MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tanzania, John Heche amesema Serikali iiliyopo madarakani imeshindwa kutatua changamoto za wananchi hivyo “inapaswa kuondoka madarakani na kuwaachia wanaoweza.” Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Heche ameyasema hayo leo Alhamisi tarehe 14, Julai, 2022, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali yanayoendelea nchini.
Kada huyo wa Chadema ambaye amewahi kuwa mbunge wa Tarime Vijiji, amesema wajibu namba moja wa Serikali yeyote duniani ni kukusanya kodi kutoka kwa umma na kupeleka huduma,“na wakati wote kuhakikisha wananchi wanatoka kwenye hali ngumu ya kimaisha kwenda kwenye unafuu wa kimaisha.”
Heche amesema “kwa bahati mbaya sana” sehemu kubwa ya Afrika Serikali zinatumikisha wananchi badala ya kuwatumikia na kwamba inatokana na viongozi “kuwa vibaraka, kushindwa kusimamia majukumu yao na kushindwa kusimamiwa vizuri na Mabunge na Mahakama.”
“Na sisi wajibu wetu ni kukumbusha wananchi kwamba kama wamechagua mtu anapaswa kuwatumikia wao kwanza kwasababu bila wananchi hakuna nchi kwasababu wao wamewekwa na watu,” amesema Heche.
Heche amesema nchi “ni kichekesho” kwamba nchi ambayo vijana wake hawana ajira, asilimia 90 ya ngano inayotumia inaagizwa kutoka nje.
“Watu waliopo Serikali ni watu walioshindwa Serikali yenyewe imeshindwa inatakiwa kutoka madarakani iwaachie watu wanaoweza kushughulikia matatizo ya watu,” amesema.
Katika mkutano huo Heche ameeleza namna Serikali inavyochangia kupanda kwa bei ya nishati ya mafuta kutokana na tozo na kodi zilizowekwa.
Amesema licha ya ukweli kwamba bei hiyo imethiriwa na Uviko-19 na vita ya Ukraine na Urusi lakini kwa kiasi kikubwa ni tozo na kodi za Serikali.
Leave a comment