Saturday , 27 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Benki ya Exim yapiga kambi Lindi, Mtwara kuimarisha sekta ya elimu, kilimo
Habari Mchanganyiko

Benki ya Exim yapiga kambi Lindi, Mtwara kuimarisha sekta ya elimu, kilimo

Spread the love

BENKI ya Exim Tanzania imeelezea adhma yake ya kukuza na kuchochea ukuaji wa kiuchumi katika mikoa ya Lindi na Mtwara kwa kukuunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali katika kukuza sekta ya kilimo, biashara na elimu katika mikoa hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu… (endelea).

Katika kuthibitisha adhma yake hiyo, viongozi waandamizi wa benki hiyo wakiwemo Mkuu wa Huduma ya Rejareja wa benki hiyo, Andrew Lyimo pamoja na Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo Stanley Kafu mwishoni mwa wiki walitoa msaada wa madawati 200 katika mikoa hiyo sambamba na kuandaa hafla ya chakula cha jioni kwa ajili ya wateja wa benki hiyo Mkoani Mtwara.

Mbunge wa Mchinga, mkoani Lindi, Mama Salma Kikwete (kushoto) akipokea msaada wa madawati 100 kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano kutoka Benki ya Exim, Stanley Kafu (kulia) kwa ajili ya kusaidia kuondoa adha ya upungufu wa mawadati katika shule mbalimbali za jimboni kwake ikiwa ni sehemu ya mpango wa benki hiyo wa ugawaji wa madawati 1000 katika mikoa mbalimbali nchini kupitia mpango wake wa kusaidia jamii ujulikanao kama Exim Cares. Wanaoshuhudia ni pamoja na Mkuu wa Huduma ya Rejareja wa benki hiyo, Andrew Lyimo (wa tatu kulia)na maofisa wengine kutoka serikalini na benki hiyo.

Hatua hiyo ilitoa fursa kwa benki hiyo kuelezea huduma zake mpya, fursa za biashara pamoja na mkakati wake katika kukuza sekta za elimu pamoja na kilimo husasani kupitia zao la korosho.

Akizungumza kuhusu matukio hayo, Lyimo alisema yameweza kutoa fursa kwao kukutana na wateja wao, viongozi waandamizi wa serikali na wadau wengine muhimu mkoani humo hivyo kutoa wasaa kwao wa kutambulisha huduma mpya sambamba na kupokea mrejesho kuhusu mahitaji ya wateja wao hususani kipindi hiki ambacho mikoa hiyo ipo kwenye mkakati wa kuboresha zaidi sekta ya kilimo na bandari ya Mtwara.

“Mikoa ya Mtwara na Lindi ni miongoni mwa mikoa muhimu sana kwetu kibiashara na hiyo ndio sababu mikoa hii ilikuwa ni miongoni mwa mikoa ya awali kabisa kufungua matawi yetu. Katika kipindi chote cha uwepo wetu katika mikoa hii tumekuwa na mchango mkubwa kwa wakazi wa mikoa hii kwa kutoa huduma zinazowalenga haswa ikiwemo mikopo ya kilimo, biashara, mikopo ya watumishi na sasa tumekuja na huduma mahususi kwa ajili ya wajasirimali,’’ alisema.

Zaidi alisema hali ya uchumi katika mikoa hiyo kupitia uboreshwaji wa bandari ya Mtwara inazidi kutoa fursa kubwa kwa benki hiyo kuhudumia wateja wengi zaidi wakiwemo wafanyabiashara wakubwa na wa kati kutoka ndani na nje ya nchi ambao wanatumia bandari hiyo.

Mbunge wa jimbo la Mchinga, mkoani Lindi, Mama Salma Kikwete (kushoto) akitoa neno la shukrani kwa viongozi waandamizi wa benki ya Exim akiwemo Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano kutoka Benki ya Exim, Stanley Kafu (katikati walioketi), Mkuu wa Huduma ya Rejareja wa benki hiyo, Andrew Lyimo (wa pili kulia walioketi) wakati wakati wa makabidhiano ya madawati 100 yaliyotolewa na benki ya Exim Tanzania.

