Wednesday , 8 February 2023
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Wachezaji Simba onesheni ukubwa
Makala & UchambuziMichezo

Wachezaji Simba onesheni ukubwa

Spread the love

WEKUNDU wa Msimbazi, Timu ya Simba kesho inacheza mchezo wa marudiano wa hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini. Anaripoti Anicetus Mwesa, Dar… (endelea).

Mchezo huo unapigwa mjini Soweto nchini Afrika Kusini na kuchezeshwa na mwamuzi wa kati, Bernard Camille kutoka Shelisheli.

Simba inashuka dimbani kesho ikiwa na mtaji wa bao 1-0 ushindi iliyoupata katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, Jumapili iliyopita.

Mbali na Camille, waamuzi wasaidizi katika mchezo huo ni James Emile Fredrick pia kutoka nchini Shelisheli na Lionel Hasinjarasoa Andrianantenaina wa Madagascar. Mwamuzi wa akiba katika mtanange huo atakuwa Helder de Carvalho Martins wa Angola.

Timu imesafiri jana, hivyo tayari ipo bondeni Afrika Kusini ikisubiri kesho iingie diwani kulinda ushindi wake wa bao 1-0, sare ya aina yoyote au kusaka ushindi zaidi. Hakuna ubishi kwamba maandalizi yamekamilika.

Kwa muda mchache uliobaki hakuna mambo mengi ya kujiandaa, ni wachezaji kuingia uwanjani kuonesha talanta yao kwa kucheza kandanda safi litakalowawezesha kupata ushindi kwenye uwanja wa ugenini ili kusonga mbele kibabe.

Ni jambo la kushukuru, kwamba kikosi kimefika salama Afrika Kusini na kupokelewa na ubalozi wa Tanzania nchini humo, hivyo hakuna kitu kitakachokwenda vibaya. Kikubwa ni kwa benchi la ufundi kupanga kikosi kitakachoipeleka Simba katika hatua ya nusu fainali.

Niwaombe wachezaji kwamba ile ari ya kushinda katika uwanja wa nyumbani wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam muwe nayo vichwani mwenu. Mpambane kwelikweli ili kushinda ugenini.

Hivyo, ni muhimu wachezaji wa Simba wakacheza huku wakitambua kwenye kandanda lolote linawezekana, kushinda, kufungwa au kutoka sare iwe ugenini ama nyumbani.

Ikumbukwe ndani ya miaka mitano, Simba imecheza robo fainali tatu za CAF, kimsingi hayo ni mafanikio makubwa na jambo la kujivunia kwa wapenda kandanda nchini. Kwa maana hiyo sasa kwa robo fainali hii mnakila sababu ya kupambana kushinda mtinge nusu fainali.

Kwa kuwa uongozi umekusudia kutengeneza standard ya Tanzania kwenye michuano ya kimataifa. Aidha, kwa kuwa Simba imewafanya Watanzania waone kucheza robo fainali ni jambo la kawaida kila mmoja anakila sababu ya kuwaombea wachezaji wacheze kwa ari kubwa ili washinde.

Tambueni wapinzani wenu watashuka uwanjani kama tembo aliyejeruhiwa. Na hilo mnalitambua kwamba mmewajeruhi hivyo wamejipanga sawasawa, msiwe wanyonge kuwakabili kwa namna yoyote ile. Kila mchezaji anapaswa kuuangalia mchezo wa kesho kwa jicho la kipekee la kushinda au sare na si vinginevyo.

Kwa hiyo wachezaji wanatakiwa kujituma kwelikweli, kwamba yasifanyike makosa ya kizembe ndani ya dakika 90 za mchezo huo. Kwa kuwa tayari benchi la ufundi limeshamaliza kazi zake, kilichobaki ni kwa wachezaji washambuliaji kucheza kandanda safi na kupachika mabao, walinzi wakilinda lango lao ili lisikumbwe na madhara ya kufungwa.

Ni vizuri wachezaji mkajipanga ili kutumia vema dakika 90 kuamua hatima nzuri kwenu ya mashindano haya. Kimsingi itazameni nusu fainali sasa. Na iwapo mtafika hatua hiyo mtakuwa mnazidi kuandika rekodi Afrika na kuzidi kukonga nyoyo za mashabiki wenu na Watanzania kwa ujumla.

Pia niliombe benchi la ufundi kuandaa wachezaji kisaikolojia kwamba timu inaweza kushinda pia kwenye uwanja wa ugenini. Hivyo, wajitoe kwa asilimia 100 kuipambania timu ishinde.

Sahauni kabisa kauli alizozitoa kocha wa Orlando Pirates mara baada ya mchezo wa raundi ya kwanza uliochezwa wiki iliyopita.

Kila mchezaji wa Simba aseme imetosha kuishia robo fainali. Wapambanie ushindi ili iwe rahisi kwao kucheza nusu fainali ya michuano hiyo na ikiwezekana fainali kabisa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

ElimuMakala & Uchambuzi

Waraka maalumu kwa NECTA, “hawapaswi kuungwa mkono”

Spread the loveHATUA iliyotangazwa na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA), ya...

Michezo

GGML: Uwanja mpya wa Geita Gold FC kukamilika Mei, 2023

Spread the loveUWANJA wa Magogo unaojengwa na Halmashauri ya Mji wa Geita...

Michezo

Wanafunzi chuo Mwalimu Nyerere wapongezwa kwa ushindi

Spread the love  UONGOZI wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA)...

ElimuMakala & UchambuziTangulizi

Shule ya msingi yajengwa miaka 25 bila kukamilika, wanakijiji wachoka kuchangia

Spread the love  Wakazi wa Kijiji cha Makomba kilichopo kata ya Makazi...

error: Content is protected !!