Monday , 11 December 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Alichozungumza Zitto Kabwe leo
Habari za Siasa

Alichozungumza Zitto Kabwe leo

Spread the love

Serikali Imevuruga Zao La Korosho, Imeshindwa Kulinda Ustawi na Usalama wa Raia

A: Utangulizi

Jana, Kamati ya Uongozi ya Chama cha ACT Wazalendo, ambayo ni Kikao cha Kikatiba ambacho wajumbe wake ni Viongozi wote wa juu wa chama chetu ilikutana katika kikao chake cha kawaida kujadili hali ya chama na hali ya nchi kwa ujumla.

Pamoja na mambo mengine, pia Kamati ya Uongozi ya ACT Wazalendo ilitathmini mwenendo wa usalama wa nchi na hali ya Uchumi, hususan masuala yanayohusu wakulima na hasa uzalishaji wa zao la Korosho, zao linaloongoza kwa kuingizia nchi yetu Mapato ya Fedha za kigeni kuliko mazao yote kwa ujumla. Hivyo leo, tumewaita hapa kwa niaba ya Kamati ya Uongozi ili kupitia nyinyi tufikishe mawazo, mapendekezo kwa wanaACT Wazalendo pamoja na Watanzania kwa ujumla juu ya masuala hayo mawili.

A: Hali ya Usalama ni Mbaya

1. Nchi Imejaa Khofu

Wiki ijayo itatimia miaka mitatu ya utawala wa Serikali ya awamu ya Tano, utawala ambao imedhihirika bayana kuwa silaha yake kubwa ya kuendesha nchi ni kwa kuwatia khofu wananchi. Kitu kimoja ambacho utawala huu unaweza kujivunia baada ya miaka mitatu ni khofu kutamalaki kila upande. Maana imegusa mtu mmoja mmoja, imegusa vikundi vya kijamii kama vyama vya siasa (kikiwemo chama tawala), waandishi wa habari, wafanyabiashara, wawekezaji, wakulima, wafanyakazi, asasi za kiraia, wanafunzi, wanasanaa, wavuvi, wanasiasa nk. Kila sehemu nchini kumejaa khofu!

Tanzania katika miaka mitatu ya Rais Magufuli imekuwa ni nchi ya watu kutekwa, kushambuliwa kwa risasi na ‘Watu Wasiojulikana’, kuokotwa miili yao ikiwa imeuawa, kuwekwa kwenye viroba na kutupwa kwenye fukwe za bahari na mito yetu. Ni jambo la kawaida sasa mtu kutekwa au askari kufyatulia risasi makumi na mamia ya wananchi.

Tunayo mifano iliyo wazi, Msaidizi wa Kiongozi wa Upinzani Bungeni, ndugu Ben Saanane, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Kibondo na Diwani wa kata ya Kagezi, ndugu Simon Kanguye, na Mwandishi wa Habari za uchunguzi wa gazeti la kila siku la Mwananchi, ndugu Azory Gwanda wamepotezwa, huku watuhumiwa namba moja wakiwa ni vyombo vya dola.

Mpaka sasa hakuna yeyote aliyekamatwa kufuatia tukio la kumpiga risasi nyingi kwa lengo la kumuua Mbunge wa jimbo la Singida Mashariki, ndugu Tundu Lissu, pmaoja na shambulizi kutokea ndani ya eneo la Bunge. Serikali inadhani kwa kuchagua kukaa kimya, damu ya watu hawa itapotea kimyakimya? Haiwezekani!

Miaka hii mitatu tumeshughudia Mamia ya wananchi wenzetu wakiuawa na kupotezwa katika eneo la MKIRU (Mkuranga, Kibiti na Rufiji). Majuzi, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Siro, akizungumzia sakata la kutekwa kwa Mohammed Dewji alitoa dondoo kidogo kwamba walilazimika kutumia nguvu kule MKIRU kuwaondosha watu aliodai sasa wamekimbilia Msumbiji. Kwa mara ya kwanza IGP Sirro alikiri kuwa kuna watu wengi waliuwawa.

ACT Wazalendo Tutafanya Nini?

Chama chetu kimepaza sauti juu ya masuala haya ndani ya miaka hii mitatu, pamoja na Serikali kuamua kutokueleza ukweli au kuchukua hatua kuyazuia, bado hatutakaa kimya. Tutafanya yafuatayo:

• Tutaendelea kusisitiza kuundwa kwa Tume ya Kutafuta Ukweli wa Mauaji ya MKIRU, na kupigania watu wote waliochukuliwa misikitini katika Wilaya za Kilwa na Lindi warejeshwe wakiwa hai ama ndugu na jamaa zao wawlezwe kama wameuawa.

