Friday , 26 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Askofu Shoo alilia amani, upendo Tanzania
Habari Mchanganyiko

Askofu Shoo alilia amani, upendo Tanzania

Askofu Frederick Shoo, Mkuu wa Kanisa la KKKT
Spread the love

 

MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo, ametoa mwito kwa Watanzania kuwa na imani thabiti badala ya inayolegalega, ili kulinda upendo, amani, haki na usawa katika jamii. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Askofu Shoo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) alitoa mwito huo mwishoni mwa wiki, akizungumza na waumini wa Kanisa na maaskofu wa CCT na viongozi wa Serikali kwenye Ibada maalumu ya kuadhimisha sikukuu ya umoja huo mkoani Kilimanjaro.

“Katika siku za hivi karibuni, tumeshuhudia mmomonyoko mkubwa wa maadili katika jamii, pia viongozi wengi hata wa Kanisa wakiwa na uchu wa madaraka na hata kumsahau Mungu.

“Hii yote inatokana na kuwa na imani inayolegalega, imani baridi, nawasihi Watanzania wote tuwe na imani thabiti, imani moto badala ya baridi,” alisema Askofu Shoo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa Jumuiya hiyo.

Askofu huyo aliendelea kufafanua, tatizo la mmomonyoko wa maadili, kukosekana kwa haki za watoto, wanawake na vijana ni matunda ya kutokuwa na imani thabiti, hivyo aliwataka viongozi wa dini kuendelea kusimamia haki, usawa wa kijinsia, amani na upendo wa kweli katika jamii inayowazunguka.

“Kanisa letu linahitaji sana umoja, lakini umoja wetu unaweza kubaki wa maneno kama hatutazingatia maneno tuliyousiwa na Yesu Kristo, hivyo ninawasihi wanachama wa CCT kuendelea kukaa katika umoja wetu kwa kuzingatia upendo, haki na amani,” alisisitiza Askofu Shoo katika mahubiri yake.

Aidha, alisema wapo baadhi ya viongozi wa dini kwa sasa, wamekuwa wakihangaika na mtu mmoja, badala ya kujikita katika imani yao kwa Yesu Kristo, watu hao wameanza kujikita kwa Askofu Shoo.

“Kwenye shina la mti kuna matawi na hayo matawi, yanatokana na huo mti mkubwa, hakuna matawi yaliyojikita katika matawi bila kutokea kwenye shina la mti mkubwa.

“Sasa kuna baadhi ya viongozi wa dini badala ya kujikita katika imani yao kwa Yesu Kristo, sasa wameanza kujikita kwa Askofu Shoo, hivyo kama Kanisa, tuna wajibu mkubwa sana wa kuendelea kuhubiri Injili ili nyoyo za watu hao, igeuzwe na watu wachukie maovu, watu waogope maovu na wawe tayari kukemea maovu,” alisema Askofu Shoo.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Steven Kagaigai aliwapongeza viongozi wa dini kwa kuendelea kudumisha upendo, haki na amani nchini kwa ustawi endelevu wa jamii.

“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, inatambua mchango mkubwa wa viongozi wa dini katika kudumisha upendo, haki na amani kwa Watanzania wote kwa maendeleo na ustawi endelevu wa jamii,” alifafanua Kagaigai.

Aidha, Mkuu huyo pamoja na kutoa salamu za Rais Samia, pia alitoa mwito kwa viongozi wa dini nchini kuendelea kukemea matendo maovu katika jamii, ikiwamo tatizo kubwa la mmomonyoko wa maadili.

“Kazi yenu mnayoifanya viongozi wa dini ya kuhubiri amani, inatusaidia sana sisi kama viongozi wa Serikali katika kusimamia maendeleo, badala ya kukaa na kuhangaika na usalama, wapo watu wanaotusaidia katika hilo,” alisema Kagaigai.

Katika hotuba yake hiyo, aliwasihi maaskofu kuhakikisha, kwamba wanaendelea kukemea matukio ambayo kwa kipindi hicho, yameonekana kukithiri katika jamii hususan ya ulawiti na ndoa za jinsia moja.

“Baba zangu maaskofu, mna kazi kubwa kweli, sasa hivi kuna matukio mengi, ambayo nina uhakika kama nyoyo za wanadamu wangekuwa wanaweza kama dhamira ya mkusanyiko huu ulivyo leo, baadhi ya matukio yasingekuwa yakitokea.

“Sasa hivi kuna makosa ambayo kwangu mimi hapa kanisani siwezi kuyatamka, ni makosa ambayo mimi nilikuwa mwendesha mashitaka toka zamani, nilikuwa nakutana nayo huko mahakamani, kule nilikuwa na ruksa ya kuyatamka, kama wakili na mwendesha mashitaka,” alisema na kuongeza:

“Lakini ndani ya Kanisa naomba nisiyatamke, ni matukio ambayo kwa kweli najiuliza yanatoka wapi. Mbona miaka yote ya nyuma hayakuwapo?

“Baba Askofu naomba mimi nanyi tutafute namna ya kuyafanyia kazi, kwa sababu kwa kweli inasikitisha sana, kwanza kwangu naona kutamka kama ni unyanyasaji, nadhani kuna neno zaidi linatakiwa litumike, sasa nadhani kwa maoni yangu, lingetumika kama mauaji kabisa.”

Aliendelea kusema: “Makosa haya yanaharibu ustawi wa nchi, utamaduni, mila na desturi za nchi, na sijui tumekosea wapi…Baba Askofu huko twendako tutakosa waumini humu makanisani.

“Tutakosa watoto wa kulea, waumini wa kuhubiri Injili watakosekana, lakini pia hata familia zitakosa watoto na huu ndio utakuwa mwisho wa kila kitu.

“Nadhani kitu tunachotakiwa kufanya sasa, ni kurejesha maadili ya nchi na pengine tungeanza na familia zetu, iwe ni jukumu la kila mzazi kuhakikisha malezi katika familia yanazingatiwa zaidi,” alisema.

“Pia, niwaombe viongozi wa dini mwendelee kukemea vitendo viovu katika jamii, likiwamo tatizo la mmomonyoko wa maadli kwa vijana na hata kwa viongozi wa umma, likiwamo tatizo la ushoga,” alisisitiza Mkuu huyo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Wakili: Ukimpa zawadi mwenza marufuku kumpora hata mkiachana

Spread the love  WANANDOA na watu waliko kwenye mahusiano ya kimapenzi, wamekumbushwa...

Habari Mchanganyiko

Majaliwa: Mvua zimesababisha vifo vya watu 155, kuendelea hadi Mei

Spread the love  WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mvua kubwa za El-Nino...

Habari Mchanganyiko

Exim Bank yatoa  vitanda kwa shule ya Jeshi la Polisi Moshi

Spread the love  BENKI ya Exim imekabidhii  seti ya vitanda kwa Shule...

Habari Mchanganyiko

NBC yakabidhi vitanda Shule ya Polisi Moshi

Spread the loveBenki ya NBC imekabidhi msaada wa vitanda 28 kwa Shule...

error: Content is protected !!