May 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Biashara United yaanza mwaka kwa Tuzo

Spread the love

 

MSHAMBULIAJI wa Biashara United ya Mara, Deogratius Mafie amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Januari wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania (VPL) msimu wa 2020/21, huku Francis Baraza pia wa Biashara United akichaguliwa Kocha Bora wa mwezi huo. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).

Mafie na Baraza walitwaa tuzo hizo, baada ya kuwashinda wenzao walioingia nao fainali kwa mwezi Januari katika uchambuzi uliofanywa wiki hii na Kamati ya Tuzo za VPL, kutokana na mapendekezo ya makocha waliopo vituo mbalimbali ambavyo ligi hiyo inachezwa.

Mafie aliwashinda kiungo wa Ruvu Shooting, Mohammed Issa na mshambuliaji wa Mwadui FC, Wallace Kiango, huku Baraza akiwashinda Charles Mkwassa wa Ruvu Shooting na Abdallah Mohammed wa JKT Tanzania.

Wachezaji wengine ambao tayari wameshatwaa tuzo hiyo ya mwezi kwa msimu huu na miezi yao katika mabano ni Prince Dube wa Azam (Septemba), Mukoko Tonombe wa Yanga (Oktoba), John Bocco wa Simba (Novemba) na Saidi Ntibazonkiza wa Yanga (Desemba).

Makocha waliotwaa tuzo hiyo ni Aristica Cioaba aliyekuwa Azam (Septemba), Cedric Kaze wa Yanga (Oktoba), Charles Mkwassa wa Ruvu Shooting (Novemba) na Cedrick Kaze  wa Yanga (Desemba).

TFF na Bodi ya Ligi zimekuwa na utaratibu wa kutoa Tuzo ya Mchezaji Bora na Kocha Bora wa VPL kila mwezi, ambapo pia mwisho wa msimu kunakuwa na tuzo za wachezaji mbalimbali waliofanya vizuri kwa msimu mzima, ikiwemo Tuzo ya Mchezaji Bora wa msimu.

error: Content is protected !!