May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Jina la Hifadhi ya Burigi-Chato lapingwa bungeni

Spread the love

 

MBUNGE wa Biharamulo (CCM), Ezra Chiwelesa, ameiomba Serikali ya Tanzania, ibadili jina la Hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato, ili kuzima mjadala ulioibuliwa na baadhi ya watu, wanaopinga jina hilo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Chiwelesa ametoa ombi hilo leo Ijumaa, tarehe 4 Juni 2021, kwenye mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022, bungeni jijini Dodoma.

Hifadhi ya Taifa Burigi-Chato, iliyozinduliwa Julai mwaka 2019 na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania, Hayati John Magufuli, inaundwa na sehemu za wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera na Chato mkoani Geita.

“Hifadhi imekuwa na kelele kidogo, hasa kwa wakazi wa Biharamulo. lakini kikubwa kilichokuwepo ni jina la hifadhi. Maana kwetu sisi wakati hifadhi inaundwa, imechukua sehemu ya Chato na sehemu ya Biharamulo, ikiunganisha wilaya mbili kama hifadhi moja,” amesema Chiwelesa.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbaro

Akielelezea kiini cha mjadala huo, Chiwelesa amesema “lakini sasa kwa upande wa Biharamulo sababu pori lilikuwa linaitwa Burigi, wakazi wa Biharamulo walipoona pori inaundwa hifadhi na inabaki jina Burigi na huku chato, wakaona pori linasomeka chini ya Chato na hii hali imeleta kelele.”

Mbunge huyo wa Biharamulo, ameshauri jina la hifadhi hiyo libadilishwe kuwa Hifadhi ya Taifa ya Biharamulo-Chato, kwa kuwa sehemu kubwa ya hifadhi hiyo iko wilayani humo.

“Sasa nikuombe Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbaro, kwa sababu mbuga hii inaunganisha wilaya mbili, tuna Wilaya ya Biharamulo na Chato, ninaomba kwenye neno Burigi mridhie na kubali neno liwe Biharamulo,” amesema Chiwelesa na kuongeza:

“Mbuga isomeke Biharamulo Chato National Park, ili wakazi wa Biharamulo wanaobeba sehemu kubwa ya pori, waone kwamba juhudi hizo inaleta faida kwao, mchukue ushauri huu mkubali kubadili jina.”

error: Content is protected !!