November 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Magufuli awatakia Watanzania Heri ya Krismas

Rais John Magufuli

Spread the love
RAIS wa Tanzania, Dk. John Magufuli ameungana na Watanzania kuadhimisha siku ya kuzaliwa Yesu Kristo, kwa kusali Misa Takatifu ya Krismasi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Misa hiyo imefanyika leo Ijumaa tarehe 25 Desemba 2020, katika Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Imakulata,  Chamwino mkoani Dodoma.

Kwa mujibu wa taarifa ya Gerson Msigwa, Mawasiliano ya Rais, misa hiyo iliongozwa na Paroko wa Parokia hiyo Padre Paul Mapalala.

“Rais Magufuli amewapongeza na kuwatakia heri Watanzania wote kwa sikukuu ya Krismasi na amewataka kuendelea kumshukuru Mungu kwa miujiza na upendo mkubwa anaolitendea Taifa la Tanzania,” inaeleza taarifa ya Msigwa.

Katika misa hiyo, Rais Magufuli amesema upendo na miujiza ya Mungu kwa Tanzania, inajidhihirisha katika kipindi hiki ambapo Dunia inapita katika wakati mgumu wa janga la ugonjwa wa Korona (Covid-19).

Ambapo maelfu ya watu wanaendelea kupoteza maisha kila siku, lakini Tanzania imeepushwa na janga hilo na maisha ya Watanzania yanaendelea kama kawaida.

Rais Magufuli ametoa wito kwa viongozi wa Mataifa mbalimbali duniani, kumweka Mungu mbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Korona, badala ya kutegemea nguvu za binadamu pekee.

error: Content is protected !!