May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ligi Kuu Tanzania Bara kurejea leo

Kikosi cha timu ya Namungo FC

Spread the love

 

LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), iliyokuwa imesimama kupisha kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) ya michezo ya kirafiki kwa timu za Taifa, ligi hiyo inarejea tena kuanzia leo Jumanne, tarehe 15 Juni 2021. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).

Mchezo utakaopigwa leo Jumanne ni kati ya Biashara United dhidi ya Namungo FC, kuanzia saa 10:00 jioni, katika Uwanja wa Karume, mkoani Mara.

Ligi hiyo ilisimama kwa wiki mbili kupisha maandalizi ya kambi ya timu ya soka la Tanzania ‘Taifa Stars’ iliyocheza mchezo wa kirafiki na Malawi, juzi Jumapili, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na kuibuka na ushindi wa 2-0.

Hadi ligi hiyo inasimama, mabingwa watetezi Simba ya Dar es Salaam, ilikuwa ikiongoza kwa pointi 67 baada ya kushuka dimbani mara 27 huku watani zao, Yanga wakishika nafasi ya pili ikiwa na pointi 61, baada ya kucheza michezo 29.

Mwadui FC inayoshika mkia kwenye msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 19, baada ya kushuka dimbani mara 30, tayari imekwisha kata tiketi ya kushuka daraja.

Ushindani mwingine kwenye ligi hiyo inayoshirikisha timu 16, ni wanaowania ufungaji bora ambapo mshambuliaji wa Azam FC, Prince Dube, anaongoza kwenye mbio hizo, baada ya kuzifumania nyavu mara 14.

Anayefuati kwenye mbio hizo ni Nahodha wa Simba, John Bocco akiwa na magoli 13 na mshambuliaji mwenzake kwenye timu hiyo, Meddie Kagere akiwa na magoli 11.

error: Content is protected !!