Tuesday , 30 April 2024
Home Hatimaye muswada marekebisho sheria ya habari watinga bungeni, TEF yampongeza Rais Samia

Hatimaye muswada marekebisho sheria ya habari watinga bungeni, TEF yampongeza Rais Samia

MUSWADA wa Marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari ya 2016, umesomwa kwa mara ya kwanza bungeni jijini Dodoma, kupitia Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa 2023. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Muswada huo umesomwa leo Ijumaa, tarehe 10 Februari 2023, bungeni jijini Dodoma.

Baada ya muswada huo kusomwa, Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, alisema utapelekwa katika kamati husika za mhimili huo ili ufanyiwe kazi.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, muda mfupi baada ya muswada huo kusomwa bungeni, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa hatua hiyo, huku akibainisha kwamba jukwaa hilo linaamini mapendekezo yaliyotolewa na wadau juu ya marekebisho ya sheria hiyo yamezingatiwa.

Balile amesema kuwa, marekebisho ya sheria hiyo ya habari yakikamilika, yatapandisha hadhi ya Tanzania kimataifa, hususan katika kipengele cha uhuru wa habari. Lakini pia, yataimarisha demokrasia na utawala bora nchini kwa kuwa vyombo vya habari vitatimiza majukumu yake ya kuhabarisha, kuonya na kuelimisha umma.

Aidha, Balile ameipongeza Serikali kwa kuuwasilisha bungeni muswada huo kwa njia ya kawaida badala ya dharura, kwa kuwa wabunge na wadau watapata nafasi ya kuujadili kwa ajili ya maboresho zaidi.

Naye Mjumbe wa TEF, Salim Said Salim, amesema “tunachotaka Watanzania wawe Taifa la watu wanaosema, ikiwa unatoa uhuru wa habari, uhuru wa kujieleza, panaweza kuwa tofauti vile mtu anavyotafisiri lakini kusikia sauti hii ndiyo kujenga demokrasia.”

Muswada huo umewasilishwa bungeni baada ya kukwama Novemba mwaka jana, ambapo Serikali iliahirisha kuuwasilisha kwa ajili ya kutoa nafasi kwa wadau kutoa mapendekezo yao juu ya namna ya kuuboresha ili ipatikane sheria bora isiyokuwa na malalamiko.

error: Content is protected !!