October 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Jaji Warioba ataja mambo 7 yaliyompa heshima Nyerere

Spread the love

JAJI Mstaafu Joseph Warioba ametaja mambo saba yaliyompa heshima Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na kusisitiza kuwa kiongozi huyo alikataa kuitwa mtukufu.

Pia amesema licha ya kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa mcha Mungu hasa kwa kuhudhuria kanisani kila siku asubuhi, hakuwahi kusimama madhabahuni kuzungumza pindi akiwa Rais. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Jaji Warioba ametoa kauli hiyo leo tarehe 23 Aprili, 2022 nyumbani kwa Mwalimu Nyerere Msasani jijini Dar es Salaam katika sherehe za kumbukizi ya miaka 100 ya kuzaliwa kwa Rais huyo wa kwanza.

Akisimulia historia ya maisha ya Mwalimu Nyerere, Jaji Warioba ambaye pia ni waziri mkuu mstaafu amesema Baba huyo wa Taifa hakuwa na uchu wa madaraka.

Aidha, Jaji Warioba alitoboa siri kuhusu nyumba ya Mwalimu Nyerere kwamba licha ya kwamba nyumba hiyo aliijenga mwenyewe, lakini baadaye aliiuzia Serikali kisha akabaki kuwa mpangaji hadi alipong’atuka madarakani mwaka 1985.

Amesema baada ya kutoka madarakani, Serikali iliyokuwa inaongozwa na Rais Ali Hassan Mwinyi ilimrejeshea nyumba hiyo lakini Mwalimu Nyerere aliikataa kwa madai kuwa utajengeka utaratibu kwamba kila kiongozi anayetoka madarakani anakabidhiwa mali.

“Lakini baada ya mashauriano akakubali akakubali kuinunua hiyo nyumba na Mzee Mwinyi wakati huo nilikuwa msaidizi wake… akasema tutamuuzia kwa Shilingi moja, tukamwambia ukienda kumwambia Mzee mwenzako unamuuzia kwa shilingi moja atakataa ataona huo ni ujanja.

“Mzee Mwinyi akatuambia niachieni niyamalize haya na mzee mwenzangu, wakaenda wakaa wakakubaliana, Mwalimu akainunua kwa fedha za kutosha sio Shilingi moja ndio nyumba ikarudi mikononi mwake,” amesema.

Aidha, amesema ndani ya nyumba kuna chumba ambacho asilimia kubwa ya maamuzi ya Taifa yamefanyika ndani ya chumba hicho huku nje ya nyumba hiyo pakikutanisha wapigania uhuru wa mataifa mbalimbali.

“Mtaona mtu alivyokuwa anaishi, ukimwambia umpatie mahali penye nafasi anasema kwani mimi tembo, wengine tuna imani kwamba siku moja serikali kwa kushirikiana na familia wataweza kuacha rekodi ya pahala pale kwa sababu huwezi kuzungumzia historia ya Tanzania bila kuzungumzia nyumba hii,” amesema.

Ameongeza kuwa Mwalimu alikuwa muadilifu ndio maana aliichukia rushwa.

“Alikuwa muaminifu sana kwa nchi yake na wananchi, alikuwa na nidhamu ya hali ya juu, wapo hapa ambao tulifanya naye kazi,” amesema.

“Mwalimu hakuwa na mbwembwe wala makundi, alipokuwa rais watu walianza kumuita mtukufu, akakataa… akasema mtukufu ni Mungu tu binadamu hawezi kuwa mtukufu akasema mimi ni Mwalimu wa kawaida na ndipo tulipoanza kumuita mwalimu likawa na heshima, mke wangu sio first lady, ni Mama Maria tu.

Julius Nyerere, Hayati Baba wa Taifa

“Mwalimu hakuwa na uchu wa madaraka, mtakumbuka kama alivyokuwa akisema Makongoro, alitoroka kwa mwaka mzima akamuachia Kawawa, akaenda kuimarisha TANU, angeingia mtu mwingine pale angesema endelea na kazi hiyo unayofanya lakini Mwalimu hakujali hiyo hata mwisho aliamua mwenyewe kung’atuka… alitaka aondoke mwaka 1980 lakini wenzake wakamuomba aongeze mitano ili mambo fulani yaaandaliwe,” amesema.

Pamoja na mambo mengine Jaji Warioba, amesema Mwalimu Nyerere hakuwa na tamaa ya mali wala fedha.

“Alikuwa hatembei na fedha, huwezi kusikia maisha yake kwamba alilundika mali mahali, lakini kikubwa alijaribu kuishi kama mtu wa kawaida, hakusahau watu wa kawaida, marafiki zake, wananchi wa kawaida, wafanyakazi,” amesema na kuongeza;

“Alikuwa mtu ambaye anajali kila mtu, kuna rais anaweza kutoka kwenye ofisi yake na kumfuata karani wake ofisi kwake? lakini ndio uongozi!

Jaji Warioba amesema Mwalimu alikuwa anasikiliza ushauri kwa wale ambao walikuwa wanamsaidia na wale waliokuwa wanachangia mijadala kwenye vikao vya serikali, chama.

“Alikuwa na uwezo wa kuchangamsha mkutano, hata katika serikali alikuwa anafanya hivyo aliishi kwa vitendo, alichokisema kilitoka moyoni na alitenda hivyohivyo, kwa mfano aliposema tuache ubaguzi, alikuwa anashirikiana na viongozi wa kila rangi, dini kabila.

“Alikuwa binadamu mwema mwenye busara, hekima na hizi sifa ndizo zilizomfanya aendelee kuheshimika ndani na nje,” amesema Jaji Warioba.

error: Content is protected !!