June 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

RC Dar: Kila mtu avae barakoa kwenye daladala, sokoni

Spread the love

 

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC) nchini Tanzania, Amos Makalla amepiga marufuku wananchi mkoani humo kuingia kwenye vyombo vya usafiri na sehemu za kutoa huduma pasipo kuvaa barakoa huku akitaka mabasi kuzingatia ‘level seat.’ Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

RC Makalla ametoa agizo hilo leo Jumatatu, tarehe 26 Julai 2021, ili kuendana na mwongozo uliotolewa na wizara ya afya wa tahadhari ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona.

Amesema watafanya ziara za kustukiza kwenye vituo vya daladala, feri, stendi, stendi za mabasi ya mwendokasi, maeneo ya masoko na sehemu zote za kutoa huduma ili kuangalia utekelezaji wa agizo hilo.

Mkuu huyo wa mkoa, amewataka wananchi kuchukuwa tahadhari dhidi ya ugonjwa wa corona.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC) nchini Tanzania, Amos Makalla

Aidha, Makalla amesema Serikali imejipanga kutoa huduma bora za matibabu kwa wagonjwa wote watakaofika hospital na kuwataka wananchi watakaoona dalili za corona kuwahi vituo vya Afya.

Katika mwongozo huo uliotolewa na wizara ya afya inazungumzia tahadhari kwenye vyombo vya usafiri na stendi za mabasi, daladala au bodaboda ambapo corona inaweza kusambazwa.

Miongozo hiyo sita kwenye vyombo vya usafiri ni;

i. Wasafiri wawezeshwe kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka kabla ya kuingia kwenye vyombo vya usafiri hivyo, viongozi wa mtaa husika wahakikishe kuna vyombo vya kuhifadhia maji na sabuni vya kutosha katika kila kituo. Aidha, uongozi wa vituo vya mabasi usimamie uwepo wa vifaa vya kunawia kwa maji tiririka na kuhakikisha abiria wote wananawa mikono.
ii. Wamiliki wa vyombo vya usafiri wahakikishe wanaweka vipukusi vya kutakasa mikono katika vyombo vya usafiri.
iii. Kila msafiri anayeingia kwenye chombo cha usafiri wa umma lazima awe amevaa barakoa kama ilivyoelekezwa kwenye mwongozo isipokuwa watoto wenye umri wa chini ya miaka 8.
iv. Abiria wote waendelee kuelimishwa kuhusu umuhimu wa kutosongamana ndani ya vituo vya Mabasi kupitia walinzi getini, wahudumu wa mabasi na askari wa usalama wa barabarani.
v. Bodaboda wabebe kwa idadi sahihi (1-2) (siyo mishikaki) na wavae barakoa
vi. Stendi zihakikishe zinatoa ujumbe wa kuelimisha jamii ya wasafiri mara kwa mara kupitia vipaza sauti, na wanapokuwa safarini, madereva na wahudumu wa vyombo vya usafiri
wahakikishe ujumbe wa kuelimisha unatolewa kwenye chombo mara kwa mara.
vii. Wananchi wakae au kuongozana kwa umbali wa zaidi ya mita moja katika maeneo yote
wanayokuwepo kabla ya kuingia kwenye chombo cha usafiri.
viii. Vyombo vya ulinzi na usalama vihakikishe magari ya usafiri wa umma wanapakia abiria
kulingana na idadi ya viti pasipo kusimama; kwa magari maalumu yenye nafasi kubwa kama mwendokasi, inapolazimika kusimama basi kila abairia avae Barakoa na kuachiana angalau umbali wa nusu mita.

error: Content is protected !!