Saturday , 15 June 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kesi ya Zitto: Polisi akiri mauaji Uvinza
Habari za SiasaTangulizi

Kesi ya Zitto: Polisi akiri mauaji Uvinza

Spread the love

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imeendelea kusikiliza kesi Na 327 ya 2018 ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe. Anaripoti Faki Sosi …(endelea).

Leo tarehe 25 Aprili mwaka 2019 mahakama hiyo ilishuhudia shahidi wa kwanza wa upande wa mashitaka, SSP John Malulu akikabiliana na maswali mbalimbali ya mawakili wa utetezi wakiongozwa na Peter Kibatala ambaye mara kadhaa alilazimika kumuomba hakimu amtake shahidi kujibu badala ya kutaka kuyakwepa.

SSP Malulu alianza kutoa ushahidi wake juzi tarehe 23 Aprili akiongozwa na wanasheria wa serikali, Nassoro Katuga na Tumaini Kweka.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shahidi anayesikiliza kesi hiyo iliyofikishwa mahakamani mara ya kwanza tarehe 2 Novemba mwaka jana. Zitto anatuhumiwa kwa makosa ya uchochezi yakihusiana na maelezo aliyoyatoa kwa waandishi wa habari aliokutana nao kwenye makao makuu ya ACT-Wazalendo, Kijitonyama, Dar es Salaam.

Wakili Kibatala alianza mahojiano kwa kumuonesha shahidi nakala ya maelezo yake aliyoyatoa Polisi akimuomba ayatambue kama ndio yenyewe. Ilionesha kuwa lengo la wakili Kibatala lilikuwa kutaka nakala hiyo aitoe mahakamani ili iwe kielelezo kimojawapo kwa upande wa utetezi.

Wakili Kibatala alisaidiana na Jeremiah Mtobesya na Steven Mwakibolwa ambao walitumia muda mfupi kuuliza maswali yaliyombana zaidi shahidi SSP Malulu, baada ya kuonekana akizongana na wakili Kibatala kiasi cha wanasheria wa upande wa mashitaka kuingilia na kuomba hakimu atoe muongozo.

Aidha, mara mbilitatu Hakimu Shahidi alilazimika kuingilia kati kuwatuliza wanasheria waliokuwa wanatupiana maneno mabaya.

Mtindo huo ulimlazimu hakimu Shahidi kumuomba Hashim Rungwe, wakili mkongwe kutoa nasaha kwa mawakili hao vijana.

Pamoja na “rusharusha” za Shahidi SSP Malulu wakati akiulizwa maswali na Wakili Kibatala, hatimaye alikiri kuwa alitoa maelezo Polisi na akaridhia nakala ya maelezo yake itolewe kwa Mahakama kama sehemu ya vielelezo.

Pamoja na mahojiano kwenye maeneo mengine yaliyotokana na maelezo aliyoyatoa wakati akiongozwa na wanasheria wa upande wa mashitaka, mwenendo ulianza hivi:

Kibatala: Shahidi naomba ufafanuzi wako; ni wewe uliyeapa kiapo kilicholenga kuzuia dhamana ya mshtakiwa mahakamani tarehe 2 Novemba mwaka 2018?

Shahidi: Sikumbuki vizuri.

Kibatala: Hukumbuki… kwamba unahitaji muda?

Shahidi: Sikumbuki.

Kibatala: Majina yanayoonekana kwenye kiapo hiki ni yako?

Shahidi: Ni yangu.

Kibatala: Na hii saini.

Shahidi: Zinafanana na za kwangu?

Kibatala: Unakumbuka kuwahi na kuandaa kiapo cha kuzuia dhamana ya Zitto Kabwe?

Shahidi: Sikumbuki.

Kibatala: Unakumbuka kuwa na nia ukiwa kama Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (RCO) ya kuzuia dhamana ya mshtakiwa?

Shahidi: Ndio.

Kibatala: Ni sahihi kuwa wewe ndio umelalamika juu kesi hii?

Shahidi: Sahihi.

Kibatala: Ni sahihi kuwa wewe ndio uliyemkamata Zitto Kabwe?

Shahidi: Ndio.

Kibatala: Wewe ndio uliyekula kiapo?

Shahidi: Ndio.

Kibatala: Unafahamu dhana ya kuwa na interest (maslahi) kwenye kesi?