• Tutaendelea kuhamasisha umma wa watanzania uendelee kushikamana kuwapigania Azory Gwanda, Simon Kanguye na Ben Saanane mpaka pale watakapopatikana au ukweli juu yao kujulikana. Ukweli wa mambo ni kuwa Mfanyabiashara Mohammed Dewji asingepatikana bila nguvu ya umma. Watanzania wasingepaza sauti naye angepotezwa tu kama Saanane, Kanguye na Azory.

Watanzania waendeleze mshikamano huu kwa watu wengine ili kukomesha kabisa vitendo hivi vya utekaji na watu kupotea.

• Tutaendelea kuitaka Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) ijitathmini. Kwa muda mrefu tumepigania mageuzi ya kimfumo na ya kiuendeshaji ndani ya TISS. TISS si usalama wa CCM wala serikali. TISS ni usalama wa taifa. Yanapotea matukio makubwa yanayotishia usalama wa taifa letu, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa anapaswa kuwajibika. TISS ikikaa kimya huku matukio yanayotishia usalama wa wananchi yakikita mizizi, hisia kwamba ‘WATU WASIOJULIKANA ni TISS zitapata uhalali. Wakati umefika kwa Wazalendo ndani ya TISS kuamka na kurejesha hadhi ya chombo hicho.

• Tutaendelea kuyasema bungeni, na katika kila pahala tutakapopata nafasi ya kupaza sauti yetu. Tutafanya hilo la kupaza sauti pamoja na kutambua unyeti wa usalama wa nchi yetu, lakini tukipinga njia ya kuua, kuteka, kupoteza na kutesa wananchi wenzetu kwa kigezo cha kulinda usalama wa nchi, ni njia inayowajaza khofu tu wananchi. Khofu ni ishara ya kukosa uhuru, na bila uhuru watu hawawezi kusemwa kuwa wapo salama. Pia, bila uhuru hakuna maendeleo.

2. Wananchi Zaidi ya 100 Wanadaiwa Kuuawa Uvinza

Wiki iliyopita yalitokea mauaji ya Askari wa jeshi la Polisi katika eneo la mto Malagarasi, kijiji cha Mpeta wilayani Uvinza, mkoani Kigoma, ambapo Mkuu wa Kituo cha Polisi Nguruka aliuwawa na wanaodaiwa kuwa ni wananchi. Chama chetu kilitoa salaam za rambirambi kwa IGP kufuatia mauaji hayo, kikilaani na kikitaka uchunguzi ufanyika na wahalifu wakamatwe na kufikishwa mahakamani.

Tumekuwa tukifuatilia kwa kina yote yanayojiri huko Uvinza tangu kuuawa kwa askari Polisi wetu. Tunasikitika kusema kuwa taarifa tunazozipata kutoka Uvinza zinaogofya mno, kwani tunaambiwa kuwa wananchi zaidi ya 100 wa Kabila la Wanyantuzu wamepoteza maisha kwa kupigwa risasi na Polisi, wengine wakisemwa kuuawa hata wakiwa kwenye matibabu hospitalini baada ya kujeruhiwa kwenye purukushani na jeshi la polisi.

Jeshi la Polisi limekalia kimya suala hili, pamoja na IGP kutembelea eneo hilo la maafa. Haiwezekani kamwe tukio kubwa namna hii kutokea halafu Serikali ibaki kimya bila kutoa maelezo yeyote kwa Wananchi. Uchunguzi wa kina unapaswa kufanywa ili kutambua nini kimetokea pale Mgeta.

ACT Wazalendo Itafanya Nini?

Kwa sasa tunaitaka Serikali ieleze nini hasa kimetokea Mgeta, maelezo hayo yawe ya kina na yawe ya ukweli. Chama chetu kinaendelea kukusanya majina na taarifa za wote wanaodaiwa kuuawa, na kitaweza wazi taarifa husika.

B: Serikali Iwajibike kwa Kuchezea Suala la Korosho

Kwa wiki mbili sasa mjadala ni juu ya bei ya zao la Korosho. Wakati wa Bunge la Bajeti mjadala ulikuwa mkubwa pia, hasa juu ya hatua ya Serikali kudhulumu fedha za Wakulima wa Korosho zaidi ya shilingi 200 bilioni zilizopaswa kutolewa kwa ajili ya kusaidia uendezwaji wa zao hilo (kurahisisha usambazaji wa pembejeo kama madawa na viatilifu vingine, uendeshaji wa chuo cha Utafiti Naliendele na kujenga mazingira ya kuongeza ubanguaji nchini ili kuongeza thamani ya korosho kwa wakulima wetu na hivyo kuongeza uzalishaji na kipato chao).

