TUNDU Lissu, mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Demokraisa na Maendeleo (Chadema) amesema, kesho Jumanne tarehe 29 Septemba 2020 hatokwenda mbele ya Kamati ya Maadili ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Anaripoti Mwandishi Wetu, Serengeti … (endelea).
Amesema, tume hiyo inapaswa kwanza kuzingatia Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2020.
Lissu amesema hayo leo jioni Jumatatu tarehe 28 Septemba 2020 wakati akihutubia mkutano wa kampeni za urais Jimbo la Serengeti Mkoa wa Mara.
Kauli hiyo ya Lissu inakuja ikiwa ni siku moja imepita tangu, Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC, Dk. Wilson Mahera kuutangazia umma juu ya tuhuma za uvunjivu wa maadili uliofanywa na Lissu.
Soma zaidi:-
Dk. Mahera akizungumza na waandishi wa habari jana Jumapili jijini Arusha alisema Lissu anatuhumiwa kusema uongo dhidi ya Dk. John Magufuli, mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alisema, Lissu ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho-Bara, alisema Dk. Magufuli aliitisha kikao cha wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo yote nchini, jijini Dodoma kwa ajili ya kupanga mikakati ya kuhujumu uchaguzi.
Dk. Mahera alisema, wamemwandikia barua Lissu ili kufika mbele ya kamati hiyo tarehe 29 Septemba 2020 (kesho) kujieleza na kutoa ushahidi juu ya kauli hizo.

Hata hivyo, Lissu akihutubia mkutano mkubwa wa kampeni Jimbo la Serengeti leo Jumatatu amesema “hapa nilipo mpaka sasa hivi (ilikuwa saa 9.55 jioni), sijaletewa au kuambiwa na Tume kuna malalamiko yoyote yaliyopelekwa na mgombea yeyote, tume, serikali au chama kilichoweka mgombea kwamba mimi nimekiuka maadili, wanatakiwa kuniletea kwa maandishi.”
Lissu akitumia kitabu cha maadili ya uchaguzi amesema, “hakuna malalamiko ya maandishi kutoka chama au tume aliyoyasema mkurugenzi au kuniletea na kwa sababu hiyo, siwezi kwenda na sitakwenda Dodoma kesho.”
“Ile kauli ya mkurugenzi wa uchaguzi ni kauli ya mtandaoni kama zilivyo kauli za mtandaoni zingine na kwa sababu hakuna malalamiko yoyote mpaka sasa, sitakwenda Dodoma,” amesema Lissu huku akishangiliwa
“Kama kuna mtu alikuwa anafikiria kuna tatizo, nawatoa hofu kwamba hakuna tatizo lolote na kama kuna tatizo waniletee mimi, wasiyapeleke kwenye chama, nyumbani kwangu, waniletee mimi kwa sababu mimi ndiye mgombea na wasipofanya hivyo tunasonga mbele,” amesema.

Lissu amesema, maadili ya uchaguzi yanayoongoza uchaguzi huo, yanazungumzia utaratibu wa kushughulikia malalamiko sehemu ya tano kifungu cha 5.7(c) kinasema.
“Baada ya kupokea malalamiko, kamati itamtaka anayelalamikiwa kuwasilisha utetezi wake kwa maandishi ndani ya saa 48 tangu kupokea taarifa ya malalamiko dhidi yake.”
Katika hilo, Lissu amesema “kwa maana hiyo, safari ya mimi kwend Dodoma bado iko mbali sana, wakiniletea malalamiko hayo, nikiwapelekea maandishi ndiyo watajua kuna kikaokipo au watalegea.”
“Wanaofikiria mgombea huyu atatishwa na tume, hawanijui, hawanijui, hawanijui na niwatoe wasiwasi watu wangu, hakuna habari ya kwenda Dodoma kesho na kama itakuwepo wafuate maadili waliyoyatunga wao wenyewe ikiwemo kunipa saa 48 kuwasilisha utetezi wa tuhuma ninazokabiliwa nazo,” amesema.
Leave a comment