuni yake ya Victoria Media Services (VMS).

MAWIO kwa sasa halichapishwi kwa kuwa serikali haijajibu ombi la leseni mpya baada ya amri ya kulifungia iliyotolewa na serikali mwaka 2017, kutenguliwa na Mahakama Kuu mwaka mmoja baadaye.

error: Content is protected !!