May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Aua mwanawe akidaiwa kung’oa karanga kwa njaa

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Songwe, Janeth Magomi

Spread the love

 

MTOTO aliyejulikana kwa jina la Tofa Simchimba (5) mkazi wa kijiji cha Chizumbi kata ya Ukwile wilayani Mbozi mkoani Songwe, anadaiwa kuuawa kwa kupigwa na baba yake mkubwa Sikujua Simchimba kwa madai ya kung’oa karanga. Anaripoti Mwandishi Wetu, Songwe … (endelea).

Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Hosea Mbembela alisema mtoto huyo alipoteza maisha tarehe 1 Mei 2022 baada ya kushambuliwa kwa kung’oa karanga za baba yake huyo, Hasara Simchimba.

Mbembela alisema baada ya mtoto huyo kupigwa, alifichwa ndani kwa zaidi ya siku saba, lakini hali ilipoanza kubadilika walimpeleka zahanati ya kijiji cha Tensya, ambako mganga wa zahanati hiyo alitoa barua ya kupata matibabu hospitali ya wilaya ya Mbozi iliyoko Vwawa, baada ya kugundua anavuja damu masikioni.

“Baba yake mkubwa alimkuta aking’oa karanga kwenye shamba lake wiki mbili zilizopita, wakati mtoto huyo akiishi na bibi yake na kwamba aling’oa karanga ili kupoza njaa,” alisema Mbembela.

Mwenyekiti huyo alifafanua, kuwa baada ya mtoto huyo kufariki dunia, wananchi waligoma kuchimba kaburi wakimshinikiza mtuhumiwa achimbe.

Hata hivyo, alitokomea kusikojulikana ndipo mtendaji wa kijiji hicho kutoa taarifa kituo cha Polisi Vwawa, walifika eneo la tukio na wananchi kukubali kuzika.

Mwenyekiti alisema jamii inapaswa kuachana na ukatili ambavyo vimeendelea kukithiri, kutokana na baadhi ya watu kukosa na hofu ya Mungu, hali kadhalika amewasihi wazazi na walezi kuwalea watoto bila kujali kama si mwanao.

Baba mzazi wa mtoto huyo Joshua Simchimba alisema amesikitishwa na kitendo alichofanya kaka yake kwa kumpiga mtoto wake mpaka kupoteza maisha, hali ambayo imezua taharuki kwenye jamii.

“Nilipewa taarifa ya mwanangu kuumwa kutokana na kupigwa na kaka yangu, nami naishi wilaya ya Chunya nimefika hapa siku mbili kabla ya mtoto wangu kufariki dunia.

“Na alikuwa anaishi na bibi yake ambaye na mama yangu, hivyo kama aliona kung’olewa karanga na mwanangu kumwingiza hasara angeniambia nimlipe,” alisema Simchimba.

Jirani wa familia hiyo, Obadia Singogo alilieleza gazeti hili kuwa baada ya tukio, mtoto alipewa matibabu zahanati ya Hatensya kwa ushirikiano na uongozi wa kijiji na kuruhusiwa, lakini hali yake iliendelea kuzorota na hatimaye Mei mosi akafariki dunia.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Songwe, Janeth Magomi alikiri kuwapo tukio hilo na wanamtafuta mtuhumiwa Simchimba kwa tuhuma za kusababisha kifo hicho, huku akitoa rai kwa wananchi kuacha ukatili wa namna hiyo.

error: Content is protected !!