ASKOFU Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Yuda Thadeus Ruwa’ichi, amewataka watu waishi duniani kama wapiti njia, huku akiwahimiza kutenda yaliyo mema kwa kuwa ipo siku watadaiwa hesabu za matendo yao mbele ya Mungu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Askofu Ruwa’ichi ametoa wito huo leo Jumanne, tarehe 24 Agosti 2021, katika Kituo cha Hija cha Pugu, mkoani Dar es Salaam, akihubiri kwenye adhimisho la misa takatifu ya mazishi ya Padri Paul Peter Haule.
“Kila mmoja wetu anayehudhuria adhimisho hili la misa takatifu ni mpita njia, wote tuko wapita njia. Basi tuishi kama wapita njia na wasafiri. Tuishi kama watu ambao siku moja tutadaiwa hesabu ya ukarani wetu,” amesema Askofu Ruwa’ichi.
Askofu Ruwa’ichi ameongeza “tuwe tayari, sababu iko siku Mungu atatutaka tuitoe hesabu ya ukarani wetu na ukarani wetu ni maisha tuliyopewa tuyaishi, ushuhuda tuliyokabidhiwa tuufanye, utume na wajibu tuliokabidhiwa.”
Padri Haule aliyefariki dunia tarehe 18 Agosti 2021, kwenye Hospitali ya Kardinali Rugambwa, Ukonga, akipatiwa matibabu, alikuwa Paroko Msaidizi wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Mtakatifu Petro, Oysterbay mkoani Dar es Salaam.
Akimzungumzia marehemu Padri Haule, Askofu Ruwa’ichi amesema alitumikia nafasi hiyo kwa zaidi ya miaka 20.
“Hayati Paul alianza safari yake ya ufuasi na ushuhuda pale alipobatizwa, akaukumbatia wito wa upadri. Ameishi upadri kwa miaka inayokimbilia, haijafikia 30 lakini inakimbilia huko, tumshukuru Mungu kwa miaka ya upadri aliyomjalia,” amesema Askofu Ruwa’ichi.
Askofu Ruwa’ichi amesema, Padri Haule alijiandaa na safari yake ya kwenda mbinguni, kwa kuwa kabla hajapelekwa hospitalini kwa ajili ya matibabu, alipata sakramenti ya kitubio.
“Padre Paul alijindaa, kabla ya kwenda hospitalini alijiandaa kwa kupokea maskramenti. Sakramenti ya kitubio na sakramenti ya ukaristi, amekimbilia kiti cha huruma ya Mungu na kuomba huruma ya Mungu,” amesema Askofu Ruwa’ichi na kuongeza:
“Akamuomba Mungu aliyemjalia moyo wa kujifahamu na kujiamini sana, amsamehe yale yaliyopungua katika ufuasi na majitolea yake, amjalie mapunziko ya milele pamoja na wateule wake.”
Leave a comment