Serikali kupitia Bodi ya Korosho huweka bei elekezi ya kuuzwa kwa zao hilo, na kwa mwaka huu bei elekezi ni Shilingi 1,550. Bei hii iliwekwa kwa kigezo kuwa Mkulima alinunua dawa ya Salfa (sulphur) kwa shilingi 32,000 kwa mfuko, hivyo ikikadiriwa kuwa gharama za uzalishaji kwa kila kilo moja ya korosho kwa mkulima ni shilingi 1,350, na hivyo kwa hiyo bei elekezi mkulima anatarajiwa kupata faida ya shilingi 200 kwa kila kilo moja atakayouza.

Ukweli ni Kwamba mwaka 2018 kulikuwa na ulanguzi mkubwa wa Salfa, na mkulima alinunua dawa mpaka shilingi 84,000 kutoka shilingi 14,000 iwapo fedha za Ushuru wa Korosho (exports levy) zingetumika kama ilivyopaswa na Serikali isingezidhulumu.

Katika minada minne ya TANECU (Tandahimba na Newala), MAMCU (Mtwara, Masasi na Nanyumbu), RUNALI (Ruangwa, Nachingwea na Liwale) na ule wa Lindi Mjini wakulima wamegoma kuuza korosho zao kwa bei ya juu ya shilingi 2700 (zaidi ya shilingi 1150 kutoka bei elekezi) kwa sababu bei elekezi haikuwa halisi. Zaidi Wakulima wanasema kuwa Serikali iliwaahidi kuwa bei ya kilo moja ya Korosho itafikia shilingi 5,000 kwa mwaka huu kwa sababu kuna wanunuzi kutoka Marekani.

Maamuzi Mabaya ya Serikali Yatashusha Uzalishaji

Mwaka 2017 Tanzania ilizalisha Korosho tani 331,000 Sawa na ongezeko la 96% ya uzalishaji wa 2016. Kwa uzalishaji huo nchi yetu ilipata fedha za kigeni Dola 542 milioni, Sawa na ongezeko la 100% kutoka Dola 271 milioni za mwaka 2016. Bila Serikali kuingilia mfumo wa Korosho Mwaka 2018 tungepaswa kuzalisha tani 500,000 za Korosho na hivyo ama kuongeza Mapato ya fedha za kigeni au hata kuzuia kuporomoka kwake.

Bahati mbaya Sana Mwaka 2018 Serikali ikaamua kuwanyanganya Wakulima fedha zao za export levy, shilingi 200 bilioni, na hivyo kuathiri upatikanaji wa Salfa kwa wakulima wa Korosho. Inakadiriwa kwamba uzalishaji unaweza kuporomoka kwa 40%. Habari za ndani zinasema kuwa uzalishaji wa Korosho mwaka 2018 utakuwa chini uzalishaji wa mwaka 2012 ambapo zilishalishwa tani 131,000 tu.

Kutokana na uzalishaji kwenda chini na bei nayo kushuka, wananchi na serikali wote watapungukiwa mapato. Wananchi watapata mapato chini ya shilingi 4,000 kwa kilo waliyouza Mwaka jana na Taifa litapata dola za kimarekani $209m tu kwa bei ya sasa ya soko la dunia ya dola 1.6 kwa kilo.

Anayepasa kubeba mzigo wa lawama kwenye hili ni Serikali ambayo imekwapua fedha za export levy ambazo zingetumika kwenye utafiti, kununua pembejeo na uendeshaji wa tasnia nzima ya zao la korosho na hivyo kukuza uzalishaji. Kukwapua fedha za export levy ilikuwa ni sawa na mkulima kula mbegu! Tunapotafakari uwezekano wa kushuka kwa uzalishaji uliosababishwa na kukosa pembejeo, tukumbuke kumuwajibisha aliyekula mbegu.

Udhibiti wa Bei

Uchumi wa nchi nyingi za Kiafrika bado una sifa ya uchumi wa kikoloni ambapo sehemu kubwa ya malighafi yalisafirishwa kwenda nje. Hadi sasa, zaidi ya miaka 60 tangu uhuru wa taifa letu, bado tunasafirisha malighafi ya viwandani kwenda Barani Ulaya, Asia na Amerika. Kwa korosho hali ni hiyohiyo. Kwa msingi huo, kwa sehemu kubwa bei hudhibitiwa na kupangwa nje.

Mwaka 2016/2017 bei ya korosho ilivyopanda tulipoieleza Serikali ya CCM kwamba ongezeko hilo la bei ya korosho hadi kufikia 4000 na zaidi kwa kilo halikutokana na mikakati ya ndani bali hali ya mahitaji ya nje hasa nchini Vietnam tulionekana wazushi na wenye wivu.

