Sunday , 19 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Barabara ya Kidatu- Ifakara kukamilika Mei, 2023
Habari Mchanganyiko

Barabara ya Kidatu- Ifakara kukamilika Mei, 2023

Spread the love

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amemtaka Mkandarasi Reynolds Construction Company Nigeria ltd, anayejenga kwa kiwango cha lami barabara ya Kidatu-Ifakara yenye urefu wa Kilomita 66.9 pamoja na daraja la Ruaha Mkuu lenye urefu wa mita 130, kuhakikisha ujenzi huo unakamilika mwezi Mei mwakani.

Amesema changamoto zote zilizokuwa zikichelewesha mradi huo zimepatiwa ufumbuzi hivyo kazi iliyobaki ni kwa Mkandarasi kukamilisha ujenzi. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi huo Mhandisi Kasekenya amesema barabara hiyo itakuza kilimo katika mkoa wa Morogoro na ukanda wa kusini mwa Tanzania, kupunguza muda wa usafiri na gharama za kusafirisha mazao na pembejeo za kilimo, kuongeza thamani ya mazao na hivyo kukuza uchumi wa wananchi kwa ujumla.

Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Morogoro, Mhandisi Lazack Kyamba akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya alipokagua ujenzi wa barabara ya Kidatu-Ifakara KM 66.9 ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami unaendelea mkoani Morogoro.

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha tunaufungua mkoa wa Morogoro ambao ni ghala la chakula ili kuunganisha kwa njia fupi na mikoa ya Njombe na Ruvuma,” amesema Naibu Waziri huyo.

Amemtaka msimamizi wa mradi huo, Kitengo cha Uhandisi Ushauri cha TANROADS (TECU), kuhakikisha maeneo yote yanayohitaji kuboreshwa ili kuimarisha usalama katika barabara hiyo yanafanyiwa kazi haraka na kwa viwango.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro Eng. Lazack Kyamba amesema mradi huo ambao umefikia asilimia 68 uko katika hatua nzuri na watamsimamia mkandarasi ili ukamilike kama ilivyopangwa.

Barabara ya Kidatu-Ifakara KM 66.9 ni sehemu ya barabara ya Mikumi-Ifakara yenye urefu wa KM 130 inayopita katika ukanda wenye uzalishaji mkubwa wa mazao hivyo kukamilika kwake kutaboresha ustawi wa jamii kwa kukuza uchumi wa watu na taifa kwa ujumla.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kasekenya amekagua na kuridhishwa na ujenzi wa barabara ya Dumila –Kilosa- Mikumi KM 142, sehemu ya Rudewa-Kilosa KM 24 ambayo inajengwa na wakandarasi wazawa na kuwataka waongeze bidii ili kujenga imani kwa Serikali.

Kampuni hiyo ya Umoja-Kilosa JV inajumuisha kampuni saba za kihandisi za wazawa ikiwa ni mkakati wa Serikali wa kuwajengea uwezo wakandarasi wazawa ili kumudu kujenga miradi mikubwa na hivyo kunufaika kiuchumi na kiuzoefu.

“Barabara hii ya Dumila-Kilosa-Mikumi inayopita nje ya mbuga ya wanyama ya mikumi itakapokamilika itapunguza msongamano wa magari katika barabara ya Morogoro-Iringa na kupunguza ajali za magari kugonga wanyama katika mbuga hiyo,” amesema Mhandisi Kasekenya.

Msimamizi wa mradi huo Mhandisi Protas Mwasyoke amesema wamejipanga kuhakikisha sehemu iliyobaki ya kuunganisha kwa lami barabara ya Dumila-Rudewa –Kilosa inakamilika ifikapo Machi mwakani.

Naibu Waziri Kasekenya yuko katika ziara ya siku tatu mkoani Morogoro kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara za lami.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

CCM yamteua Pele kuwa mgombea ubunge Kwahani

Spread the loveKamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Canada yatenga bilioni 38 kutekeleza mradi ya kuinua vijana TZ

Spread the loveSERIKALI ya Canada kupitia ‘CARE International Canada’ imetenga takribani Sh...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Ujenzi kituo cha kupoza umeme Chalinze wafikia asilimia 93.7

Spread the loveKamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeeleza...

Habari Mchanganyiko

Balile ateuliwa rais wa wahariri Afrika Mashariki

Spread the loveJumuiya ya Wahariri wa Afrika Mashariki (EAES), imemchagua Mwenyekiti wa...

error: Content is protected !!