“Uwepo wa benki ya Exim katika visiwa vya Comoro unatoa fursa kwa wafanyabiashara wa pande hizi mbili kufanya biashara kwa urahisi zaidi kwa kuwa Exim tunawahakikishia huduma za uhakika za kifedha ikiwemo mikopo,’’ alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo Stanley Kafu alisema mchango wa benki hiyo katika mikoa hiyo haujaishia katika utoaji wa huduma za kifedha tu bali pia imekuwa mdau muhimu wa maendeleo ya kupitia mpango wake wa uwajibikaji kwa jamii ujulikanao kama Exim Cares

“Serikali kupitia viongozi mbalimbali wanafanya jitihada kubwa kuboresha sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya na kilimo hivyo ni jukumu letu sisi kama taasisi za kifedha kuunga mkono jitihada hizo za serikali. Kupitia mkakati huu uliozinduliwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mwishoni mwa mwaka jana tumeweza kutoa msaada wa madawati katika mikoa mbalimbali hadi sasa ikiwemo mikoa ya Dodoma, Mbeya, Mwanza, Shinyanga, Tabora, Lindi na Mtwara na bado tunaendelea mikoa mingine zaidi.’’ alisema Kafu.

Akizungumzia hatua hiyo Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Brigedia Jenerali Marco Gaguti aliipongeza benki ya Exim kwa msaada wa madawati katika mkoa wake huku akibainisha kuwa msaada huo utasaidia katika kukabiliana na upungufu wa madawati katika baadhi ya shule zilizopo mkoani humo.

Wafanyakazi wa Benki ya Exim wakiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wanafunzi watakaonufaika na msaada wa madawati 100 yaliyotolewa na benki hiyo kwa ajili ya jimbo la Mchinga .

“Msaada huu umekuwa na tija kubwa kwenye mkoa wetu kwa kuwa tuna uhitaji wa madawati kutokana na muitikio mkubwa wa agizo la Mheshimiwa Rais la ujenzi wa madarasa. Tuna miradi mingi ya ujenzi wa madarasa ambayo inakwenda sambamba na hitaji la madawati hivyo tunawapongeza sana wenzetu wa Exim kwa kutuunga mkono kwenye hili,’’ alisema.

Kuhusu ukuaji wa biashara, Brigedia Jenerali Gaguti alisema uboreshwaji wa bandari ya Mtwara unaoshuhudiwa hivi sasa imekuwa ni kivutio kikubwa cha wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi ikiwemo visiwa vya Comoros, hivyo wananchi wa mkoa huo wanahitaji huduma bora za kifedha ili waweze kushiriki kikamilifu kutumia fursa za kibiashara zitokanazo na uwepo wa bandari hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Brigedia Jenerali Marco Gaguti akizungumza na wateja wa benki ya Exim mkoa wa mkoa huo wakati wa hafla ya chakula maalum kwa ajili ya wateja wa benki hiyo mkoani humo

“Ndio maana nimeguswa sana kusikia kwamba benki ya Exim tayari imeshaanza kujitanua zaidi nje ya mipaka ya nchi. Tafsiri yake ni kwamba wafanyabiashara wetu na wale wanaotoka nje ya nchi ikiwemo visiwa vya Comoros tayari wanaunganishwa na huduma za benki ya Exim…hongereni sana.Ni matumaini yangu kwamba wafanyabiashara mkoani Mtwara watachangamkia zaidi huduma za Exim ili waweze kunufaika na huduma za benki hii wanapofanya biashara kimataifa,’’ alisema.

Akizungumzia msaada wa madawati 100 aliyoyapata kwenye jimbo lake, Mbunge wa jimbo la Mchinga, mkoani Lindi, Mama Salma Kikwete pamoja na kuishukuru benki hiyo kwa msaada huo alisema kwa kushirikiana na viongozi wenzake atahakikisha madawati hayo yanakabidhiwa katika Shule zenye uhaba na kutunzwa vyema kwa lengo la kuleta tija iliyokusudiwa hususani kukabiliana na uhaba uliopo unaotokana na mwitikio wa wazazi kupeleka watoto shule kufuatia  sera ya elimu bila malipo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Wakili: Ukimpa zawadi mwenza marufuku kumpora hata mkiachana

Spread the love  WANANDOA na watu waliko kwenye mahusiano ya kimapenzi, wamekumbushwa...

Habari Mchanganyiko

Majaliwa: Mvua zimesababisha vifo vya watu 155, kuendelea hadi Mei

Spread the love  WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mvua kubwa za El-Nino...

Habari Mchanganyiko

Exim Bank yatoa  vitanda kwa shule ya Jeshi la Polisi Moshi

Spread the love  BENKI ya Exim imekabidhii  seti ya vitanda kwa Shule...

Habari Mchanganyiko

NBC yakabidhi vitanda Shule ya Polisi Moshi

Spread the loveBenki ya NBC imekabidhi msaada wa vitanda 28 kwa Shule...

error: Content is protected !!