Lengo letu ilikuwa ni kuiamsha serikali ijibidiishe kuimarisha uzalishaji na ubanguaji wa korosho nchini ili kutumia fursa ya bei ya korosho kupanda kuongeza mapato ya serikali na wananchi. Hakuna aliyetusikiliza. Rais mwenyewe alitamba kwamba amesababisha bei ya korosho kupanda hadi wakulima wa korosho wananywesha mbuzi soda.

Kabla ya msimu wa korosho kuanza, kutokana na ufuatiliaji wetu, tuliijulisha serikali kwamba kuna uwezekano wa bei ya korosho kushuka kiasi kutokana na mwenendo wa soko la dunia. Tuliwataka wajifunze kwa Ivory Coast ambako bei imeshuka kwa zaidi ya nusu. Badala ya kuipokea taarifa hiyo, tuliitwa wazushi na kwamba bei ya korosho mwaka huu itapanda zaidi kuweza kufikia 5000. Sasa tunaidai bei ya 5000 ambayo serikali iliahidi, inaruka kwamba bei inashuka kutokana na soko la dunia!

CCM na serikali yake ni mabingwa wa hadaa. Bei ikipanda ni wao wameipandisha. Bei ikishuka, si wao, ni soko la dunia au anatafutwa mchawi kutupiwa lawama kama wanavyofanya sasa kwa Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho.

Unawezaje kuwalaumu wafanyabiashara na Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho wakati wewe mwenyewe umeweka bei elekezi ya shilingi 1550 kwa kilo kwa madai ya kwamba mkulima atapata faida ya Tsh. 200 halafu mfanyabiashara ananunua Tsh. 2700 kwa kilo unasema anamnyonya mkulima? Mnyonyaji ni mfanyabiashara au wewe uliyepanga bei elekezi?

Vile vile tuliishauri Serikali kwamba wakati bei ni kubwa sehemu ya fedha za exports levy zitumike kujenga mfumo wa hifadhi ya jamii kwa Wakulima wa Korosho ambapo Wakulima wangepata bima ya afya, kuweka akiba na muhimu zaidi fao la bei (price stabilization) ili kukabili misukosuko ya soko la dunia. Serikali haikutaka kusikia ushauri huu na leo wanahangaika. Ingekuwa wamefanya tulivyoshauri Serikali ingeweza kufidia kushuka kwa bei kwa kuwalipa Wananchi kiasi cha fedha ambacho bei imeshuka ili kuwawezesha kukabili gharama za uzalishaji.

Tunapendekeza;

– Serikali inunue Korosho yote kwa wakulima ili kuwalinda na bei ndogo kutokana na kushuka kwa bei ya korosho kwenye soko la dunia. Kwa vile malengo ya serikali hayatakuwa kupata faida bali kufidia gharama za manunuzi, bei ya korosho haitashuka sana. Kisha Serikali iwauzie wanunuzi kwa namna wanaona inafaa. Lengo hapa ni kumlinda Mkulima kwa kumpa bei nzuri.

– Tunarudia tena rai yetu kwa serikali kuanzisha fao la bei kwenye mfumo wetu wa hifadhi ya jamii ili kumlinda mkulima na kushuka kwa bei.

– Tunamtaka Rais Magufuli awaombe radhi Wabunge wa mikoa inayolima korosho kwa kitendo chake cha kuwatisha na kuwadhihaki waliposimama kidete kupigania kutokukwapuliwa kwa fedha za export levy ambazo zingetumika kwenye uendeshaji mzima wa tasnia ya korosho na hivyo kukuza uzalishaji na kuviwezesha chombo ambacho kinasimamia soko la korosho ambacho ni Bodi ya Korosho.

– Tuongeze kasi kwenye ujenzi wa viwanda vya ubanguaji wa korosho ili kuongeza thamani yake badala ya kuendelea kusafirisha korosho ghafi

Mwisho, tunarudia rai yetu ya mara zote kuwa kuongoza ni maarifa, si mabavu. Serikali iwe tayari kupokea mawazo chanya kwa ustawi wa taifa letu. Tanzania ni yetu sote

Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo
Oktoba 28, 2018
Dar es salaam

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Jaji Kiongozi akerwa wananchi kukosa imani na mahakama

Spread the loveWATENDAJI wa Mahakama ya Tanzania, wametakiwa kuweka mikakati itakayosaidia kurejesha...

BurudikaHabari za Siasa

Samia amchangia Professa Jay mil. 50, Chadema, wasanii wamwaga manoti

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amechangia kiasi cha Sh 50 milioni...

Habari za Siasa

Biteko: Samia ni muumini wa maridhiano sio kwa kuigiza

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Mpango: Sitakufa bali nitaishi

Spread the loveMAKAMU  wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk....

error: Content is protected !!