GHARAMA za vifurushi zinazotolewa na kampuni za simu nchini Tanzania, zimepanda kuanzia leo Ijumaa tarehe 2 Aprili 2021. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Ni matokeo ya matumizi ya kanuni ndogo za gharama na tozo za vifurushi, utangazaji wa huduma maalum, zilizoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano ya Tanzania (TCRA).
Kutokana na bei hizo na mjadala unaoendelea mitandaoni na maeneo mbalimbali, wananchi wamemwomba Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kuingilia kati “ili kupunguza makali yatakayotokana na bei hizo.”
Matumizi ya kanuni hizo, ni baada ya maoni ya wateja yaliyojikita katika kulalamikia huduma hiyo, sambamba na kutoelewa namna vifurushi hivyo vinavyoisha.

Mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam, Frank Andrew anasema “Tulitarajia vifurushi vitashuka lakini kinachoshangaza vimepanda na ukizingatia matumizi ya intaneti ni muhimu.”
“Tunaiomba Serikali hasa Rais wetu, Mama Samia aliangalie hili na kutusaidia sisi wanyonge kwani litaturudisha nyuma sana. Ni bora wangeacha kama ilivyokuwa tu awali,” amesema
Mwingine Mariam Abdallah, Mkazi wa Mwenge anasema “mimi mwanzo nilikuwa nikijiunga kifurushi cha Sh.500 kwa siku, mtandao wa Airtel, nilikuwa napata dakika 60, MB200 lakini sasa napata dakika 40 na MB 100. Hii bei ni kali sana na inaumiza.”
Mariam amesema, “hapa serikali inapaswa kuangalia, hizi bei ni kutupunguzia makali au kutuongezea mzigo? Na hili nasikia ni mitandao yote, na tulisikia waziri anasema tutapunguziwa ndiyo huku kweli.”
Kwa upande wake, Albert Masanja, mkazi wa jijini Mwanza, aliyepiga simu kuzungumza na MwanaHALISI Online amesema, yeye anatumia mtandao wa Tigo, ambapo Januari 2021, alikuwa anajiunga kifurushi cha mwezi cha Sh.20,000.

Amesema, alikuwa anapata dakika 1500, GB 9 na sms 500 na ilipofika Februari 2021, mabadiliko yakafanyika ambapo Sh.20,000 ikawa dakika 1500, GB 5 na sms 500.
Masanja amesema, kwa mabadiliko ya sasa, Sh.20,000 “napata dakika 900, GB 4 na sms 200. Sasa hii ni kuumizana huku. Kweli kwa maisha ya sasa unapunguza bando kiasi hiki si ni kuongeza gharama za maisha.”
“Kwa kuwa Rais wetu Samia, ameanza vizuri, tuliona TRA inavyowasumbua wafanyabiashara na jana tumemsikia ametoa maagizo wasinyanyaswe, sasa aangalie na huku ambako tumewekewa mzigo mzito wa maisha sasa,” amesema Masanja
Tarehe 2 Machi 2021, James Kilaba, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, akizungumzia mabadiliko hayo, alisema zitaanza kutumika tarehe 2 Aprili 2021, ambayo ni leo.
Miongoni mwa yaliyomo katika kanuni hizo ni pamoja na huduma zote za vifurushi, lazima zipate vibali vya TCRA na vitadumu kwa siku 90, kabla ya kufanyika kwa mabadiliko mengine.
Hii ina maana kuwa, kwa bei za vifurushi vilivyoanza kutumia leo Ijumaa, vitadumu kwa siku 90, sawa na miezi mitatu kwa mujibu wa kanuni hizo.
Pia, kanuni hizo zinaelekeza, mtoa huduma atatakiwa kutoa taarifa pale matumizi ya kifurushi husika yatakapofika asilimia 75, na pale kifurushi kitakapokwisha.
Itakumbukwa, Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Dk. Faustine Ndugulile aliwahi kueleza, kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara ya vifurushi, TCRA inaandaa kanuni ambazo zotawabana watoa huduma.
Dk. Ndugulile alisema, kutakuwa na mabadiliko katika vifurushi hivyo, ingawa hakueleza mabadiliko hayo ni kushuka au kupanda kama ilivyojitokeza.
Leave a comment