MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) nchini Tanzania, Charles Kichere amebaini ufanisi duni kwenye mchakato wa utoaji leseni kwa waendeshaji wa michezo ya kubahatisha hali inayoweza kuwa hatari kwa wateja wao. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Kichere amebaini hayo kupitia ripoti zake za mwaka 2020/21 alizozifanya akisema, ukaguzi alioufanya kwa mashirika ya udhibiti yenye mamlaka ya kutoa leseni ulibaini mapungufu kadhaa yakiwamo Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT) kutoa leseni kwa waendeshaji 60 wa michezo hiyo bila ya amana ya kutosha.
Anasema, amana ni kama dhamana ya usalama na ulinzi kwa ajili ya kuwalinda wateja wa michezo hiyo.
Kichere anasema, amana hiyo inaweza kutumika inapotokea waliopewa leseni za uendeshaji wa michezo hiyo wameshindwa kulipa madeni ya wateja wao kama inavyotakiwa na Kifungu cha 18A cha Sheria ya Michezo ya Kubahatisha [kama ilivyorekebishwa mwaka 2019].
“Kwa kutowasilisha dhamana, bodi haiwezi kuwalinda wadau wa michezo ya kubahatisha iwapo waendeshaji wa michezo hiyo wataingia kwenye madeni na wateja wao,” anasema Kichere kwenye ripoti ya Mashirika ya Umma na kuongeza:
“Ninapendekeza Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania ihakikishe waendeshaji wa michezo ya kubahatisha wana kiwango cha dhamana cha kutosha ili kulinda wateja iwapo mwenye leseni atashindwa kulipa madeni ya michezo ya kubahatisha.”
Leave a comment