August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia: Dodoma ni makao makuu, hakuna kurudi nyuma

Rais Samia Suluhu Hassan

Spread the love

 

RAIS Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa Serikali imedhamiria kwa dhati kuendeleza maono ya shujaa Hayati Mwalimu Julius Nyerere kwamba makao makuu ya Taifa ni Dodoma na hakuna kurudi nyuma.

Pia ameiagiza Ofisi ya Waziri Mkuu na mkoa Dodoma, kutafuta eneo lingine kwa ajili ya ujenzi wa mnara wa mashujaa kwa gharama nafuu kwa kuwa eneo mnara ulipo sasa ni katikati ya jiji ambalo linaendelea kukua. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo tarehe 25 Julai, 2022 katika maadhimisho ya sikukuu ya mashujaa ambayo licha ya kuadhimishwa katika mikoa mbalimbali nchini lakini kitaifa yamefanyika jijini Dodoma.

Amesema mashujaa walipambana katika nyanja mbalimbali dhidi ya ukoloni, udhalimu, ubeberu, ukandamizaji na uchokozi. Walipambana kifikra na kwa vitendo.

“Kati ya vita walivyopigana ni pamoja na vita vya majimaji, vita vya pili vya dunia ambavyo uwepo wa mzee wetu wa Mwenyekiti wa Tanzania legion miongoni mwetu ni ushahidi wa kipekee kuwa mashujaa hawa bado wapo.

“Pia walipambana kwenye Mapinduzi ya Zanzibar, vita vya ukombozi wa Afrika hasa kusini mwa Afrika, vita vya Kagera na operesheni mbalimbali ndani na nje ya Afrika.

“Tunawakumbuka na kuwaenzi mashujaa wetu hawa waliojitoa muhanga wakitetea uhuru na uhai wetu pamoja na heshima ya Taifa na Bara la Taifa, maadhimisho haya sio kwa waliopoteza roho zao tu, pia waliopata ulemavu wa maisha na waliotoa michango ya aina mbalimbali kwa njia moja au nyingine,” amesema.

Amesema Watanzania hawawezi kusahau mchango mkubwa wa uhai, hali na mali uliotolewa na mashujaa hao ndio maana wanakutana siku kama ya leo kila mwaka kuadhimisha na kuwakumbuka mashujaa wetu.

Amesema kwa miaka ya hivi karibuni hawakuweza kukutana kutokana na janga la uviko 19 lakini leo Mungu amewajaalia kukutana na wataendelea kukutana siku zijazo.

“Leo pia tunawakumbuka viongozi wetu ambao pia ni mashujaa walioasisi na Taifa letu la Tanzania na ambao wameshatanguliwa mbele ya haki hususani Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, Hayati Shekh Amani Abeid Karume pamoja na wengine walioshirikiana nao au waliokuja baada yao kuendeleza yale waliyoyaanzisha,” amesema.

Amesema mchango wao huo mkubwa ndio unaoifanya Tanzania kuendelea kuwa nchi yenye amani na kufuata misingi ya haki na utawala bora, misingi waliyoiacha inaifanya Tanzania kutambulika na kujijengea heshima mbele ya mataifa mbalimbai duniani kote.

Amesema kwa kutambua kazi kubwa iliyofanywa na mashujaa hao hatuna budi kuendelea kuenzi tunu za Taifa kwa kudumisha amani, upendo, umoja na mshikamano wetu.

“Maadhimisho haya yanafanyika jijini Dodoma, makao makuu ya nchi kwenye viwanja ambavyo mwaka 2016 Hayati Dk. Magufuli alitangaza rasmi uamuzi wa kishujaa wa kuhamia Dodoma.

“Napenda kusisitiza tena kwamba serikali imedhamiria kwa dhati kuendeleza uamuzi ule kama njia mojawapo ya kuenzi maono ya shujaa wetu Hayati Mwalimu Julius Nyerere, katika hili nirudie wito wa Dk. Magufuli, kwamba makao makuu ya Taifa hili la Tanzania nchi ni hapa Dodoma hakuna kurudi nyuma,” Rais Samia.

Mashujaa

Amesema jitihada za kujenga jiji la makao makuu ya Taifa zimeendelezwa na mpaka sasa ujenzi wa awamu ya pili wa kiserikali Mtumba au Magufuli city unaohusisha majengo ya kudumu, yatakayotosheleza watumishi wote unaendelea.

Amesema miondombinu ya barabara zinazonguka jiji la Dodoma inaendelea kujengwa, miradi ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimatafa pale Msalato, maji safi na salam pamoja na maji taka, umeme, mawasiliano na Tehama inaendelea ili kukuza hadhi ya jiji hili.

Aidha, amesema Serikali imekuwa ikihakikisha kunakuwa na mazingira bora kwa kupanda miti na kuweka mkoa wa Dodoma kuwa safi, sote ni mashahidi Dodoma ya miaka minane, tisa nyuma sio Dodoma iliyopo leo.

“Ushujaa sio kupambana katika vita au kuchangia kwa hali na mali wakati huo bali hata kuikweka nchi katika hali salama kwa kuhakikisha kunakuwa na uhakika wa usalama wa chakula, maji safi na salama, huduma bora za afya, elimu inayoondoa ujinga na kumuwezesha mtu kujikimu.

“Uwepo wa umeme wa kutosha kwa ajili ya kujenga uchumi na kuchangia usalama wa wananchi, huu nao pia ni ushujaa na katika hili watanzania wote ni mashujaa kwani kwa pamoja tunafanya kazi kuhakikisha mambo haya yanapatikana,” amesema.

Pamoja na mambo mengine amewakumbusha Wtanzania kuendelea kuchanja ili kujikinga na UVIKO 19 pia tarehe 23 Agosti mwaka huu ambayo ni siku ya sensa ya watu na makazi, watanzania wote washiriki kujiandikisha na kuhesabiwa.

error: Content is protected !!