May 21, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kesi ya North Mara: Kiswahili champandisha cheo Jaji

Rais John Magufuli

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, John Magufuli amempandisha cheo Jaji Zepharine Galeba, Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa. Ni baada ya kutumia kiswahili kutoa hukumu ya kesi ya North Mara Gold Mine dhidi ya Gerald Nzumbi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Jaji Galeba alitumia Lugha ya Kiswahili katika kesi hiyo ya mapitio Namba 23 ya mwaka 2020, iliyokuwa inaendeshwa katika Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma.

Rais Magufuli amempandisha cheo jaji huyo leo Jumatatu tarehe 1 Februari 2021, jijini Dodoma katika Maadhimisho ya Miaka 100 ya Mahakama nchini, wakati akihimiza matumizi ya Kiswahili katika shughuli za mahakama.

“Huyu Jaji Galeba wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma ninampongeza. Ni shujaa wa Kiswahili katika mahakama na kwasababu ameamua, mimi leo nampandisha cheo kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa kwa uzalendo huo wa Kitanzania wa kukwepa miiko iliyopo ndani ya mahakama,” amesema Rais Magufuli.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Rais Magufuli amesema, hatua hiyo ni pongezi kwa Jaji Galeba kwa kuwa jaji wa kwanza kuandika hukumu kwa kutumia Kiswahili.

“Nampongeza sana Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma kwa kutumia Kiswahili kutoa hukumu kwenye kesi ya North Mara Gold Mine dhidi ya Gerald Nzumbi, ninajua alisemwa sana, amekuwa mzalendo wa kwanza kwa kuandika kwa Lugha ya Kiswahili,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli aliamua kumpandisha cheo Jaji Galeba baada ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma kumuomba aajiri watumishi wapya wa mahakama.

Rais wa John Magufuli alipomuapisha Zepherine Galeba Kuwa Jaji wa Mahakama ya Kuu, 29 Januari 2019, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Kuhusu matumizi ya Kiswahili, Rais Magufuli ameagiza Bunge, Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuweka mikakati ili kuwezesha matumizi ya lugha hiyo katika utoaji huduma za mahakama na uandishi wa kisheria.

“Nimezungumzia suala la kuimarisha matumizi ya Kiswahili katika kutoa huduma za mahakama na uandishi wa kisheria.

“Najua suala hili lina mjadala lakini ni wazi wakati umefika wa kuanza kuweka mikakati itakayowezesha Lugha ya Kiswhaili kutumia katika mahakama kisheria na katika ngazi zote,” ameagiza Rais Magufuli.

Amesema, matumizi ya Lugha ya Kingereza katika shughuli za mahakama, yanasababisha gharama kubwa kwa Watanzania, hasa katika kutafuta wakalimani wa kuwatafsiria hukumu na mwenendo wa kesi zao.

“Sioni sababu kwa nini mahakama hamtaki kutumia Kiswahili? Kushindwa kutumia lugha hii kwenye masuala ya kimahakama na kisheria sio tu tunawanyima haki wananchi, bali kuwaongezea gharama kupitia wakalimani wa kutafisiri hukumu na mwenendo wa kesi,” amesema Rais Magufuli.

Baada ya kumaliza hotuba hiyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa amesema, Rais Magufuli amemteua Zepharine Nyalugenda Galeba kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.

Kabla ya uteuzi huo, Galeba alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya
Musoma.

Uteuzi wa Galeba unaanza leo Jumatatu tarehe 01 Februari, 2021 na ataapishwa
kesho Jumanne saa 4:00 asubuhi Ikulu Chamwino jijini Dodoma.

error: Content is protected !!