October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Chadema wamtega Msajili wa vyama

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi

Spread the love

 

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema hakitashiriki vikao vya majadiliano ya wadau wa vyama vya siasa, vilivyoitishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, hadi mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, atakapoachwa huru bila masharti yoyote. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Sharti hilo limetajwa leo Jumatatu, tarehe 11 Oktoba 2021 na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Benson Kigaila, akitoa maazimio ya kikao cha kamati kuu ya chama hicho, kilichofanyika jana Jumapili, kwa njia za kidigitali.

“Sisi kama Chadema hatuwezi kwenda kwenye vikao vya msajili, mpaka mwenyekiti wetu aachiwe bila masharti yoyote. Sababu Watanzania, Serikali na dunia inajua kwamba Mbowe sio gaidi amebambikiziwa kesi kwa lengo la kumtesa,” amesema Kigaila.

Benson Kigaila, Naibu Katibu Mkuu Chadema Bara

Kigaila amesema, Chadema hakiwezi kushiriki kikao hicho wakati mwenyekiti wake yuko ndani.

“Hatuwezi kwenda kwenye kikao kujadiliana chochote wakati kiongozi wetu yuko ndani, tunataka Serikali ifute mashtaka ya kubumba waliyomtengenezea mwenyekiti wetu atoke, aachwe huru ili kama kuna vikao vya kwenda twende naye,” amesema Kigaila.

Msimamo huo umetolewa katika kipindi ambacho Jaji Mutungi ameitisha kikao cha wadau wa vyama vya siasa, ikiwemo Inspekta wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro, ili kutafuta suluhu ya changamoto zinazokabili tasnia hiyo.

Kikao cha wadau wa vyama vya siasa nchini, kinatarajiwa kufanyika jijini Dodoma, tarehe 21 Oktoba 2021.

error: Content is protected !!