May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yataja hatua inazochukua kudhibiti mfumuko bei

Dk. Ashatu Kijaji

Spread the love

WAZIRI wa Viwanda Biashara na Uwekezaji, Dk. Ashatu Kijaji amesema Serikai imefanya tathimini ya upandaji wa bei za bidhaa nchini na kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutafuta vyanzo mbadala vya upatikanaji wa bidhaa hizo ili kukidhi mahitaji. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea)

Dk. Kijaji ameyasema hayo leo Ijumaa tarehe 6 Mei, 2022 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya mwaka 2022/23.

Dk. Kijaji amesema Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa bei za bidhaa muhimu hususan zile zilizoonekana kuathiriwa na UVIKO-19 sambamba na vita kati ya Ukraine na Urusi.

Ametaja hatua nyingine ni kuwaagiza wazalishaji na wasambazaji wa bidhaa muhimu kushusha mara moja bei za bidhaa walizopandisha pasipo kuendana na uhalisia wa bei ya soko na kuuza bidhaa husika kwa kuzingatia gharama halisi za uingizaji, uzalishaji na usambazaji.

Pia amesema Serikali inawaelekeza wazalishaji wa bidhaa muhimu kuzalisha na kusambaza bidhaa husika kulingana na uwezo wa viwanda uliosimikwa; wauzaji na wasambazaji wa mbolea zenye bei elekezi wahakikishe wanazingatia bei zilizopangwa na Serikali.

“Wale wote watakaokiuka watachukuliwa hatua kali za kisheria, ikiwa ni pamoja na kufutiwa leseni za biashara.

Dk. Kijaji amesema Tume ya Ushindani (FCC) imeelekezwa kufuatilia kwa karibu mwenendo wa biashara wa bidhaa muhimu ambazo katika tathmini iliyofanyika zimeonesha kuathirika zaidi na upandaji wa bei.

“Serikali imeendelea kushawishi na kuvutia Wawekezaji wa ndani na nje kwenye uzalishaji wa mazao ambayo tumekuwa tegemezi kwa kiwango kikubwa kutoka nje ya nchi ikiwa ni pamoja na mafuta ya kula, sukari na ngano. Amesema lengo ni kupata uzalishaji unaotosheleza mahitaji ya soko letu la ndani na hatimaye kuuza nje.

error: Content is protected !!