MKUU wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania, IGP Camillus Wambura, amewasimamisha kazi askari wote waliohusika na tukio la mauji ya raia wawili yaliyotokea tarehe 23 Oktoba, 2022 katika Kijiji cha Ikwambi Kata ya Mofu wilayani Kilombero mkoani Morogoro, ili kupisha uchunguzi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Mauji hayo yalitokea kufuatia vurugu za wananchi jamii ya wafugaji na wakulima ambao walikuwa wanalalamikia mifugo kuingizwa kwenye mashamba yao na wenzao wawili kushambuliwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya IGP Wambura aliyoitoa leo Jumatatu tarehe 24 Oktoba, 2022, amesema ameunda timu ya uchunguzi itakayoongozwa na Mkurugenzi wa Mashitaka pamoja na taasisi zingine za Serikali ili kufanya uchunguzi huru.
Amesema katika taarifa yake hiyo kuwa lengo la uchunguzi huo ni kupata majibu ya chanzo cha tukio hilo na kubaini uwiano wa matumizi ya nguvu iliyotumiwa na Jeshi la Polisi katika kudhibiti vurugu na endapo zilienda sambamba na vurugu zenyewe.
“Nimeelekeza kuwa askari wote waliohusika kwenye tukio hilo wakae kando kupisha uchunguzi ili timu hii huru iwe na nafasi nzuri ya kuweza kutimiza wajibu wake na kuweza kuja na majibu na matokeo sahihi ya uchunguzi huo kwa jamii ili Watanzania waweze kufahamu ukweli wa tukio hilo.
“Endapo kutabainika mapungufu, madhaifu au chochote kile amabcho kinaonesha uzembe kwa upande wa yeyote yule, basi hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” amesema Wambura.
Leave a comment