CHAMA Cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) kimeiomba Serikali ianze kutekeleza dhana ya maridhiano mapema kabla ya kubandika kwenye matangazo kuwa wameridhiana kumbe si kweli. Anaripoti Mwandishi Wetu, Morogoro…(endelea).
Makamu Mwenyekiti CHADEMA Tundu Antipas Lissu alisema hayo jana tarehe 7 Mei 2023 wakati akizungumza na wakazi wa Morogoro Mjini ambapo aliwataka wananchi kushirikiana.
Amesema anashangaa kuona mabango yaliyoandikwa kwamba wameridhiana ilihali wao (Chadema) hawayajui na hawajawahi kufanya maridhiano.
Alisema maridhiano kwao ni nafasi pekee ya kuonesha wao walitaka nini na kinafanyika nini lakini kwa sasa hakuna hayo.
Alisema walishaandika mapendelezo ya maridhiano na kuyakabidhi lakini mpaka sasa hayajafanyiwa kazi.
“Tunachokiona kwa sasa ni picha zetu kuwemo kwenye mabango kuwa tumeridhiana, kivipi, wapi tumeridhiana, kuridhiana ni utekelezaji wa mapendekezo tuliyotoa na sio kuwekana kwenye picha ” alisema Lissu.
Akizungumzia katiba mpya Lisu alisema hadi kufikia mwaka wa uchaguzi 2025 ikiwa katiba mpya bado haijatoka hapatakalika.
Alisema katiba mpya ndio itasaidia kupata viongozi thabiti wataochaguliwa kupitia uchaguzi sahihi na wakiikosa ni wazi kwamba wataenda kwenye uchaguzi mgumu kama uliopitishwa mwaka 2020 ambapo wagombea wao walikatwa na kupitishwa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hivyo Lissu alliwataka wananchi kudai katiba mpya yenye mfumo mpya wa uchaguzi na haki zao.
Aidha, aliyewahi kugombea Ubunge Jimbo la Morogoro mjini CHADEMA, Devotha Minja
amewaomba wananchi kushirikiana nae kwenda mahakama kuu kufungua kesi ya kudai viwanda sababu kwa vimejengwa kwa jasho la wananchi ambao ndio walipakodi na kufungwa kwake kunahatarisha maisha ya wakazi wa Morogoro ambao walivitegemea kwa ajili ya kujikimu.
“Miaka ya 1990 Morogoro ilikuwa ni vifijo na vigeregere kwa kufanya kazi kwenye viwanda, kulikuwa na viwanda vya kutosha ilikuwa huwezi kupata mdada wala mkaka wa kazi lakini kwa sasa vijana wanapishana tu vijiweni, twende tukadai viwanda vyetu” alisema Minja.
Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mlimba, Susan Kiwanga aliwataka wananchi wakiwemo wanawake kubadilika na kuipigia kura CHADEMA kwenye uchaguzi mkuu ujao ili waepukane na adha ya kulipia gharama za matibabu wakati wa kijifungua kwa kawaida au kwa upasuaji.
“Tangu mwaka 1960 CCM inasema huduma za mama na mtoto ni bure lakini mpaka sasa hakuna ukweli huo watu wanalipisha kila huduma wanayopewa sambamba na wanaofanyiwa upasuaji kulipishwa Sh 300,000, hiyo sahihi” alisema Kiwanga
Leave a comment