Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kina Mbowe waandika barua hospitali aliyotibiwa shahidi, wajibiwa
Habari za SiasaTangulizi

Kina Mbowe waandika barua hospitali aliyotibiwa shahidi, wajibiwa

Spread the love

 

PETER Kibatala, Kiongozi wa Jopo la Mawakili wa Utetezi, katika kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu, ameiandikia barua Hospitali ya TMJ jijini Dar ea Salaam, kuomba taarifa za matibabu ya shahidi wa Jamhuri, Tumaini Swila. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Kibatala ametoa madai hayo leo Jumatatu, tarehe 14 Februari 2022, katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, jijini Dar es Salaam, wakati akimuuliza maswali ya dodoso askari polisi Swila, mbele ya Jaji Joachim Tiganga.

Kibatala alimhoji Swila ambaye ni shahidi wa 13 wa Jamhuri, kama anafahamu uongozi wa hospitali hiyo umeijibu barua yake na kwamba wahusika wako tayari kuja mahakamani kutoa ushahidi kuhusu matibabu yake, ambapo alijibu akidai hafahamu.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo inayodaiwa kufunguliwa na Swila, tarehe 18 Julai 2020, ni waliokuwa makomando wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya.

Kiongozi huyo wa mawakili wa utetezi, alimuuliza maswali hayo Swila, baada ya Alhamisi iliyopita, mawakili wa Jamhuri kuwasilisha cheti kinachodaiwa kuwa cha Hospitali ya TMJ, ambacho taarifa zake zilieleza shahidi huyo wa Jamhuri amepewa mapunziko ya siku tatu.

Cheti hicho kililetwa mahakamani hapo na Jamhuri, ili kuthibitisha kuwa Inspekta Swila anaumwa na amepatiwa matibabu, baada ya Jumatano ya tarehe 9 Februari 2022 kuishia njiani kutoa ushahidi wake akidai anaumwa na anatakiwa kwenda hospitali kupatiwa matibabu.

Yafuatayo nimahojiano kati ya Wakili Kibatala na Inspekta Swila;

Kibatala: Una daktari wako mahsusi au unakwenda hospitali na kuhudumiwa na yeyote unayemkuta siku hiyo?

Shahidi: Huwa nakwenda na kuhudumiwa na madaktari wawili tofauti.

Kibatala: Na ulianza kuhudumiwa mwaka gani au lini kwenye hiyo Hospitali ya TMJ?

Shahidi: Zaidi ya miaka miwili.

Kibatala: Unafamu majina ya hao madakatari wote wawili?

Shahidi: Mmoja anaitwa Mohamed, jina lake la pili silikumbuki.

Kibatala: Alikuhudumia kwa muda gani ambaye jina lake la pili hulikumbuki?

Shahidi: Ndani ya miaka miwili.

Kibatala: Ulitaarifiwa na uongozi wa Hospitali kuwa niliandika barua kuulizia huduma kadha wa kadha ambayo uliiharifu mahakama ulipatiwa na waliijibu?

Shahidi: Rudia swali lako.

Kibatala: Uliambiwa niliandika barua kwa mkono wangu kwenda hospitali na wakanijibu?

Shahidi: Sijajulishwa.

Kibatala: Hufahamu kwamba wamenijibu madaktari na wahusika wako tayari kuja kutoa ushahidi mahakamani wakati husika?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Ni ushahidi wako ukiacha Dk. Mohamed huyo daktari mwingine jina lake hata moja hufahamu?

Shahidi: Sahihi.

Kibatala: Ni hali ya kawaida kutofahamu jina la daktari anayekuhudumia kwa miaka miwili?

Shahidi: Huwa nafahamu kwa chumba.

Kibatala: Ni hali ya kawaida?

Shahidi: Hali ya kawaida.

Kibatala: Ulilazwa au ulienda kupumzika nyumbani?

Shahidi: Nilipumzishwa kwa muda, baadae nikaenda nyumbani, siku hiyohiyo

Kibatala: Kwa hiyo tarehe 10 na 11 ulikuwa uko nyumbani?

Shahidi: Sahihi.

Kibatala: Uko nyumbani ulikuwa unahudumiwa na madaktari wanaokuja nyumbani?

Shahidi: Hapana.

Shahidi huyo anaendelea kutoa ushahidi wake, katika kesi hiyo mbele ya Jaji Tiganga.

Mbowe na wenzake wanakabiliwa na mashtaka sita ya ugaidi, likiwemo la kuoanga njama za kudhuru viongozi wa Serikali, kulipua vituo vya mafuta na maeneo yenye mikusanyiko ya watu na kuandaa maandamano yasiyo ya kikomo.

Mashtaka mengine ni, kukutwa na sare za JTWZ na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), kinyume cha sheria, linalomkabili Bwire peke yake. Shtaka la kukutwa na silaha kinyume cha sheria, linalomkabili Kasekwa peke yake.

Na shtaka la kutoa Sh. 699,000,kwa ajili ya kufadhili vitendo hivyo, linalomkabili Mbowe peke yake.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Julai na Agosti 2020, kwa lengo la kuzua taharuki kwa jamii na kuifanya nchi isitawalike.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI TV, MwanaHALISI Online na mitandao yetu ya kijamii kwa habari na taarifa mbalimbali

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!