Thursday , 28 March 2024
Home Habari Mchanganyiko Simulizi kifo cha Padri Dar, Polisi wasema…
Habari Mchanganyiko

Simulizi kifo cha Padri Dar, Polisi wasema…

Spread the love

UTATA umeibuka juu ya kifo cha Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Yohanne Paul II, iliyoko Mbezi Mshikamano, jijini Dar es Salaam, Padri Francis Kangwa ambaye alifariki dunia tarehe 12 Aprili 2022. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Taarifa za kifo cha Padri Francis ambaye alikuwa kipenzi cha waumini wa Parokia yake, kilitangazwa kwa mara ya kwanza tarehe 15 Aprili 2022 na Paroko Msaidizi, Padri Louis Mtamati wakati wa Misa ya Ijumaa Kuu.

Tangazo hilo lililotolewa mwishoni mwa Ibada ya Ijumaa Kuu, liliibua vilio, simanzi na huzuni kwa waumini wa Kanisa hilo, huku wengine wakishindwa kuamini walichosikia.

Mwili wa Padri Francis ulikutwa kwenye tangi la maji nyuma ya nyumba ya mapadri wa Shirika la Missionaries of Africa (Atman House), Dar es Salaam na hadi sasa hakuna anayejua chanzo cha kifo hicho.

Taarifa ambazo MwanaHALISI Online ilizipata, zilieleza kuwa Padri Francis ambaye pia alikuwa Mkuu wa Missionaries of Africa nchini, hakuwa mgonjwa na muda wote alishiriki maandalizi ya sikukuu ya Pasaka katika Kanisa lake.

Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Missionaries of Afrika Jimbo la Afrika Mashariki na Kati, ilieleza kuwa Jumanne ya 12 Aprili 2022, Padri Francis aliegesha gari lake kwenye nyumba ya mapadri wa Shirika hilo, ya Atiman House eneo la Posta, Dar es Salaam na kuhudhuria Ibada ya kubariki mafuta ya Crism ndani ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa baadaye, Padri Francis alipata chakula cha mchana na mapadri wengine hapo hapo Atiman House.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, siku zilizofuata, Padri Francis hakuonekana na wala kupatikana kwenye simu yake ya mkononi, lakini gari lake liliendelea kubaki kwenye eneo la maegesho Atiman House.

“Baada ya hali hiyo, baadhi ya mapadri walihisi kuna jambo haliko sawa, hivyo wakamtafuta kwenye vyumba vya nyumba hiyo ya mapadri na kuulizia katika baadhi ya hospitali kama wana mgonjwa wa aina hiyo, lakini hawakufanikiwa,” ilisema taarifa hiyo na kuongeza:

“Lakini leo (Aprili 12), walivyokuwa wanajiandaa kutoa taarifa Polisi, mwili wake uligundulika ndani ya tangi la maji nyuma ya Atiman House.

Bado tunasubiri uchunguzi wa Polisi kuhusu chanzo cha kifo chake. Tunaweka familia yake na jumuiya nzima kwenye maombi ni wakati mgumu sana kwetu, lakini tunamwamini Mungu na acha mapenzi yake yatimizwe na Padri Francis, apumzike kwa amani,” ilihitimisha taarifa hiyo.

Askofu Ruwai’chi

Askofu Mkuu Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Yuda Thaddeus Ruwai’chi, alieleza katika taarifa yake, kwamba alipokea kwa masikitiko kifo cha Padri Francis na kuwapa pole waumini wa Kanisa Katoliki, familia na Shirika lake la Missionaries Of Africa.

Taarifa ya Askofu Ruwai’chi ilifuatiwa na taarifa zingine kutoka parokia mbalimbali nchini, zikieleza kusitishwa na kifo cha Padri huyo.

Kamanda Muliro

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alikiri Polisi kuwa na taarifa za kifo cha Padri huyo na inaendelea na uchunguzi.

Alisema hakuna sababu ya waumini wa Kanisa hilo na wengine kuhoji na kupeana taarifa zisizo sahihi juu ya kifo hicho, kwani ni cha kawaida.

“Kwa kifupi niseme tu, kwamba taarifa ya kifo cha Padri Francis tunazo ni kweli amekufa, ni kweli mwili wake umekutwa kwenye tangi la maji, lakini hatujui aliingia mwenyewe au aliingizwa na watu, hilo hatujui, uchunguzi ukikamilika tutatoa taarifa kamili, hivyo nawaomba wawe na subira,” alisema Kamanda Muliro.

Mazishi

Wakati Polisi wakiendelea na uchunguzi, maandalizi ya kuhifadhi mwili wa Padri huyo yanaendelea katika Parokia ya Mtakatifu Yohanne Paul II, Mbezi Mshikamano.

Mwenyekiti wa Parokia hiyo, Fortunatus Kapinga aliwatangazia waumini wa Kanisa hilo jana Jumapili, kuwa wanasubiri kibali cha Polisi na kukabidhiwa mwili kwa ajili ya maziko.

Alisema Askofu Ruwai’chi anatarajiwa kuongoza mazishi ya Padri huyo raia wa Zambia, lakini pia kutakuwa na wageni kutoka nchi mbalimbali ambazo Shirika hilo linatoa huduma ya kiroho.

Aliwataka waumini hao kuwa na imani, kwamba kifo cha Padri Francis ni cha kawaida, hivyo aliwataka kuwa watulivu na kuacha kusikia maneno ya kupotosha juu ya kifo hicho.

Padri Francis atakumbukwa na waumini wa Kanisa la Mtakatifu Yohanne Paul II kutokana na hamasa yake, kujitolea kuhakikisha ujenzi wa Kanisa hilo unakamilika.

Tangu alipoingia kwenye Parokia tarehe 18 Juni 2017, Padri Francis alifanikisha ujenzi wa Kanisa hilo la kisasa na hivi karibuni alianza ujenzi wa nyumba za mapadri, lakini pia ndiye aliyewezesha Kanisa hilo kuwa Parokia kamili.

2 Comments

  • Wivu uliokithiri!
    Badala ya kujifunza anavyofanya kazi kwa akili alizopewa na Mungu, watu mnamuonea wivu. Sasa unataka uendeshe Kanisa ukidhani uno uwezo wake…kumbe huna!
    Mungu mmulike aliyefanya haya kwa laana kali.

  • Hi, can you translate to English, even is you do it with a simple translator, the page is protected and I can’t translate. Thank you very much.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kapinga kuongoza usambazaji wa mitungi ya gesi 10,000 ya Taifa Gas

Spread the loveNaibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ameahidi kuongoza kwa ufanisi...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Wafanyabiashara, wawekezaji China waridhia kuwekeza bil. 800 katika sekta 5 nchini

Spread the loveUJUMBE wa wafanyabiashara na wawekezaji wakubwa kutoka Jimbo la Changzhou...

Habari Mchanganyiko

Bil. 4.42 kumaliza uhaba maji kata 2 Musoma Vijijini

Spread the loveWANANCHI wa kata za Busambara na Kiriba, Jimbo la Musoma...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Soko nepi za watoto lashuka, watu wazima lapaa

Spread the loveKiwanda cha kutengeneza nepi cha Japan kimetangaza kuwa kitaacha kutengeneza...

error: Content is protected !!