Sunday , 5 February 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Lissu aeleza machungu ya 2020
Habari za Siasa

Lissu aeleza machungu ya 2020

Tundu Lissu, Mgombea Urais Tanzania kwa tiketi ya Chadema
Spread the love

TUNDU Lissu, aliyekuwa Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020, amesema mwaka huo ulikuwa mchungu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Lissu amesema hayo jana Alhamisi tarehe 24 Desemba 2020, wakati akitoa salamu zake za Siku Kuu ya Noel (Krismasi), kwa Watanzania.k

Makamu mwenyekiti huyo wa Chadema Bara,  amesema uchungu wa mwaka 2020 ulichangiwa kwa kiasi kikubwa na Uchaguzi Mkuu, akidai kuna baadhi ya watu walipoteza maisha na kujeruhiwa katika mchakato wa uchaguzi huo.

Pia, amedai baadhi ya wananchi walipokwa haki yao ya kuchagua, hata hivyo, tuhuma za vyombo vya usimamizi wa uchaguzi kuendesha uchaguzi huo kinyume na sheria, zilikanushwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ambapo ilisema iliendesha mchakato wake katika misingi ya haki na usawa.

Tundu Lissu, Mgombea Urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chadema

“Mwaka 2020 ulikuwa mwaka mgumu na wenye machungu mengi kwa nchi yetu na kwa wananchi wetu. Wote tulishuhudia haki yetu ya kuchagua viongozi tunaowataka ikipokwa kwa kutumia vyombo vya usimamizi wa uchaguzi. Wapo ambao ndugu zao waliuawa au waliojeruhiwa na kulemazwa  wakati wa Uchaguzi Mkuu na hata kabla ya hapo,” amedai Lissu.

Akitoa tathimini ya uchaguzi huo tarehe 19 Novemba 2020,  jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Simon Sirro alisema raia wawili na Askari Polisi mmoja, walipoteza maisha visiwani Zanzibar.

Na wananchi wawili walipoteza maisha kwa kupigwa risasi, Tarime Vijiji mkoani Mara, wakati wa mchakato wa uchaguzi huo.

Vilevile, IGP Sirro alisema katika mchakato wa kampeni za uchaguzi huo, kuliibuka vurugu maeneo ya Ukerewe mkoani Mwanza.  Mara, Songwe, Kusini Pemba na Kaskazini Pemba visiwani Zanzibar.

Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi nchini, alisema Kaskazini Pemba wananchi kadhaa walikatwa mapanga msikitini, kutokana na vurugu za uchaguzi

Kufuatia vurugu hizo, IGP Sirro alisema Jeshi la Polisi liliwakamata watu zaidi ya 250, kwa tuhuma mbalimbali kuhusiana na uchaguzi huo.

Huku akiahidi kufanya uchunguzi dhidi ya Askari Polisi waliotuhumiwa kukiuka haki za binadamu, wakati wa uchaguzi huo.

Akielezea zaidi machungu ya 2020, Lissu amesema baadhi ya wananchi waliugulia kwa kukosa ajira.

“Aidha wapo, kwa mamilioni mengi, wanao sononeka kimya kimya kwa sababu ya kutokupatiwa ajira, au kutokulipwa mishahara au pensheni zao halali au kutotendewa haki zao nyingine mbali mbali,” amesema Lissu.

Lissu amedai kuwa, mwaka 2020 yeye na baadhi ya wanasiasa, walikimbia nchi kutokana na vitisho juu ya usalama wa maisha yao.

Mwanasiasa huyo  alirudi nchini Ubelgiji tarehe 10 Novemba 2020, baada ya kudai kupewa vitisho vya mauaji kutoka kwa watu wasiojulikana.

Lissu alirejea Ubelgiji alikokuwa anaishi kabla ya kurudi Tanzania tarehe 27 Julai 2020, kwa ajili ya kushiriki uchaguzi mkuu.

Makamu huyo mwenyekiti wa Chadema aliishi Ubelgiji kwa zaidi ya miaka miwili, alikokuwa anapatiwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana jijini Dodoma, mwezi Septemba 2017.

“Wengine, kama mimi mwenyewe, wamelazimika kuikimbia nchi yetu kwa sababu ya njama na vitisho vya mauaji dhidi yao,” amedai Lissu.

Mwanasiasa mwingine aliyeondoka nchini baada ya Uchaguzi Mkuu, ni aliyekuwa Mgombea Ubunge Arusha Mjini kupitia Chadema, Godbless Lema, aliyepata hifadhi nchini Canada pamoja na familia yake.

Baada ya wanasiasa hao kuondoka nchini, IGP Sirro aliwaita warudi Tanzania akiwaahidi  kwamba atawapa ulinzi.

Kutokana na machungu hayo, Lissu amewaomba Watanzania wasikatishwe tamaa , kwa kuwa ipo siku watapata faraja.

“Kwa wote hawa wenye njaa na kiu ya haki, ujumbe wangu wa Krismasi ni ule ule alioueleza mwandishi wa riwaya wa Kimarekani, Taylor Caldwell ‘Hatuko peke yetu. Hata usiku unapokuwa wa giza zaidi, au upepo wa baridi kali, au ulimwengu unapoonekana kutokujali kabisa.’ Hatuko peke yetu,” amesema Lissu.

Mwanasiasa huyo amesema wiki ijayo atazungumza na Watanzania, kuhusu mikakati yake kuelekea mwaka mpya wa 2021.

“Msivunjike moyo au kukata tamaa. Wiki ijayo, katika salamu zangu za mwaka mpya, nitazungumza kwa kirefu kidogo  juu ya majukumu yetu kwa mwaka ujao na masuala mengine,” amesema Lissu.

1 Comment

  • Asante ndugu lissu na kupongeza kwa kukubari kushindwa pia na kusifu kwa kukimbia fedhea lakini umekubari lawama ndani ya chadema na ukuwaonea haya wa uruma wapiga kura wako ndugu lissu baada muda sio mrefu uishsngae utakapo nya nyaswa na kubangali kwa sababu ya kikosa rangi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Prof. Muhongo aungana na wananchi ujenzi maabara za sekondari

Spread the loveMBUNGE wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo, kwa kushirikiana na...

Habari za Siasa

CCM apiga marufuku wazazi kuwatumia watoto wa kike kwenye mambo ya kimila

Spread the loveKATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Daniel Chongolo...

Habari za Siasa

Ofisi za mabalozi wa mashina zitumike kuwale vijana kimaadili – Chongolo

Spread the loveKATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo ameagiza...

Habari za Siasa

Vijana ACT-Wazalendo Dar wampa tano Rais Samia

Spread the love  NGOME ya Vijana ya Chama cha ACT-Wazalendo, kimempongeza Rais...

error: Content is protected !!