October 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

IGP Sirro aagiza aliyetishia kwa bastola, akamatwe

IGP Simon Sirro

Spread the love

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, Simon Sirro amesema kijana aliyefahamika kwa jina moja la Shaban, atakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani, kwa kosa la kumtishia mwenzake na bastola. Anaripoti Martin Kamote … (endelea).

Akizungumza na wanahabari leo tarehe 1 Novemba 2019 jijini Dar es Salaam, IGP Sirro amesema mtu anayekiuka masharti ya kumiliki silaha, hunyang’anywa silaha na kufikishwa mahakamani .

“Kimsingi mtu unapopewa silaha ufuate hayo masharti, usipofuata masharti  la kwanza, tutakunyang’anya silaha,  la pili tutakupeleka mahakamani, la tatu tutamuomba Mungu atusaidie tukufunge ili ukirudi nyumbani kwako uwe na adabu ya kutumia silaha,” amesema IGP Sirro.

IGP Sirro amemtaka Shaban kujisalimisha katika kituo cha polisi, sambamba na kusalimisha silaha yake.

Amesema,  Shaban amekiuka masharti ya kumiliki silaha, kufuatia hatua yake ya kumtishia mwenzie, aliyekuwa anajibizana nae.

“Sisi silaha tuliwapa kwa masharti maalumu,  hatukuwapa silaha kwa ajili ya kutishia Watanzania, tukibaini umetishia watanzania kama alivyofanya yule  kijana, hatujui ugomvi ulikuwa ni nini. Lakini je,  kama ni kweli yale yaliyokuwa yanaelezwa,  alikuwa na sababu za kutoa silaha kumtishia mwenzake?” amehoji IGP Sirro.

Hivi karibuni ilisambaa video katika mitandao ya kijamii, inayomuonesha Shaban akitishia kumdhuru na bastola, mwanaume ambaye jina lake halijafahamika.

Kitisho hicho cha Shaban kilifuata kutokana na majibizano yaliyozuka baina yake na huyo mwenzie.

error: Content is protected !!