August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Washauri uchaguzi, mikutano ya siasa ifanyike kidigitali

Dk. Wilson Mahera

Spread the love

 

SERIKALI imeshauriwa kutumia teknolojia katika chaguzi na mikutano ya vyama vya siasa ili kupunguza gharama za uendeshaji wa shuguli hizo. Anaripoti Selemani Msuya, Dar es Salaam … (endelea).

Ushauri huo umetolewa na Wizara ya Fedha na Mipango ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakati ikiwasilisha maoni na mapendekezo yake kwa Kikosi Kazi cha Rais jijini Dar es Salaam.

Ushauri huo wa Wizara ya Fedha unaungana na ule uliotolewa na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dk. Wilson Mahera alipowasilisha maoni yake kwa Kikosi Kazi hicho hivi karibuni.

Akiwasilisha maoni na mapendekezo hayo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Zanzibar, Rashid Said Rashid, amesema ili kupunguza gharama kubwa za uchaguzi na kuondoa malalamiko ya mikutano ya kisiasa ni vema serikali ikaanza kufikiria na kuona haja ya kutumia teknolojia ya kisasa kwenye kuendesha michakato hiyo.

Amesema ili kufanya uchaguzi inahitajika vifaa mbalimbali kama karatasi, magari, wasimamizi na mambo mengine ambayo gharama zake ni kubwa hivyo teknolojia ndio njia sahihi katika kupunguza gharama.

Rashid amesema mfumo wa kidigitali upo wazi kuanzia hatua ya awali ya kupiga kura hadi kutangazwa matokeo.

“Sisi tumechangia maeneo makuu matatu, mosi ni elimu ya uraia, uchaguzi na uwakilishi wa wanawake. Hapa kwenye uchaguzi na elimu ya uraia tungependa nchi ianze kutumia teknolojia kwani tutapunguza gharama za kuchapisha makaratasi, kuweka mawakala na mengine,”amesema.

Naibu Katibu huyo amesema kwa kuwa kitambulisho cha Taifa kina sifa za kiteknolojia hivyo ni vema kuanzia hapo.

Amesema faida nyingine ambayo itapatikana kwa kutumia mfumo wa kidigitali ni vyama vya siasa kuacha kutumia mawakala kwenye vituo na kuondoa malalamiko na wasiwasi uliojengeka na baadhi ya watu juu ya utendaji wa tume ya uchaguzi.

Rashid amesema uwekezaji wa mfumo huo una gharama kubwa lakini faida zake ni kubwa kuliko kuendelea na mifumo inayotumika kwa sasa.

“Sisi kama Wizara ya Fedha na Mipango tunachoangalia ni namna ya kuokoa fedha na tumeona mfumo wa teknolojia ni mwarobaini,” amesema.

Naibu huyo amesema iwapo teknolojia hiyo itafanya kazi fedha zitakazookolewa zitaelekezwa kwenye matumizi mengine.

Naibu Katibu Mkuu huyo amesema wajumbe wa kikosi kazi wamepokea wazo hilo kwa mtazamo chanya ambapo wamepewa kazi ya kwenda kufanya tathmini iwapo wataanza kutumia mfumo huo serikali itaokoa kiasi gani cha fedha na kuelekezwa sehemu nyingine.

Akifafanua kuhusu teknolojia kutumiwa na vyama vya siasa kujijenga amesema hakuna haja ya vyama hivyo kuzunguka kila mahali kutoa elimu ya uraia wakati teknolojia ipo.

Amesema mfumo wa kidigitali au teknolojia unawezesha vyama kuwafikia wanachama na wananchi kwa urahisi na gharama ndogo, hivyo ni vema navyo vikaanza kufikiria njia hiyo.

“Mfano waandishi wa habari wanakaa kwenye vyombo vyao au kupitia mitandao yenu ya kijamii Facebook na Twitter mnawasiliana na watu hata kiongozi wa chama anaweza kufanya hivyo,

“Tunaona Rais wetu Zanzibar anafanya hivyo vikao kila mwezi ambapo anaeleza namna Serikali yake inavyofanya kazi kwanini vyama vya siasa visifanye hivyo, pia vitaondoa misuguano na Jeshi la Polisi,”amesema.

Rashid amesema njia ya kidigitali inamuwezesha Rais kuwasiliana na Watanzania wote ikiwemo wanaoishi nje.

Kwa upande mwingine amesema ushiriki wa wanawake na mahitaji maalum nalo linapaswa kupewa kipaumbele katika utoaji wa elimu ya kiraia.

error: Content is protected !!