Shahidi: Sijui.

Kibatala: Ni sahihi kuwa Jeshi la Polisi limejaali watu wa darasa la saba na kufikia ngazi ya Ukuu wa Upelelezi Mkoa (RCO)?

Shahidi: Wengi tu, kinachoangaliwa ni utendaji wake tu.

Kibatala: Ni sahihi kwetu raia kupima utendaji wa RCO dhidi ya elimu yako ya darasa la saba?

Shahidi: Sio sahihi.

Kibatala: Jana umeongozwa kwenye ushahidi; unakumbuka uliongozwa kumuonesha (kwa maana ya kumtambua mshitakiwa) Zitto Kabwe na ukamshika bega na ukamuonesha?

Shahidi: Niliongozwa ndio.

Kibatala: Ulimtambua kwa kumshika bega?

Shahidi: Ndio.

Kibatala: Uliongozwa kumshika bega, mguu, kiatu au kwa namna yoyote ile?

Shahidi: Haikuwa lazima.

Baada ya mvutano kidogo kati yao, Hakimu Shahidi aliingilia akisema “Point noted (imezingatiwa).”

Wakili Kibatala: Ulizungumzia watu waliokusanyika Manzese, Mahakama itapata vipi nafasi ya kupata maoni ya watu wengine ukiachilia huyo mmoja uliyezungumza naye?

Shahidi: Ikipata kwa mmoja watawawakilisha wengine.

Kibatala: Mahakama itapata nafasi ya kusikiliza watu wengine hao 14 kati ya watu 15 uliowataja umewaona Kimara?

Shahidi: Nimemleta mmoja, Mahakama isiporidhika itafanya uamuzi.

Kibatala: Kwa ushahidi wako je Mahakama inawafahamu hao wengine 14?

Shahidi: Mimi nimeleta wawili.

Kibatala: Shahidi tukumbushe ulipata nafasi ya kuingia kwenye Press Conference ya Zitto (Mkutano wa vyombo vya habari) binafsi?

Shahidi: Hapana.

Kibatala: Kwa hiyo maneno hayo uliyodai yametamkwa kwenye Press Release ya Zitto wewe binafsi umeyasikia au hujayasikia?

Shahidi: Nilituma watu wangu.

Kibatala: Wewe binafsi umeyasikia?

Shahidi: Mimi nimeona kwenye Youtube (moja ya aina za mitandao ya kijamii).

Kibatala: Shahidi kwenye maelezo yako umetaja Youtube tu au umetaja vyombo vengine vya mitandao ya kijamii?

Shahidi: Youtube.

Kibatala: Mheshimiwa Hakimu naomba maelezo ya shahidi ajikumbushe. (Shahidi amepitia maelezo)

Shahidi: Nimekuwa nikiona mitandao ya kijamii Youtube, Instargram, Facebook, zipo nyingi.

Kibatala: Mwambie Hakimu kuhusu mitandao mingine ambayo hujaitaja wakati unatoa ushahidi?

Shahidi: Youtube, Facebook na Instargram.

Kibatala: Mwambie hakimu kuwa hujatoa ushahidi hiyo mitandao mengine.

Shahidi: Sijasema chochote.

Kibatala: Shahidi jana nilikuuliza kuhusu hati ya mashtaka haya maneno yanayoonekana kwenye shitaka la kwanza na la pili. Mwambie hakimu hayo maneno yaliyokuwepo kwenye hati ya mashtaka kama yapo kwenye maelezo yako. Naweza nikakupa kujikumbushia?

Shahidi: Haina haja tutapoteza muda tu.

(Shahidi anapitia).

Shahidi: Maelezo yangu ina sehemu ya maneno yaliyobeba kwenye hati ya mashtaka kwa kifupi tu sio neno kwa neno.

Kibatala: Bila shaka sasa maneno yaliyoandikwa kwenye hati ya mashitaka sio yale yaliyopo kwenye maelezo yako.

Shahidi: Mimi sio shahidi wa mwisho.

Kibatala: Ni sahihi maneno yaliyoandikwa kwenye hati ya mashitaka sio yale yaliyokuwepo kwenye maelezo yako. Na Mwendesha mashitaka ameyatoa sehemu nyengine?

Shahidi: Mimi sio shahidi wa mwisho.

