May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Askofu Bagonza: Ulimwengu umejaa unafiki, kujipendekeza

Askofu Benson Kagonza, KKKT Dayosisi ya Karagwe

Spread the love

 

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera, Dk. Benson Bagonza, amesema ulimwengu umejaa unafiki, woga, kujipendekeza. Anaripoti Rgina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Kiongozi huyo wa kirogo ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, tarehe 28 Juni 2021, kupitia tanzia yake aliyoitoa katika ibada ya kuuaga mwili wa Padri Privatus Karugendo, iliyofanyika Kanisa Katoliki la Roho Mtakatifu, Segerea jijini Dar es Salaam.

Privatus Karugendo alikuwa mwandishi na mchambuzi wa siasa katika gazeti la Mwananchi na Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani (DW).

Kwenye msiba huo, Askofu Bagonza amewataka

Watanzania kujiepusha na vitendo vitakavyoshusha heshima zao katika jamii.

“Naadhimisha maisha ya Father Privatus katika ulimwengu uliojaa unafiki, woga, kujipendekeza na uwongo mwingi, kumpata rafiki unayeweza kumuamini wakati wote ni jambo la thamani sana. Father Privatus hakuwahi kuniachia mashaka wakati wote nilipoongea naye.

“Kuna wakati ningesikia mambo kuhusu yeye nisiamini, kisha nikaja kumuuliza nikitamani moyoni aseme si kweli, lakini yeye kwa moyo mweupe alisema ni kweli. Alikuwa mkweli mpaka anakera,” amesema Askofu Bagonza.

Askofu Bagonza amewaomba Watanzania wamuenzi Padri Privatus, kwa kufuata nyayo zake kwa kuwa wakweli.

Askofu Bagonza amesema, wako baadhi ya watu wanapoteza heshima zao kwa kuyumbishwa na vitu vidogo, lakini Padri Privatus enzi za uhai wake, hakuwa mtu wa namna hiyo.

“Maisha ya namna hiyo ni ya kuadhimisha yanapotoweka. Amekufa na ukweli wake unaoudhi. Wako watu ambao kwa sababu zisizo nzito, wanapoteza heshima kwa kuyumbishwa na vitu vidogo.

“Kwa kuwa wote tutakufa, ni faida kufa kwa kusimamia unachokiamini, nawaalika tuadhimishe mazuri yote aliyoyasimamia Father Privatus,” amesema Askofu Bagonza.

Wakati huo huo, Askofu Bagonza ametoa wito kwa viongozi wa kiroho kuacha kuwahukumu watu.

“Ndugu zanguni, hata kwetu ambako daraja hili la kichungaji si Sakramenti, mambo ya wito si mepesi. Punguzeni hukumu, kanuni ya kwetu hata kama si Sakramenti inasema, “kuingia humo ni vigumu.

“Ukiishaingia, kutoka ni kugumu. Ukiishatoka, kurudi tena ni kugumu”. Tusichoke kuombeana na kuwatia moyo waliomo,” amesema Dk. Bagonza.

Ametoa wito huo, akikumbushia namna alivyomsaidia Padri Privatus, alipokuwa na mgogoro na Kanisa lake la Katoliki, Jimbo la Rulenge mkoani Kagera.

Enzi za uhai wake, Privatus alikuwa Padri kwa miaka takribani 20, ikiwemo katika Jimbo Katoliki la Rulenge, Parokia ya Buziku mkoani Kagera, alikokuwa Paroko Msaidizi. 2009, Karugendo alivuliwa upadri kwa tuhuma za kukiuka maadili ya Kanisa Katoliki.

Akikumbushia mgogoro huo, Dk. Bagonza amesema alikuwa miongoni mwa watu waliomsaodia Padri Privatus, alipofukuzwa katika kanisa hilo.

“Katika mgogoro wa kitume na kanisa lake alikimbilia kwangu. Akisindikizwa na baadhi ya mapadre kwa siri usiku, alibisha hodi kuomba hifadhi.

“Nilifungua milango akakaa kwetu, nikamwambia hasira yako ikiisha urudi nyumbani. Ukitaka msaada wa kukupeleka nyumbani uniambie. Miaka mitatu tulikaa naye akitafakari,” amesema Askofu Bagonza.

Askofu Bagonza amesema “katika tafakari hiyo aligundua ndani yake wito mwingine, akaufuata kwa hiari na furaha ya moyo wake.”

error: Content is protected !!