September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

COSTECH kumpiga jeki Kipanya, yalia wabunifu wengine kuingia mitini

Spread the love

TUME ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imeunga mkono ubunifu wa gari la umeme la Mwandishi wa habari na mchoraji vibonzo maarufu nchini, Masoud Kipanya kwa kumjengea mfumo wezeshi kwa ajili ya kutengeneza gari nyingi za aina hiyo. Anaripoti Faki Ubwa … (endelea)

Hayo yameelezwa leo tarehe 18, Aprili 2022, na Dk. Amos Nungu alipotembelea maegesho ya muda ya gari hiyo Ofisi za Clouds Media kwa ajili ya kuzungumza na Kipanya.

Dk. Nungu amesema ili aina ya gari kama iliyotengenezwa na Kipanya zitengenezwe kwa wingi nchini ni lazima kuwe na mfumo wezeshi kwa ajili ya kutengeneza gari hizo.

“Serikali kupitia Costech tumekuja kuangalia tunaweza kumsaidia nini hususani kupitia viwanda vilivyopo nchini ili kuwe na muendelezo kuwepo na gari nyingi za aina hii zinazozalishwa nchini kwa kutumia malighafi zinazozalishwa katika viwanda vya Tanzania.

“Kwa sababu katika gari hili la kwanza, Kipanga ametafuta vifaa vyote mwenyewe, lakinin ili aendelee kuzalisha magari mengi atahitaji vifaa vingi zaidi,” amesema.

Dk. Nungu amesema kuwa COSTECH si mara ya kwanza kuzungumza na Kipanya na kwamba mara hii imezungumza naye juu ya mfumo jumuishi wa utengenezaji wa gari kwa vifaa vyote vipatikane nchini kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali.

“Tumekuja kuzungumza naye vifaa gani anataka kuagiza vipi anataka kutengeneza kusudi tuone uwezekano wa taasisi zetu hapa nchini zinawezaje kushiriki kwenye kutoa vifaa vya gari hilo mfano Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kuna karakana ya magari, DIT na vyuo vyengivyo wanaweza kusema kwenye hii gari wao wanaweza kutengeneza kifaa fulani wapo wanaoweza kutengeneza taa za magari tu kwa kuwa tayari soko lipo Kipanya anataka vifaa” amesema Dk Nungu.

Amesema Tume hiyo inazungumza na Kipanya ili kujua kifaa gani kitakuwa kinahitajika kwenye matengenezo ili COSTECH kuwawezesha wabunifu wenye uwezo kwenye kutengeneza vifaa hivyo ili nchi ijitosheleze kwa vifaa.

Dk. Nungu ameeleza kuwa mfumo huo utakuwa na matokeo chanya na kwamba viwanda hivyo vitanyanyua uchumi wa nchi na kwamba mfumo wezeshi uwasaidia wabunifu wa ndani kwa ujumla.

Amesema kuwa Kipanya ametoa changamoto kwa wabunifu nchini ambapo Taasisi hiyo tangu mwaka 2018 imetoa takribani Shilingi 200 Milioni kwa ajili ya ubunifu lakini haukutoa matokeo chanya zaidi ya pesa hizo kuwanufaisha wabunifu hao.

Kipanya amekubaliana na wazo la COSTECH na kueleza kuwa wazo hilo litainyanyua nchi kiuchumi kutokana na kuokoa fedha nyingi kwenda nje kwa ajili ya kununua vifaa vya magari.

”Ukiitengeneza hivyo vitu hapa nchini umeanza kuvipa neema na ajira viwanda vyetu vya ndani mfano Kioo limited walikuwa wakitengeneza bidhaa nyingine za vioo tukizungumza nao na kuanza kututengenezea vioo tayari tumeongeza biashara na ule mnyororo wa thamani unaongezeka” amesema Kipanya.

Kipanya amesema endapo vifaa vyote vitanunuliwa nchini na gari hiyo vikauzwa kiasi chote cha fedha kitabaki ndani ya nchi.

Amesema kuwa COSTECH wamefanya muendelezo wa mazungumzo naye na kwamba nia ya Tume hiyo ni kuinua bunifu za ndani.

error: Content is protected !!