Kibatala: Nakuuliza shahidi hayo maneno yametolewa kwenye chanzo kingine sio maelezo yako.

Shahidi: Kimya (Majadiliano).

Kibatala: Zitto Kabwe aliongea maneno haya tu yaliyokuwepo kwenye hati mashitaka au kuna mengine?

Shahidi: Haya ndio yenye jinai. Jeshi la Polisi linahusika na jinai tu.

Kibatala: Swali langu hujajibu, hiyo Press Conference Zitto aliongea maneno mengine au alifika na kuongea maneno yaliyomo kwenye shitaka la kwanza na la pili akaondoka?

Shahidi: Kimya.

Kibatala: Ishike hiyo nyaraka iangalie.

Shahidi: Hapana siwezi kushika nyaraka ambayo sijaileta mahakamani.

Hakimu Shahidi: Ishike baadaye utaulizwa.
(shahidi amepokea karatasi aliyopewa na Wakili Kibatala)

Kibatala: Hiyo ndio karatasi ya maneno aliyoyasema Zitto?

Shahidi: Haina saini hii inaweza kuwa imeokotezwa mtaani tu?

Kibatala: Kwa hiyo sio hii kwa sababu haina saini au siyo yaliyotamkwa?

Shahidi: Haikusainiwa.

Kibatala: Taratibu zote za upekuzi zilifuatwa ikiwemo hati ya upekuzi?

Shahidi: Zote zilifuatwa.

Kibatala: Hati ya upekuzi ilisainiwa?

Shahidi: Atajibu shahidi atakayefuata.
huyo akija tutaongea naye nakuuliza wewe ndiye uliyekuwa mkuu wa upelelezi na ndiye ulimkamata Zitto. Wewe ulisaini hati ya upekuzi?

Shahidi: Sikusaini.

Kibatala: Kwasababu wewe ndio ulimkamata Zitto, ulimfikisha kituoni au ulikwenda kumpekua kwanza?

Shahidi: Alifikishwa kituoni kisha akapekuliwa.

Kibatala: Mwambie hakimu lini mulimkamata mshtakiwa na lini alipekuliwa?

Shahidi: Tulimkamata tarehe 31 Oktoba mwaka 2018 na kupekuliwa siku hiyo.

Kibatala: Unayakumbuka majina ya askari waliokwenda kumpekua?

Shahidi: Yupo Inspekta Salumu.

Kibatala: Mwengine?

Shahidi: Nakumbuka huyo.

Kibatala: Uliwahi kuwasiliana na Mkuu wa Kituo (OCS) cha Osterbay aisaini hati ya upekuzi?

Shahidi: Ni wajibu wake.

Kibatala: Zitto mlipomkamta alikaa rumande siku ngapi kabla ya kumpeleka mahakamani?

Shahidi: Siku nyingi.

Kibatala: Alikaa muda unaoruhusiwa kisheria au zaidi ya masaa 48?

Wakili Katuga: Hayo maswali ya kisheria. Wewe ndiye uliyemkamata; alikaa rumande muda unaoruhusiwa kisheria au zaidi ya masaa 48?

Shahidi: Sikumbuki.

Kibatala: Alikwenda kufanyiwa upekuzi wapi?

Shahidi: Niliwapa askari majukumu wameenda kuyatekeleza.

Kibatala: Kwa hiyo hufahamu?

Shahidi: Sikumbuki.

Kibatala: Uliwahi kwenda Nguruka?

Shahidi: Mimi sio RCO wa Kigoma.

(Kimya kidogo)

Hakimu Shahidi: Mimi nimeandika hakwenda.

Shahidi: Mimi sio RCO wa Kigoma.

Kibatala: Hebu tumzungumzie Martin Gelard (RCO wa Kigoma)… ni sahihi aliwahi kwenye kituo cha polisi cha Osterbay kwenye nafasi kama yako kabla hajaja Kigoma?

Sahihi: Ndio.

Kibatala: Ni sahihi kuwa yeye na maofisa wengine wamehamishwa Kigoma?

Shahidi: Sijui.

Kibatala: Ni sahihi kuna maofisa wengine mara baada ya tukio hili walihamishwa Kigoma?

Shahidi: Sijui.

Kibatala: Tufikirie ushahidi uliotoa ni wa kweli na tufikirie Zitto alifanya kweli; je Jeshi la Polisi lilishawahi kutoa maelezo juu ya taarifa aliyoitoa Zitto?

