Friday , 26 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Hukumu ya Mbowe: Hivi ndivyo hakimu alivyomkwepa Akwilini
Habari za Siasa

Hukumu ya Mbowe: Hivi ndivyo hakimu alivyomkwepa Akwilini

Spread the love

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imesema hukumu yake juu ya kesi ya jinai Na. 112/2018 iliyokuwa ikiwakabili viongozi waandamizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), haikuzingatia suala la mauaji ya Akwilina Akwilini, aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT). Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza wakati anasoma hukumu ya kesi hiyo jana tarehe 10 Machi 2020, Thomas Simba, Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, amesema hakutaka kugusa suala hilo kwa sababu “sheria haikumruhusu.”

Hakimu Simba amesema “mauaji ya Akwilina” ilikuwa ni hoja ya upande wa mashtaka kwa ajili ya kuipa nguvu kesi hiyo. Kisheria, amesema Hakimu Simba, suala hilo liko chini ya mamlaka za kiuchunguzi kwa ajili ya kuandaliwa mashitaka yake mahsusi.

“Mada ya kesi ya Akwilina haipo, wala sitaki kuigusa kwa sababu ni maneno ya upande wa mashtaka kusapoti kesi yao. Kisheria waacheni wapelelezi wapeleleze. Na wala sitaki kujua kama amekufa au hajakufa, sheria imenikataza (kushughulikia hilo). Ikija kesi ya Akwilina kufunguliwa nitaisikiliza,” amesema Hakimu Simba.

Mauaji ya Akwilina yalitokea eneo la Kinondoni Mkwajuni wakati msichana huyo akiwa ndani ya basi likitokea Mabibo kwenda Stendi ya Makumbusho. Alipigwa risasi wakati wa hekaheka za Jeshi la Polisi katika kudhibiti maandamano ya wanachama wa Chadema yaliyotokea uwanja wa Buibui, Kiondoni ambako chama hicho kilikuwa kinakamilisha mikutano ya kampeni ya uchaguzi mdogo wa ubunge Kinondoni.

Tukio hilo ndilo lilizalisha purukushani na hatimaye viongozi kadhaa wa Chadema kukamatwa na kuishia kushitakiwa kwa tuhuma za uchochezi. Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, jina la Akwilina lilitajwa kwenye shtaka la nne ikidaiwa kuwa viongozi wa Chadema kukaidi amri ya polisi ya kuacha kufanya mkusanyiko haramu, kulizua vurugu na kusababisha mauaji hayo kutokea.

Ilidaiwa pia kuwa ukaidi huo katika tukio la tarehe 16 Februari 2018, ulisababisha polisi wawili kujeruhiwa.

Maandamano yalilenga kwenda kumshinikiza Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, atoe barua za kuidhinisha mawakala wa uchaguzi wa chama hicho.

Viongozi waliohusishwa katika kesi hiyo wakiongozwa na Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Taifa, ni pamoja na wajumbe wa Kamati Kuu ya chama akiwemo John Mnyika, mbunge wa Kibamba ambaye sasa ni Katibu Mkuu aliyechukua nafasi ya Dk. Vincent Mashinji aliyekuwepo wakati ule lakini akiwa amehama na kukimbilia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wengine ni Halima Mdee (Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake –Bawacha), John Heche (Mbunge wa Tarime Vijijini), Esther Matiko (Mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti), Mchungaji Peter Msigwa (Mbunge wa Iringa mjini na Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa), Esther Bulaya (Mbunge wa Bunda Mjini) na Salum Mwalimu (Naibu Katibu Mkuu Zanzibar).

Wote walitiwa hatiani kwa mashtaka 12 yaliyothibiti na jana kuhukumiwa kulipa faini inayofikia Sh. milioni 355 au kutumikia vifungo vya miezi mitano kila mmoja gerezani. Jana walipelekwa gerezani kusubiri taratibu za kulipa faini ili kukwepa kufungwa.

Suala hilo la kuuawa kwa Akwilina ndilo hasa lililozidisha hofu fikirani mwa washitakiwa hao kuwa hwenda wangehukumiwa kufungwa gerezani.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

error: Content is protected !!