June 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Mollel: Wananchi hawataki katiba mpya, wanataka maendeleo

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto nchini Tanzania, Dk. Godwin Mollel

Spread the love

 

NAIBU Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, amedai kwamba wananchi hawataki katiba mpya, bali wanataka maendeleo na huduma bora za kijamii. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mtwara … (endelea).

Dk. Mollel ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, tarehe 26 Julai 2021, katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi la Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini, mkoani Mtwara.

Naibu waziri huyo wa afya, amedai kuwa, wananchi wanaunga mkono msimamo wa Serikali wa kuweka kando mchakato wa upatikanaji katiba mpya, ili kuimarisha maendeleo ya nchi.

“Vijana wa Tanzania wako pamoja na nyie, nimezungumza katika ziara yangu jimboni kwangu na katika mikoa mitano, hakuna anayezungumzia katiba mpya, wote wanataka dawa, maji, huduma bora za afya na kupunguza vifo vya kina mama na watoto,” amesema Dk. Mollel.

Dk. Mollel amesema kuwa, badala ya Serikali kutumia fedha katika kuendesha Bunge la Katiba, ipeleke fedha hizo katika miradi ya maendeleo.

“Badala ya sisi kukaa bungeni kutumia fedha kutunga katiba mpya, fedha hizo mmeamua kutupa Sh. 6.5 bilioni, tuwanunulie watu wa Mtwara vifaa tiba na hospitali yao ianze,” amesema Dk. Mollel na kuongeza:

“ Badala ya sisi kutumia pesa kwenda kukaa kujadili katiba, mmeamua kutoa Sh. 157 bilioni zijenge bandari Mtwara, ambayo haitagusa watu wa korosho peke yake, itaongeza ajira kwa vijana.”

Kauli hiyo ya Dk. Mollel imekuja huku kukiwa na vuguvugu la madai ya katiba mpya, yaliyoibuliwa na baadhi ya makundi hasa ya vyama vya siasa na asasi za kiraia.

error: Content is protected !!