WAZIRI Mkuu wa zamani wa Japan Shinzo Abe (67) amefariki dunia, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya kimataifa. Anaripoti Mwandishi Wetu kwa msaada wa mashirika ya habari ya kimataifa…(endelea).
Abe ambaye anasalia kuwa waziri mkuu aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi nchini Japan, alipigwa risasi alipokuwa akitoa hotuba ya mkutano mmoja wa kampeni.
Mshukiwa wa shambulizi hilo aliripotiwa kuwa mwanamume mwenye umri wa miaka 40 na alikamatwa katika eneo la tukio.
Abe alipigwa risasi mara mbili alipokuwa akitoa hotuba katika mji wa kusini wa Nara asubuhi ya leo Ijumaa tarehe 8 Julai 2022.
Mara moja alianguka na kukimbizwa katika hospitali ya karibu. Picha zilizopigwa eneo la tukio zilimuonyesha akivuja damu.
Shirika la Kudhibiti Moto na Majanga lilithibitisha kuwa Abe alikuwa na jeraha la risasi upande wa kulia wa shingo yake, na pia alitokwa na damu chini ya ngozi chini ya sehemu ya kushoto ya kifua chake.
Haijulikani ikiwa risasi zote mbili zilimpata, au ikiwa risasi ilimpata shingoni na kutokea kwingine.
Shirika la utangazaji la taifa NHK lilisema kuwa Abe alikuwa “na fahamu ” alipokuwa akisafirishwa hadi hospitalini, likinukuu vyanzo vya polisi.
Lakini pia ilimnukuu mwanachama mkuu wa chama cha Abe akisema hali ya kiongozi huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 67 ni ya “kusumbua” na kwamba alikuwa akiongezewa damu.
Aliyekuwa gavana wa Tokyo Yoichi Masuzoe alikuwa amesema hapo awali kwenye ujumbe wa Twitter kwamba Abe alikuwa katika hali ya mshtuko wa moyo. Neno hilo mara nyingi hutumika kabla ya kifo kuthibitishwa rasmi nchini Japani.
Abe, ambaye alikuwa waziri mkuu aliyekaa muda mrefu zaidi madarakani nchini Japan, alijiuzulu mwaka 2020 akitoa sababu za kiafya. Baadaye alifichua kwamba alikuwa ameugua tena ugonjwa wa vidonda vya tumbo.
Alirithiwa na mshirika wake wa karibu Yoshihide Suga, ambaye baadaye nafasi yake ilichukuliwa na Fumio Kishida.
Matukio ya mashambulio ya bunduki ni nadra sana nchini Japani, ambapo bunduki zimepigwa marufuku – na matukio ya vurugu za kisiasa sio jambo la kawaida .
Katika mwaka 2014, kulikuwa na matukio sita tu ya vifo vya bunduki nchini Japani, ikilinganishwa na 33,599 nchini Marekani. Watu wanapaswa kufanyiwa uchunguzi mkali na vipimo vya afya ya akili ili kununua bunduki – na hata hivyo, ni aina fulani ya zinazoruhusiwa.
Leave a comment