January 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Balozi Mndolwa: Msiwachukie wapinzani

Spread the love

 

BALOZI Fransic Mndolwa, ameshauri wanasiasa wa vyama vya upinzani wasichukiwe bali wapendwe, akisema wana msaada katika Taifa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Balozi Mndolwa ametoa wito huo leo Jumatatu, tarehe 6 Desemba 2021, katika Kongamano la Kitaifa la Miaka 60 ya Uhuru, lililofanyika katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), jijini Dar es Salaam.

Tanzania Bara inatarajia kutimiza miaka 60 ya uhuru, tarehe 9 Desemba mwaka huu, ambapo ilipata uhuru wake kutoka kwa Uingereza, tarehe 9 Desemba 1961.

“Bahati nzuri tunakwenda vizuri wala msiogoe vitu vidogo, ambavyo vinajitokeza, unasikia vyama vya upinzani vinalaumu huku na huko. Wala msiwachukie wapinzani, muwapende kwa sababu wanatusaidia kutuchangamsha tufikirie zaidi,” amesema Balozi Mndolwa.

Balozi huyo amesema, ili kulinda heshima ya Tanzania katika mahusiano ya kimataifa, inatakiwa iondoe tofauti zake.

“Ushirikiano wa kimataifa uimarishwe na utaimarika kama ndani ya nchi na sisi wenyewe tunakazana kutoa tofauti zetu na kujiimarisha. Hatuwezi kuwasaidia wengine wa nje kama humu ndani wenyewe tunavurugana,” amesema Balozi Mndolwa.

Akizungumzia miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara, Balozi Mndolwa amesema Watanzania wanatakiwa kuenzi amani na utulivu, uliodumu katika kipindi hicho.

“Tunao mtihani mkubwa kuhakikisha tunayamudu maisha ya amani kwa miaka mingine 60 ijayo, miaka 60 tuliweza kukaa tulivyokaa na sasa tunaanza muhula mwingine wa miaka 60,” amesema Balozi Mndolwa na kuongeza:

“Hakuna budi kuongeza juhudi kuhakikisha tunaishi kwa amani kama tulivyoishi miaka 60 iliyopita.”

error: Content is protected !!