October 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Agizo la kwanza la Nondo baada ya kukwaa Uenyekiti ACT

Spread the love

ABDUL Nondo, Mwanaharakati wa haki za binadamu nchini, amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya Chama cha ACT-Wazalendo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Nondo amechaguliwa kushika wadhifa huo jana tarehe 9 Machi 2020, katika uchaguzi wa viongozi wa ngome hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya matokeo kutangazwa, Nondo aliwataka vijana wa ACT-Wazalendo kuwa wamoja kwa ajili ya kujenga chama hicho.

Wakati huo huo, Nondo  amewaomba vijana wa ACT-Wazalendo kujitokeza kwa wingi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kusikiliza hukumu ya viongozi wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), inayotarajiwa kutolewa leo.

“Pia tunaomba vijana wote wa ACT wazalendo na viongozi  kuhudhuria na kufika Mahakama ya Kisutu leo kuanzia saa 3 asubuhi, kwani ni siku ya hukumu ya kesi dhidi ya viongozi wakuu wa chama cha Chadema,” ameagiza Nondo na kuongeza:

“Lengo ni kuonesha umoja na mshikamano kwani changamoto wanazopitia Chadema ndio changamoto ambazo viongozi wetu wa chama na chama chetu tunapitia. Hivyo naomba tujitokeze kwa wingi, pia kuzidisha maombi kwa viongozi wote wa CHADEMA, Mungu azidi kuwasimamia dhidi ya hujuma yeyote.”

Katika uchaguzi huo, Khadija Mohammed amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ACT-Wazalendo Zanzibar , wakati Seleman Misango akishinda nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa ngome hiyo Bara.

error: Content is protected !!