Saturday , 4 May 2024
Home Habari Mchanganyiko EWURA yateta na Wahariri, “ruzuku bilioni 100 imepunguza maumivu”
Habari Mchanganyiko

EWURA yateta na Wahariri, “ruzuku bilioni 100 imepunguza maumivu”

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile (kushoto aliyesimama) akizungumza kwenye mkutano huo.
Spread the love

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imesema, uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kutoa ruzuku ya shilingi bilioni 100 kupunguza bei za mafuta hapa nchini imeleta nafuu kubwa mitaani. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa jana tarehe 16 Julai, 2022 na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Mhandisi Modestus Lumato katika kikao kazi cha siku moja na wahariri mbalimbali wa vyombo vya habari nchini kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

Amesema hivi karibuni Rais Samia aliagiza ruzuku ya shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kukabiliana na kupanda kwa bei kuanzia mwezi Juni ili kukabiliana na upandaji wa bei za mafuta hapa nchini.

“Suala kubwa la mafuta kupanda bei ni la dunia, lakini kila mmoja anahangaika kuona anafanyaje kwa sababu kila mmoja analia kivyake, ndiyo maana kama mnakumbuka Rais Samia amekubali kutoa ruzuku angalau kupunguza ingawa kwa macho haionekani, kwa sababu unaongeza shilingi 500, halafu yenyewe yanaongezeka shilingi 700 sasa ukiitoa huku kwa wananchi wenyewe hawaioni wanaona tena shilingi 200 imeongezeka kumbe ilikuwa imeongezeka shilingi 700,” amesema Mhandisi Lumato na kuongeza;

“Sasa, kila kukicha na sisi tunazidi kuangalia ni wapi tunaweza kusaidia kuweza kupunguza hata ninyi (wahariri) kama mna solutions au mna mawazo napenda kuyasikia mawazo yenu niyachukue kama mnafikiri ni wapi tunaweza tukasaidia katika suala hili la kupunguza bei kwenye mafuta.”

Mhandisi Lumato akizungumzia kwa upande wa nishati mbadala amesema gesi ni miongoni mwa maeneo ya vipaumbele kwa mamlaka hiyo katika kuona inatumika katika kuendeshea vyombo vya moto nchini hususani magari.

Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Mhandisi Modestus Lumato (kulia aliyesimama) akizungumza katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam, kushoto ni Mwenyekiti wa Jukwaa la wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile.

“Kwenye suala la alternative fuel na kwenda kwenye gesi hili ni moja ya kazi ambayo kwa EWURA kwa mwaka huu wa bajeti tumeweka kipaumbele, kwa hiyo kama mnakumbuka hapo katikati kama wiki mbili zimepita tuliita wadau wote wanaotumia gesi, wanaozalisha gesi, wanaounganisha magari na wanaouza kwenye vituo vya kuzalishia ili kutafuta changamoto zinazosababisha watu wengi wasibadilishe magari kwenda kwenye gesi.

“Sababu kuna faida kubwa, ukitumia gesi kama ulivyosema ukitumia gesi kwa shilingi 17, 000 unaenda kilomita 300, lakini mafuta utatumia ya shilingi ngapi mpaka uende kilomita 300? Ukitumia mafuta ni kiasi kikubwa sana, lakini tulikuwa tunatafuta kwa nini watu hawabadilishi? Tumepata baadhi ya majibu mengi tu mojawapo kubwa ni elimu, elimu haijaenda kwa watu hawajaelewa faida yake.

“Yaani wanaangalia ile hela ya kubadilishia gari ile peke yake bila kujua ile hela ya kubadilishia gari ndani ya miezi miwili au mitatu inakuwa imerudi akiwa anatumia gesi, sasa wahariri ndio sehemu yenu sasa mnatakiwa mtusaidie kuelimisha watu tukija tukawaonesha, tukawaelimisha zile hesabu zake jinsi anavyoweza kusave halafu na ninyi mkaenda kuwaambia watu watakimbia kubadilisha,”amesema Mhandisi Lumato.

