May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CCM yaanza safari kumpata mrithi wa Magufuli

Spread the love

 

SAFARI ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kumpata mwenyekiti mpya wa chama hicho, imeanza rasmi jijini Dodoma. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Mwenyekiti huyo, atapatikana katika mkutano mkuu maalum, utafanyika Ijumaa hii ya tarehe 30 Aprili 2021, ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma, ikiwa ni saa 48 zimesaliwa, kuifikia siku hiyo.

Ni baada ya aliyekuwa mwenyekiti wake, Dk. John Pombe Magufuli, kufariki dunia tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, Makumbusho mkoani Dar es Salaam.

Mara baada ya kifo hicho, Samia Suluhu Hassan, aliyekuwa makamu wa Rais, aliapishwa, Ikulu ya Dar es Salaam na Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma kuwa Rais tarehe 19 Machi 2021

Maandalizi ya mkutano huo maalum, yamekwisha kuanzia ikiwemo, kuwasili kwa wajumbe hususan wa kamati kuu ambao leo Jumatano, wamekutana katika ukumbi wa Jakaya Kikwete kisha utafanyika mkutano wa halmashauri kuu na baadaye mkutano mkuu maalum.

Kikao hicho, kimeongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip Mangula.

Rais Samia, anapigiwa chapuo na vigogo wa chama hicho, akiwemo mwenyekiti mstaafu wa CCM, Jakaya Mrisho Kikwete na aliyewahi kuwa waziri mkuu, Cleopa Msuya.

Vigogo hao wanasema, Rais Samia anao uwezo wa kukiongoza chama hicho, kwani anakifahamu na amekuwa mshiriki mzuri wa vikao vya CCM kwa kipindi kirefu.

Kauli za vigogo hao, zinatolewa kipindi ambacho kumekuwa na minong’ono ya chini kwa chini kwamba, nafasi ya uenyekiti, itenganishwe na ya Rais. Sababu hasa bado haijajulikana.

Hata hivyo, kwa nyakati tofauti, Rais Samia mwenyewe, amekuwa akisema amepikwa vyema na watangulizi wake, kama Kikwete, Rais mstaafu wa Zanzibar, Aman Abeid Karume na Hayati Magufuli.

Hivi karibuni, akihutubia Bunge jijini Dodoma kwa mara ya kwanza, Rais Samia alitumia fursa hiyo kuwaondoa hofu akisema, Mwenyezi Mungu hakuumba ubongo hafifu kwa mwanamke na ubongo wenye uwezo mkubwa kwa mwanaume.

Rais Samia alisema, makuzi na umakini wa akili hutegemea jamii inayokuzunguka na shughuli unazokuwa nazo.

“Nataka nikuhakikishieni, nimekuzwa kwenye jamii sahihi na kwamba nina uzoefu wa kutosha kwenye Serikali na kwenye Chama changu cha Siasa CCM,” alisema Rais Samia

Ikiwa wajumbe wa mkutano mkuu maalum huo, watampitisha Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mwenyekiti wa chama hicho, wataendeleza utamaduni wa Rais aliyepo madarakani kuwa na kofia mbili ya urais na uenyekiti.

CCM

Wengine waliomtangulia ni; Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mzee Ali Hassan Mwinyi, Hayati Benjamin Willium Mkapa, Jakaya Mrisho Kikwete na Hayati John Pombe Magufuli.

Rais Samia ikiwa atapewa kofia hiyo ya pili ya mwenyekiti, atakuwa na jukumu la kumpata mtendaji wake mkuu yaani katibuy mkuu, ndani ya chama.

Nafasi ya katibu mkuu, imekuwa wazi tangu tarehe 26 Februari 2021, baada ya aliyekuwa katibu mkuu, Dk. Bashiru Ally kuteuliwa na Hayati Magufuli kuwa katibu mkuu kiongozi.

Kwa sasa, nafasi hiyo ya katibu mkuu, inakaimiwa na Dk. Rodrick Mpogolo ambaye ni naibu katibu mkuu wa CCM-Bara.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI TV, MwanaHALISI Online na mitandao yetu ya kijamii kwa kwa habari na taarifa mbalimbali

error: Content is protected !!