Sunday , 28 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa DED Katimba awafunda watendaji Msalala
Habari za Siasa

DED Katimba awafunda watendaji Msalala

Spread the love

WATENDAJI  wa Halmahauri ya Msalala, Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga wametakiwa kuwa waadilifu na kutenda haki kwa wananchi wote wanaowahudumia, ili kujenga imani na Serikali iliyopo madarakani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Shinyanga…(endelea).

Wito huo ulitolewa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Msalala, Khamis Katimba, akifungua semina ya kuwajengea uwezo watendaji hao ambapo alisema utumishi wenye weledi na ufanisi mkubwa utapunguza kero kwa wananchi.

Katimba aliwashauri watumishi hao kuwashauri vizuri viongozi waliopo katika maeneo yao ya kazi na kuwasimamia watumishi waliopo katika kata na vijiji vyao.

“Masuala haya yote yatawezekana iwapo watendaji mtakuwa mfano kwa watumishi wengine ikiwa ni pamoja na kufika ofisini kwa wakati na kutoka saa 9.30 alasiri, lakini pia kutumia lugha yenye staha kwa wateja wanaokuja kupata huduma katika ofisi zenu. Nakutana nanyi mara kwa mara lengo langu kubwa ni kuhakikisha mnaweza kujiendesha wenyewe na kuwaza nini utaifanyia halmashauri yako na nchi yako kwa ujumla,” alisema Katimba.

Alisema, halmashauri hiyo inatumia gharama kubwa ili kuhakikisha watumushi  wanasimama imara na kuwa nguzo muhimu ya utatuzi wa changamoto za wananchi.

“Simamieni mapato na kuhakikisha fedha za serikali zinakusanywa. Ndio maana watendaji wa kata wote nimewapa pikipiki. Fanyeni ziara za kushtukiza ndani ya vijiji ili kuongeza uwajibikaji kwa watumishi wengine, nami nitapita kuona hili kama linatekelezwa na pale nitapoona kuna uzembe, nitachukua hatua,” alisema Katimba.

Kwenye mafunzo hayo, miongoni mwa mada zilizowasilishwa ni majukumu ya mtendaji wa kata na kijiji, vikao vya kisheria vinavyopaswa kufanywa ngazi ya kijiji na kata, chimbuko la Mamlaka za Serikali za Mitaa na sababu za kuanzishwa kwake.

Pia dhana nzima ya utawala bora, ukusanyaji mapato na sababu za msingi za kisheria za kwa nini Mamlaka za Serikali za Mitaa zikusanye mapato, masuala ya TASAF na fursa zijazo kwa ajili ya machinga.

Mada hizo ziliwasilishwa na Mwanasheria wa Halmashauri hiyo, Leonard Mabula akishirikiana na Mkuu wa Idara ya Utawala na Usimazi wa Rasilimali Watu, Mary Nziku, ambaye amewataka watendaji hao kuthamini nafasi walizonazo na kuzitumikia kwa bidii ili kuleta tija ndani ya halmashauri hiyo.

Baadhi ya washiriki wamepongeza hatua ya halmashauri hiyo kukutana nao mara kwa mara katika jitihada za kuhakkikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi.

“Hongera sana kiongozi wetu (mkurugenzi) nasi hatutakuangusha,” alisema Patrick Mahona, Mtendaji wa Kata ya Segese, Msalala.

Neema Magwega, Mtendaji wa Kijiji cha Ntambalale ameishukuru halmashauri kwa kutoa mafunzo kwa mabaraza ya ardhi ya kata ili kukabiliana na migogoro ya ardhi.

Mafunzo hayo yaliyohusisha Watendaji wa Kata 18 na Watendaji wa Vijiji 92, yalitokana na maelekezo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa aliyeaguzi wakurugenzi wote kuwapa mafunzo mbalimbali watumishi ili kuwaongezea ujuzi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Biteko aipongeza GGML kudhibiti vifo, majeruhi mahali pa kazi

Spread the loveNAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

Habari za Siasa

Askofu Shoo awataka ACT kupigania maslahi ya Taifa, wasikubali kuhongwa

Spread the loveALIYEKUWA Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri, Askofu...

Habari za Siasa

Biteko aagiza waajiri kudhibiti vifo mahali pa kazi

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mavunde aibana kampuni kutimiza masharti ya mkataba

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameitaka Kampuni ya Xin Tai...

error: Content is protected !!