May 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Akamatwa kwa kusambaza taarifa ‘JPM mgonjwa’

Spread the love

CHARLES Majura (35), fundi simu na mkazi wa Dar es Salaam, anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni, kwa madai ya kusambaza taarifa kwenye mitandao ya kijamii, kuwa Rais John Magufuli ni mgonjwa. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumamosi tarehe 13 Machi 2021, na Kamanda wa Jeshi la Polisi Kinondoni, Ramadhani Kingai wakati akizungumza na vyombo vya habari Dar es Salaam.

“Watu wanaosambaza taarifa za uongo katika mitandao ya kijamii, kwamba mheshimiwa rais ni mgonjwa, taarifa ambazo zinaleta hofu kwa wananchi, kwa taarifa hizi tumeanza kuzifanyia kazi.

“Tulifanikiwa kumkamata  Majura,  ambaye yeye alikuwa kinara wa kusambaza taarifa hizi,” amesema Kamanda Kingai.

Amesema, Majura alikamatwa tarehe 11 Machi mwaka huu, na kwamba anaendelea kuhojiwa juu ya madai yanayomkabili.

 

Kamanda huyo amesema, baada ya mahojiano hayo kukamilika na ushahidi kukusanywa, mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani.

“Tulimkata ili aweze kushughulishwa kisheria, tunaye na tunaendelea na mahojiano naye, tunakusanya ushahidi kuhakikisha anapelekwa kwenye mahakama kwa ajili ya kuhudumia kosa ambalo amelitenda,” amesema Kamanda Kingai.

Amesema, Jeshi la Polisi bado linaendelea kufuatilia taarifa za watu wengine wanaotia hofu wananchi kwa kusambaza taarifa za uzushi mitandaoni.

Akiwa ziarani Njombe jana tarehe 12 Machi 2021, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema, Rais Magufuli ni mzima wa afya na anaendelea na majukumu yake.

Waziri Majaliwa aliwatoa hofu Watanzania akisema kwamba, Rais Magufuli haonekani hadharani kwasababu kuna majukumu anayoyatekeleza.

error: Content is protected !!