Shahidi: Sio msemaji wa Polisi.

Kibatala: Ni sahihi katika (Press Conference) Zitto alisema jeshi litoke litoe taarifa juu ya tukio la Uvinza?

Shahidi: Hayo sijayasikia.

Kibatala: Kwa ushahidi wako ulipitia Youtube, Zitto alisema nalitaka Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi?

Shahidi: Sikusikia.

Kibatala: Ni sahihi Zitto ni Mbunge wa Jamhuri ya Tanzania?

Shahidi: Ni kweli.

Kibatala: Ni kweli pia Zitto ni mbunge wa eneo la Nguruka na Uvinza?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Kwa ufahamu wako haya maneno Zitto aliwahi kuyazungumzia Bungeni?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Unafahamu kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani aliwahi kulizungumzia hili tukio bungeni?

Shahidi: Sikumbuki.

Kibatala: Kwa ufahamu wako ni kweli hili tukio lilitokea Uvinza, tuanze na askari wawili kuuawa?

Shahidi: Ndio lilitokea.

Kibatala: Ni kweli lilitokea kwenye tarehe hizo hizo Zitto Kabwe anazizungumzia?

Shahidi: Sikumbuki.

Kibatala: Ni kweli kwenye tukio la Nguruka na Uvinza kuna wananchi walijeruhiwa?

Shahidi: Kweli.

Kibatala: Unafahamu idadi ya wananchi waliojeruhiwa?

Shahidi: Ndio.

Kibatala: Mwambie hakimu, ni wananchi wangapi na walijeruhiwa na nani?

Shahidi: Taarifa nilizonazo wanne.

Kibatala: Katika taarifa ya Zitto Kabwe inasema ni wananchi wangapi walijeruhiwa?

Shahidi: Wanne.

Kibatala: Walijeruhiwa na nani?

Shahidi: Sikuwa Kigoma.

Kibatala: Martin Gelard (RCO Kigoma) aliwahi kukuambia hao watu walijeruhiwa na nani?

Shahidi: Hapana.

Kibatala: Ni kweli kwamba watu hao wanne walijeruhiwa kwenye uvamizi wa ranchis ya Uvinza?

Shahidi: Ndio.

Kibatala: Ni kweli ranchi ya Uvinza inamilikiwa na Serikali?

Shahidi: Sijui.

Kibatala: Unaufahamu kuwa Kamishna wa Jeshi la Polisi Simon Sirro alikwenda Nguruka na Uvinza baada ya tukio hilo?

Shahidi: Sikumbuki.

Kibatala: Hao watu wanne walifikishwa mahakamani?

Shahidi: Siwezi kukumbuka.

Kibatala: Kuna mtu yeyote aliyefikishwa mahakamani kwa kuuawa kwa hawa askari wawili?

Shahidi: Sijapata taarifa.

Kibatala: Kwa miezi sita hatujapata taarifa?

Shahidi: Mimi sio RCO wa Kigoma.

Kibatala: Kuna watu wowote waliofikishwa mahakamani kuhusiana na uvamizi wa ranchi?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Kuna mtu yeyote aliyewahi kufikishwa mahakamani kwa kujeruhi watu wanne?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Kuna askari yeyote aliyemhoji Zitto juu ya chanzo chake cha habari juu tukio la Uvinza?

Shahidi: Hakuna.

Kibatala: Wewe ulivyomkamata Zitto ulimuuliza chanzo chake juu ya tukio la Nguruka na Uvinza?

Shahidi: Sijamuuliza.

Kibatala: Uliwahi kumuuliza Zitto kwanini alitamka maneno hayo?

Shahidi: Ndio.

Kibatala: Alikujibu nini?

Shahidi: Alikataa kujibu, alikuwa bubu.

Kibatala: Alitoa maelezo yoyote?

Shahidi: Ndio.

Kibatala: Bila shaka ipo karatasi ya maelezo aliyoyatoa Zitto?

Shahidi: Ndio.

Kibatala: Siku moja kabla ya tukio uliingia Youtube na uliwapa kazi askari waingie kwenye Youtube wafanye uchunguzi. Ni sahihi hawa watu makosa ya mtandaoni (Cyber Crime) wewe ndio uliowasimulia?

