August 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Gesi asilia kuinua uchumi wa wananchi

Mhandisi Haruna Mchessu wa Kampuni ya Maurela & Prom inayomiliki visima vya gesi asilia eneo la Mnazi Bay Mtwara akiwaelezea waandishi namna wanavyozalisha gesi na kusafirisha kwa wateja.

Spread the love

IMEELEZWA kwamba iwapo Tanzania itawekeza kwenye utafutaji na uchimbaji wa gesi asilia iliyogundulika nchini uchumi utakuwa na kupunguza ugumu wa maisha. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Serikali kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali hadi sasa Tanzania imegundua futi za ujazo trilioni 57 za gesi asilia majini na nchi kavu ambapo hadi sasa ilichimbwa katika visima 44 kati 96 ni chini ya asilimia 1 ya gesi yote.

Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki mkoani Lindi, Mkuu wa Kitengo cha Ushiriki wa Wazawa na Ushirikishwaji wa Wadau wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Charles Nyangi alisema gesi asilia ni nishati safi na rahisi ambayo inaweza kutumia na kila Mtanzania kwa gharama ndogo.

Mhandisi Msafiri Joseph wa Kampuni ya GASCO, akitoa maelezo kwa mteja wa gesi asilimi Mtwara mjini Theresia Ndoromi

Nyangi alisema maeneo ambayo kwa asilimia kubwa yanazalisha gesi asilia ni Songo Songo Kilwa na Mnazi Bay Mtambaswala ambao wanawauzia wazalishaji wa nishati mbalimbali.

Alisema upatikanaji wa gesi asilia umewezesha Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuzalisha umeme na kusambaza kwa wananchi kupitia Kampuni Tanzu ya GASCO ambayo ina kituo chake eneo la Madimba mkoani Mtwara.

Nyangi alisema pia Kiwanda cha Saruji cha Dangote mkoani Mtwara ni moja ya kiwanda kinachonufaika na gesi asilia inatoka katika visima vilivyochimbwa.

“Dhumuni la ziara hii lilikuwa ni kuwapatia uelewa kuhusu masuala ya mafuta na gesi, namna ambavyo gesi inapunguza ukali wa maisha kuanzia majumbani, viwandani na kwenye magari.

Sisi PURA tutahakikisha wawekezaji wanakuja kuchimba gesi katika maeneo ambayo yamegundulika kwani utafiti umeonesha nishati hiyo ya gesi asilia ni rahisi na inaweza kutumiwa na wananchi wote,” alisema.

Mitambo ya kupokea na kusafirisha gesi asilia iliyopo katika Kituo cha Somanga Fungu wilayani Kilwa mkoani Lindi

Nyangi alisema utafutaji na uchimbaji wa gesi unahitaji fedha nyingi, hivyo kuwaomba wazawa kuchangamkia fursa hiyo, kwa kuwa soko lake ni la uhakika ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake Msimamizi wa Shughuli za Uzalishaji na Matengenezo ya Mitambo ya Kiwanda cha Kampuni ya GASCO, Mhandisi Kassim Mkombwa alisema, uwekezaji katika eneo hilo ni gharama ila faida zake ni kubwa kwa nchi.

Mhandisi Mkombwa alisema itakuwa vizuri iwapo tafiti katika eneo hilo zitaongezeka, ili uti za ujazo trilioni 57 zilizogundulika ziweze kuvunwa kwa wingi.

“Tanzania tumejaliwa rasilimali madini nyingi ikiwemo gesi, rai yangu ni tafiti kuongezeka ili kuhakikisha Watanzania wananufaika zao, kama ambavyo tumeanza kunufaika na gesi, kwani kwa sasa asilimia 60 ya nishati ya umeme inatokana na gesi asilia,” alisema.

Mkombwa alisema katika kiwanda hicho cha GASCO Madimba mitambo waliyonayo wanaweza kuchakata futi za ujazo milioni 210 za gesi asilia kwa siku, hivyo kuwaomba wawekezaji kuendelea kutafiti na kuchimba gesi hiyo.

Mwananchi wa Mtwara mjini Theresia Ndoromi akisha jiko ambalo linatumia gesi asilia

Mkuu wa Uzalishaji wa Kampuni ya Maurel &Prom ya Mnazi Bay Mkoani Mtwara, Hussein Chitomo alisema uchimbaji na utafutaji wa gesi asilia unahitaji gharama ila ikipatikana mahitaji yake ni makubwa.

Alisema tangu mwaka 2006 hadi sasa wamezalisha gesi asilia yenye futi za ujazo zaidi ya bilioni 125 na kuzipatia TPDC na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mkoa wa Mtwara.

“Sisi tuna wateja wawili ambao ni TPDC na TANESCO Mtwara ila TANESCO tunawapatia gesi asilia iliyochakatwa ili na TPDC wanachukua ambayo haijachakatwa hadi hatua ya mwisho ambao nao wanachaka na kuwapekea wateja wao,”alisema.

Alisema nishati hiyo gharama yake ni ndogo, lakini pia ni safi na salama kwa matumizi ya kila eneo ambalo linahitaji nishati.

Naye mtumiaji wa gesi Mtwara, Theresia Ndoromi alisema ujio wa gesi asilia umeweza kumpunguzia gharama za maisha ambapo kwa sasa anaweza kutumia Sh.10,000 kwa mwezi tofauti na awali ambapo alikuwa akitumia hadi Sh.50,000.

error: Content is protected !!