Friday , 3 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kesi ya Mbowe: Mpelelezi abanwa sababu msaidizi wa Sabaya kuachwa huru
Habari za SiasaTangulizi

Kesi ya Mbowe: Mpelelezi abanwa sababu msaidizi wa Sabaya kuachwa huru

Spread the love

 

MKAGUZI wa Jeshi la Polisi Tanzania, Tumaini Swila, amedai Justine Kaaya,  aliyekuwa msaidizi wa Lengai Ole Sabaya, akiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, alifutiwa mashtaka katika kesi ya uhujunu uchumi, inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, baada ya upelelezi kubaini hakuwa na hatia. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Inspekta Swila aliyekuwa mpelelezi wa kesi hiyo, ametoa madai hayo leo Jumatatu, tarehe7 Februari 2022, baada ya Wakili wa utetezi, Nashon Nkungu, kumhoji sababu zilizopelekea Kaaya kuachiwa huru, ilhali inadaiwa alipokea fedha za Mbowe kwa ajili ya kumpa taarifa za Sabaya.

Ni katika kesi hiyo namba 16/2022, inayomkabili Mbowe na wenzake, katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mawasiliano Dar es Salaam, mbele ya Jaji Joachim Tiganga.

Awali, akitoa ushahidi wake katika kesi hiyo, Kaaya aliieleza mahakama hiyo aliwahi kuwa mfanyakazi wa Sabaya akiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai na kwamba kuna kipindi aliacha kufanya kazi kwake.

Anadai, aliwahi kukutana na Mbowe katika Hoteli ya Aishi mkoani Kilimanjaro,   ambapo mwanasiasa huyo alimuomba taarifa muhimu za Sabaya, ili azitumie katika njama zake za kumdhuru.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni waliokuwa makomando wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya.

Mahojiano kati ya Wakili Nkungu na Inspekta Swila yalikuwa kama ifuatavyo;

Nkungu: Ni sawa na jambo lililifanyika kwa watuhumiwa walioko mahakamani ambapo walitumiwa fedha 699,000 kutoka kwa Mbowe, kama walivyotumiwa na hata Kaaya alitumiwa na Mbowe sahihi?

Shahidi: Ni tofauti

Nkungu: Kwamba Kaaya hakutumiwa fedha na Mbowe?

Shahidi: Alitumiwa

Nkungu: Na kwamba Bwire hakutumiwa pesa na Mbowe?

Shahidi: Alitumiwa

Nkungu: Wote hao wawili kwa mazingira tofauti walitumiwa pesa kutoka kwa mtu mmoja?

Shahidi: Walitumiwa wote lakini lengo na uelewa wa hiyo fedha ilikuwa tofati,  kwamba zililenga kwenye nini

Nkungu: Malengo au huo uelewa kwa mfano  pesa ya Kaaya unayaonea wapi?

Shahidi: Kwa shahidi mwenyewe na upelelezi nilioufanya

Nkungu: Malengo ya pesa aliyotumia Bwire we uliyaonea wapi?

Shahidi: Kutoka kwenye maelezo yake pamoja na maelezo ya watuhumiwa wengine.

Nkungu: Kutoka kwenye maelezo yao ambayo wameyakana hayakuwa ya hiari,  huo pekee ndiyo ushahidi wako unaoonesha malengo?

Shahidi: Hawajakataa

Nkungu: Kwenye hiyo statmenet uliyoandika, Kaaya alisema dhumuni la kutumiwa fedha 200,000 ilikuwa kwa ajili ya kumpatia namba za simu, majina na mahala anakopenda kushinda Sabaya, ni sahihi?

Shahidi: Ni sahihi lakini hakujuwa lengo la kumtafuta Sabaya ni nini

Nkungu: Huyu Kaaya tunayemzungum,a hukuona malengo mpaka unamleta mahakani na baade unamuachia? Hukujuwa malengo kama yalikuwa mazuri?

Shahidi: Rudia swali

Nkungu: Tulikuwa tunazungumzia kuhusu fedha nikakwambia kuna watu wawili walitumiwa fedha, ukasema ndivyo, Kaaya wakati anatoa information anasema alipatiwa fedha, nakuuliza ulifahamu malengo yalikuwa tofauti?

Ulikuja kugundua malengo  baada ya kumleta mahakamani?

Shahidi: Baada ya kumleta mahakamani

Nkungu: toka umkamate na kuja kugundua ilikuwa muda gani?

Shahidi: Zaidi ya miezi 10

Nkungu: Ulimkamata muda gani?

Shahidi: Nakumbuka alifikishwa mahakani mwezi wa tisa 2020

Nkungu: Na ukaja kumuandika maelezo tarehe  30 Julai 2021, mwaka moja baadae?

Shahidi: Sahihi

Nkungu: Baada ya kumuandika maelezo mtu uliyemshikilia zaidi ya mwaka, uliona hausiki?

Shahidi: Niliweza kumgundua kabla ya kuandika maelezo yake, ndiyo maana akaondolewa kwenye mashtaka

Nkungu: Ni sahihi kwamba pamoja na mambo mengine, Mbowe alipata majina ya walinzi wa Sabaya na maeneo anayopendelea kutembea kutoka kwa Kaaya, ni sahihi?

Shahidi: Rudia swali

Nkungu: Kwa kuwa Kaaya alitoa majina na maeneo aliyokuwa anatembea Sabaya, hivyo  yalitoka kwa Kayaa?

Shahidi: Sahihi

Nkungu: Kwa kutoa hizo information alilipwa?

Shahidi: Sahihi

Nkungu: Na wewe hukuona kosa ukamuacha huru?

Shahidi: Kama nilivyoeleza walifikishwa mahakamani baada ya kujua hakuna ushahidi dhidi yake, akaondolewa

Nkungu: Ni shaihi alishiriki vikao na Mbowe?

Shahidi: Sahihi, lakini hakujua kile kikao kilikuwa kina lengo gani

Nkungu: Kwa uhakika kabisa alishiriki kikao cha kigaidi?

Shahidi: Hakushiriki kikao cha kigaidi.

Nkungu: lakini Mbowe alishiriki kikao cha aina gani?

Shahidi: Mbowe alishiriki kikao cha ugaidi

Awali akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando, Inspekta Swila alidai, Kaaya pamoja na watuhumiwa wengine wawili, Halid Athumani na Gabriel Mhina, waliondolewa mashtaka tarehe 27 Julai 2021 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kubainika ushahidi hauwahusu.

Shahidi huyo anaendelea kutoa ushahidi wake.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Sabaya afutiwa kesi, ruksa kugombea uongozi

Spread the loveMwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali DPP leo Ijumaa amefuta rufaa...

Habari za Siasa

Serikali yasaka bilioni 3 kujenga daraja Mto Mpiji

Spread the loveSerikali imesema inaendelea na juhudi za kutafuta fedha kiasi cha...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema kwafukuta kisa chaguzi, Lissu aibua tuhuma nzito

Spread the loveCHAGUZI za kusaka viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo...

Habari MchanganyikoTangulizi

Kimbunga “HIDAYA” chaendelea kuimarika, wananchi wapewa tahadhari

Spread the loveMAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa...

error: Content is protected !!