Shahidi: Niliwaelekeza.

Kibatala: Hao watu wa makosa mitandao unafahamu walifanya nini huko Youtube kama unajua?

Shahidi: Waliifuatilia video iloandaliwa kuletwa Mahakamani.

Kibatala: Hiyo video wewe umeiona?

Shahidi: Ndio

Kibatala: Uliiona lini hiyo video?

Shahidi: Sikumbuki.

Kibatala: Video ilikuwa chini ya nani; wewe au mtaalam aliyefuatilia.
Mtaalam?

Shahidi: Huyu mtaalam ndiye aliyekuwa akiichunguza.

Kibatala: Unakumbuka karatasi ulizosaini kuhusiana na hiyo video?

Shahidi: Nilisaini karatasi video ilipotoka Osterbay Polisi kwenda Makao Makuu ya Jeshi.

Kibatala: Ripoti ya uchunguzi uliifahamu binafsi?

Shahidi: Ipo nilioneshwa.

Kibatala: Mueleze Hakimu ni nani aliyekuonesha hiyo ripoti?

Shahidi: SSP Sharmila.

Kibatala: Ndio huyu unayemzungumzia uliyemtaja kwenye maelezo yako?

Shahidi: Ndio huyo.

Kibatala: Alikuwa na kazi gani kwenye uchunguzi?

Shahidi: Ni Ofisa wa makosa ya mtandao (Cyber Crime officer).

Kibatala: Uchunguzi wa makosa ya mtandao ulifanyika wapi?

Shahidi: Makao makuu.

Kibatala: Kwa ufahamu wako Zitto akiwa chini ya ulinzi kwa siku ambazo umesema huzikumbuki kuna ofisa yeyote uliyempa kazi ya kurekodi sauti yake?

Shahidi: Hakuna.

Kibatala: Hiyo video ipo mikononi mwa nani?

Shahidi: Ipo mikononi mwa Ofisa wa Makosa ya mtandaoni.

Kibatala: Uliwahi kwa kumbukumbu zako kusaini risiti yoyote inayohusiana na hii video?

Shahidi: Sikumbuki.

Kibatala: Bila shaka kuhamishwa kwa hii video ipo kwenye kumbukumbu yoyote?

Shahidi: Ipo kwenye barua.

Wakili Katuga. Anachojibu wakili sicho kile kinachosemwa na shahidi.

Kibatala alimmgeukia wakili Katuga, “Acha kiherehere, mimi naongea na shahidi.” Naye akajibu, “Mimi pia ninajua matusi acha ufala.”

Hakimu Shahidi alitaka wote waheshimu mahakama. Utulivu ukarejea.

Kibatala: Unakumbuka ofisa Sharmila alikula kiapo mbele yako wewe juu ya kula kiapo kuhusiana na hii video yenye ushahidi?

Shahidi: Sikumbuki ilikuwa siku gani.

Kibatala: Hapo awali shahidi umesema kwamba mojawapo ya vitu ambavyo uliulizia ni nyaraka. Hivi ulipomkamata Zitto ulimkuta na Press Release?

Shahidi: Sikumkuta na chochote.

Kibatala: Wakati unamkamata alikuwa akifanya Press Conference au alikuwa akifanya shughuli nyengine?

Shahidi: Nyumbani kwake.

Kibatala: Wakati unamkamata ulitokea Osterbay au mahala pengine?

Shahidi: Mahala pengine.

Kibatala: Moja ya vitu vilivyochukuliwa ni Press Release; mwambie Hakimu iwapo uliongozwa na wakili yeyote wa serikali iwapo ulizungumzia utaalam wa uchunguzi wa saini ya Zitto?

Shahidi: Hapana.

Kibatala: Kwa ufahamu wako nani alichunguza saini ya Zitto.

Shahidi: ASP Kitunu.

Wakili Kweka: Alikuwa akizungumzia Press Release sio Press Conference. Kibatala aliridhia baada ya majadiliano mafupi kutofautisha hayo mawili.

Kibatala: Nini kilifanyika kwamba ile kompyuta iliandika nyaraka ile ilitoka ACT au nyumbani kwa Zitto?

Shahidi: Kitunu anafahamu.

Kibatala: Matokeo ya uchunguzi unayafahamu?

Shahidi: Kitunu anayafahamu.

