KATIBU Mkuu wa Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), Nusrat Hanje, Mratibu wa Uhamasishaji wa baraza hilo, Twaha Mwaipaya na wenzao sita wameachiwa huru baada ya kufutiwa mashtaka yaliyokuwa yanawakabili katika Mahakama ya Mkoa wa Singida. Anaripoti Mwandishi Wetu, Singida … (endelea).
Hanje, Mwaipaya na Samwel Gishinde Malo, Katibu wa Chadema mkoani Singida na wengine watano walikamatwa na Jeshi la Polisi mkoani humo tarehe 6 Julai 2020 wakituhumiwa kufanya mikusanyiko isiyo halali.
Wanasiasa hao wameachiwa huru jana usiku Jumatatu tarehe 23 Novemba 2020, baada ya kusota rumande mkoani Singida kwa muda zaidi ya mitano sawa na siku 170.
Hanje, Mwaipaya na wenzao walifunguliwa Kesi ya Jinai Namba 115/2020, katika Mahakama ya Mkoa wa Singida wakikabiliwa na mashtaka manne ikiwemo mkusanyiko usio halali, kudharau wimbo na bendera ya taifa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Chadema katika ukurasa wake wa Twitter, viongozi hao wa Bavicha wameachiwa usiku wa jana tarehe 23 Novemba 2020 baada ya Mkurgenzi wa Mashtaka (DPP) kuwafutia mashtaka.
“Katibu Mkuu wa Bavicha Nusrat Hanje na Mratibu wa uhamasishaji Bavicha Taifa Twaha Mwaipaya na wenzao sita wameachiwa huru usiku huu. Upande wa Jamhuri hawapo tayari kuendelea na kesi, hivyo wamefutiwa mashtaka yao,” inaeleza taarifa hiyo.
Leave a comment