RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametangaza siku saba za maombolezo ya kitaifa kufuatia kifo cha Rais wa kwanza wa Zambia, Kenneth Kaunda. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Kaunda (97), alifikwa na mauti jana Alhamisi, tarehe 17 Juni, 2021 mjini Lusaka Zambia.
Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa na Jaffar Haniu, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu imesema, katika kipindi hicho cha maombolezo, bendera zote zitapepea nusu mlingoti.
Aidha, Rais Samia ametuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Zambia, Edgar Chagwa Lungu, familia ya marehemu na wananchi wote wa Zambia kwa kumpoteza kiongozi wao.
Rais Samia amemtaja Hayati Kaunda kuwa miongoni mwa viongozi mahiri na jasiri kuwahi kutokea barani Afrika.
Wakati wa uhai wake, alitoa mchango mkubwa kwenye harakati za ukombozi wa Bara la Afrika kwa kushirikiana na viongozi wengine, akiwemo Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Vilevile, Hayati Kaunda alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Tanzania itamkumbuka Hayati Kaunda kwa mchango wake katika kukuza uhusiano na ushirikiano kati ya mataifa yetu mawili, ambao uliwezesha kutekelezwa kwa miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo Mamlaka ya Reli kati ya Tanzania na Zambia (Tazara) na Bomba la Kusafirisha Mafuta (Tazama).
Hayati Kaunda, alikuwa Rais wa Zambia kwa miaka 27 kuanzia tarehe 24 Oktoba 1964 hadi 2 Novemba 1991.
Alizaliwa tarehe 28 Aprili 1924.
Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahali pema Peponi.
Leave a comment