Kibatala: Vitu mulivyovikusanya kwenye vielelezo hamkuvihusisha printer wala kompyuta?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Kwenye taarifa ya Zitto alilitaja Jeshi la Polisi au Serikali?

Shahidi: Jeshi la Polisi.

Kibatala: Alitaja Polisi mmoja mmoja au taasisi?

Shahidi: Taasisi.
Wakili Kibatala akamaliza maswali yake na kumpisha wakili mwenziye wa utetezi Mtobyesa.

Mtobesya: Shahidi isaidie mahakama tangu jana ulisema kuwa kuna taarifa alizitoa Shabani Hamisi na Mashaka Juma; aliyelalamika ni nani?

Shahidi: Mimi.

Mtobesya: Huyu Shabani Hamisi na Mashaka Juma walikuambia taarifa walizitoa wapi?

Shahidi: Baadhi yao walikuwa wana simu. Kwenye simu zilizokuwa kwenye kundi hilo.

Mtobesya: Kwa hiyo nitakuwa sahihi kuwa taarifa hizo walizitoa mtandaoni?

Shahidi: Ndio.

Mtobesya: Aliyeziposti hizo taarifa mtandaoni unamfahamu?

Shahidi: Sifahamu.

Mtobesya: Wewe ndiye uliyejua kuwa amefanya kosa, hayo maneno ni ya uongo au ni ya kweli yamepelekea hizo hisia?

Shahidi: Ya uongo na yamepelekea hizo hisia.

Mtobesya: Wakati unaongozwa ulitoa majibu yako ya kweli.

Mtobesya: Unarekodi yoyote ya mawasiliano yako wewe na RCO wa Kigoma uliyoyatoa mahakamani?

Shahidi: Nina namba yake, nimewasiliana naye.

Mtobesya: Kwa ufahamu wako hiyo ndio rekodi?

Shahidi: Sina rekodi.

Mtobesya: Moja kati ya sababu ya kosa kuwa kosa kuchukuliwa sio kosa ni huyo anayesemekana ametenda kosa kutoamini kuwa hajafanya kosa?

Hakimu Shahidi: Hapana hiyo inatoa hitimisho.

Mtobesya: Mulimuhoji Zitto akasema kuwa hilo ni kosa au sio kosa?

Shahidi: Aligoma kutoa ushirikiano.

Mtobesya: Nitakuwa sahihi kwamba ukiingia kazi lazima usaini?
Unafahamu kitabu kinachoitwa OB?

Shahidi: Kuna ngazi lakini mimi sisaini.

Mtobesya: Hamna sehemu yoyote inayoonesha kuwa wewe upo kazini?

Shahidi: Mimi nikiingia kazini bosi wangu anajua, nikitaka kutoka namuaga bosi wangu.

Mtobyesa: Ni wapi uligundua kuwa Zitto amefanya kosa?

Shahidi: Maneno yaliyotamkwa na Zitto yamechonganisha Jeshi la Polisi na wananchi; nilipoona yale mapokeo ya wananchi wa Manzese na Kimara.

Wakili Mtobyesa alipomaliza kumhoji shahidi, alifuata wakili Mwakibolwa.

Mwakibolwa: Tarehe 28 uliwasaini makachero wako, ukiwa maeneo ya Tip Top kutokea Osterbay Polisi, uliona kundi kubwa la watu ulikuwa kwenye umbali gani?

Shahidi: Kwa ukaribu.

Mwakibolwa: Ulitumia usafiri gani, tutajie na namba ya gari lenyewe?

Shahidi: Namba T232 DDC Toyota Land Cruiser.

Mwakibolwa: Uliwakuta watu wakiwa kwenye hali gani?

Shahidi: Mihemko.

Mwakibolwa: Ni kwa wakati gani unaweza kuzuia mihemko?

Shahidi: Inategemea ukubwa wa kundi. Nilipeleka kikosi cha uchunguzi.

Mwakibolwa: Kutoka Manzese hadi Kimara kuna umbali gani?

Shahidi: Kilometa 5 hadi sita.

Mwakibolwa: Uliwakuta watu 15 hadi 20. Ulivyotoka kwenye hilo kundi ulielekea wapi?

Shahidi: Kituo cha Polisi Gogoni.

Mwakibolwa: Ulikwenda kwa shughuli gani?

