MWANAHARAKATI huru, Bihimba Mpaya, amewataka wanaharakati kujikita zaidi katika kuisaidia jamii na kuwataka baadhi yao ambao wanatumia majukwaa yao vibaya kuacha mara moja. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Bihimba alitoa wito huo jana tarehe 26 Machi 2024, wakati akitoa msaada wa kiasi cha Sh. 200,000 kwa vikundi vya wajasiriamali wadogo wadogo Tanzania (SHIVUTA) na Umoja wa Vikundi vya Ujasiriamali Kivule (UVUKI), katika hafla ya harambee ya kutafuta fedha za kununua mabasi ya kusafirisha abiria (kosta) tano.
Amedai wapo baadhi ya wanaharakati wanatumia majukwaa yao vibaya kutoa lugha za uchochezi na kusahau majukumu yao ya kuisaidia jamii.
“Kuna uanaharakati wa aina nyingi, kuna wengine wanaharakati wa kufokafoka lakini mimi ninasaidia jamii. Uanaharakati huu nimejifunza kwa Martin Luther King, alikuwa anafanya harakati za kuisaidia jamii,” alisema Bihimba.
Bihimba alisema mara kwa mara amekuwa akitumia fedha zake anazopata kupitia kampuni yake ya usafirishaji ya Bihimba Tudo Transport, kuisaidia jamii kwa kuwa anatambua umuhimu wa kusaidia makundi ya watu wenye uhitaji.
Mwanaharakati huyo amekuwa akitoa msaada kwa wananchi wenye uhitaji hususan wa Jimbo la Ukonga, ambapo ameshawahi kuchangia ujenzi wa baadhi ya shule za sekondari za umma, misikiti na madrasa. Pamoja na kusaidia watu wenye mahitaji maalum kama walemavu na wajane.
Leave a comment