Amesema tatizo lingine lilikuwa ni vituo kwani viko viwili tu mpaka sasa, lakini hilo nalo wameshalitafutia suluhisho kwa kuruhusu wenye vituo vya mafuta waweke na vituo vya gesi.

Amesema wameshapewa vibali kwa sababu mwenye jukumu hilo kubwa la kusambaza gesi kwa watu alilopewa kisheria ni Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania.

“Lakini pia TPDC ameruhusiwa kugawa hilo jukumu kwa watu wengine, kwa hiyo wengi wameshapewa Concert ya TPDC na wameshakuja kwetu (EWURA) tumewaruhusu waende wakajenge.

Amesema pia wa mabasi ya mwendokasi Dar es salaam – DART wamewashawishi watumie gesi ili nauli isipande kwani wakitumia gesi gharama za uendeshaji zitapungua.

Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA. Titus Kaguo akizungumza kwenye kikao hicho alipokuwa akiwakaribisha wahariri wa vyombo vya habari (hawapo pichani) kwenye kikao hicho kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam.

“Na baada ya muda wataweza kubadilisha na hata yaliyokuwepo hayo yakaanza kutumia gesi kwa sababu teknolojia zote zipo. Kwa mfano Dangote. Dangote, yale malori yake kama 600 yamebadilisha yanatumia gesi kwa hiyo ana kituo chake kule Mtwara anajaza, akijaza yakifika hapa Dar es Salaam yanaweza kuwa yamefika nusu ya ile mitungu anajaza tena Dar es Salaam anasogea anafika tena Dodoma,” amesema.

Akizungumzia kwa upande wa maji, Mhandisi Lumato amesema sasa kuna ahueni ukilinganisha na huko nyuma bila EWURA kwa sababu EWURA ndiye anazisimamia mamlaka zote za maji ndiye anayeenda kuzikagua na kuangalia service wanayotoa inafanana na anacholipa mwananchi? Sababu kuna wakati unakuta unalipa hewa, mita inasoma maji hayatoki.

Awali, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bw. Deodatus Balile amesema, vyombo vya habari nchini vitaendelea kufanya kazi kwa karibu na taasisi zote ikiwemo EWURA ili kuhakikisha vinafikisha taarifa mbalimbali kwa umma kwa wakati.

“Tuna magazeti ambayo yanafanya kazi nzuri, radio na Tv tuombe ule ushirikiano uliokuwepo unaoendelea kuwepo wa matangazo ya hapa na pale yanapopatikana kuyagawa, tukukaribishe na kwa pamoja tuone namna gani tunaijenga hii nchi yetu.

“Tunaomba tukukaribishe kwenye tasnia yetu…umeingia kwenye kipindi kuna dirisha zuri sana la matumizi ya gesi. Mwezi wa kwanza tuliandika habari chache sana tukiwaambia wananchi faida za gesi kwenye magari badala ya petroli, tulikuwa tuna magari kama tisa hivi, lakini wiki iliyopita tulikuwa tuna magari zaidi ya 1,000 hapa Dar es Salaam ambayo yameconvert kwenda gesi,” amesema Balile.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

RPC Dodoma akabidhiwa bunduki mbili za wahalifu

Spread the love  Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa ya Kulevya...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NBC yazindua huduma maalum kwa wastaafu

Spread the loveBenki ya Taifa ya Biashara (NBC) imezindua huduma maalum kwa...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB yazindua akaunti ya Kikundi

Spread the loveBenki ya NMB imezindua akaunti ya kikundi yenye  maboresho makubwa...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Wafanyakazi waidai STAMICO mishahara ya bilioni 1

Spread the loveWALIOKUWA wafanyakazi wa mgodi wa Shirika la Madini la Taifa...

error: Content is protected !!