Shahidi: Mambo yangu.

Mwakibolwa: Kwa hiyo yale uliyoyaona kule sio kitu kikubwa ndio maana ukaenda Kimara na ishu zako?

Shahidi: Hapana, nilienda kuhakikisha ulinzi.

Mwakibolwa: Jambo gani la kwanza kulifanya ulipofika Osterbay?

Shahidi: Niliita makechero na kupanga Section (Doria) mbili.

Baada ya Mwakibolwa, Wakili wa Serikali, Katuga alianza kumhoji shahidi wake kwatika utaratibu unaoelekea kusawazisha walipoona pana upungufu kutokana na majibu ya shahidi akiulizwa na mawakili wa utetezi.

Wakili Katuga. Umeulizwa kuhusiana na sampuli ya sauti ya mtuhumiwa uliona nini ulivyofungua Youtube?

Shahidi: Nilipofungua Youtube niliona sura ya Zitto Kabwe akihutubia watu.

Katuga: Ni kitu gani?

Shahidi: Clip (Video fupi).

Wakili Katuga: Umeulizwa maswali mengi. Iambie mahakama ni nani anayetaka utoe ushahidi?

Shahidi: Mwendesha Mashtaka ndiye anayetaka nitoe ushahidi wa aina gani.

Wakili Katuga: Ifafanunulie mahakama kuhusu majibu yako kwenye maelezo yako na utafauti kwenye hati ya mashtaka?

Shahidi: Ipo kwa kifupi kwenye maelezo yangu.

Wakili Katuga: Kuhusiana na hawa watu waliokuwepo pale hasahasa nini ulikitaka kujua kutoka kwao?

Shahidi: Nilipowaona mihemko ile nilitaka kujua kuhusiana mihemko ile.

Katuga: Umeulizwa kama kuna mashahidi wengine kwenye kila kundi ifafanulie mahakama shahidi wangapi wanahitajika kwenye kesi.

Wakili Kibatala aliingilia kati kupinga mfumo wa swali. “Katuga alijielekeza tusiyaguse maswali ya kisheria.”

Wakili Katuga aliendelea, “kwanini kwenye kila kundi uliamua kumchukua mmoja.

Shahidi: Nilizingatia mtu mmoja anaweza kutoa ushahidi.

Wakili Katuga: Iambie mahakama kuhusu majina yako.

Shahidi: SSP Kungu John Malulu na Kungu John na Kungu John Malulu, yote majina yangu.

Wakili Kweka alimpokea Wakili Katuga kumuuliza shahidi. 

Aliomba maelezo ya shahidi. Alipewa.

Kweka: Haya maelezo umeyaandika lini hasa?

Shahidi: Tarehe 31 Oktoba 2018.

Kweka: Press Conference ilifanyika lini? Kibatala aliniambia nitumie neno Press Release na sio Press Conference. Ilifanyika lini.

Shahidi: Tarehe 28 Oktoba 2018.

Kweka: Zitto ulimkamata lini?

Shahidi: Terehe 31 Oktoba 2018.

Kweka: Ulisema umemkamata nyumbani, ni sahihi?

Shahidi: Sahihi.

Kweka: Uliwahi kufanya mahojiano na Zitto kuhusiana na tukio?

Shahidi: Nilimuhoji hakutoa ushirikiano.

Hakimu Shahidi alioahirisha shauri hilo mpaka terehe 16 na 17 Mei mwaka huu saa 3 asubuhi. Mtuhumiwa Zitto anaendelea na dhamana.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

DA, ANC waridhia kuunda serikali ya mseto Afrika Kusini

Spread the loveChama tawala nchini Afrika Kusini cha African National Congress, ANC,...

BiasharaHabari MchanganyikoHabari za Siasa

Mataifa Afrika Mashariki yawasilisha bajeti 2024/2025 inayolenga kukuza uchumi

Spread the loveMataifa manne ya Afrika Mashariki jana Alhamisi yamewasilisha bungeni bajeti...

Habari za SiasaTangulizi

Gesi asilia, petroli kodi juu

Spread the loveWaziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba amependekeza kufanya marekebisho kwenye...

Habari za SiasaTangulizi

Bilioni 155.4 kugharamia kicheko cha wastaafu 2022-2030

Spread the loveWaziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba amesema jumla ya Sh...

error: Content is protected !!