LUSUBILO Mwakabibi, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke na Nyangi Msemakweli, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, wamesimamishwa kazi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Taarifa ya wakurugenzi hao kusimamishwa kazi imetolewa na Nteghenjwa Hosseah, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Taarifa hiyo imeeleza Ummy Mwalimu, Waziri wa Tamisemi, amewasimamisha kazi wakurugenzi hao kwa makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na ubadhirifu na usimamizi usioridhisha wa miradi ya maendeleo.
Taarifa hiyo imefafanua, kwamba uamuzi huo umefikiwa baada ya Tamisemi kupokea malalamiko na tuhuma kutoka mbalimbali za wananchi dhidi ya viongozi hao kuhusika na mwenendo wenye mashaka.
Na kwamba, Mwakabibi anatuhumiwa kuhusika na matumizi mabaya ya madaraka, ubadhirifu na usimamizi usiofaa wa miradi ya maendeleo.
Mwakibibi amewahi kuingia kwenye mgogoro na wanahabari kwa muda sasa kwa sababu ya kukataa kutoa taarifa mbalimbali anazoulizwa na siku chache zilizopita, aliamuru kukamatwa kwa waandishi wawili kwa madai waliingia kwenye mkutano wake na wafanyabiashara bila idhini yake.
Taarifa hiyo pia imeeleza, tuhuma zinazomkabili Msemakweli ni ubadhirifu, usimamizi mbovu wa miradi ya maendeleo na uhusiano usioridhisha kati yake na madiwani, Mkuu wa Wilaya na viongozi wengine wa Wilaya na wa Mkoa wa Rukwa.
Leave a comment